Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kunipa nafasi jioni ya leo niweze kusema machache juu ya hotuba ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Naibu Waziri wote wawili; ndugu yangu Mheshimiwa Nditiye pale na Mheshimiwa Kwandikwa wanafanya kazi kubwa sana. Namini kabisa Mheshimiwa Rais amechagua watu sahihi kwa ajili ya kumsaidia kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali hususan Wizara hii nimeona wametukumbuka juu ya barabara ya kutoka Handeni – Kibirashi – Kijungu - Nchemba

- Singida, ina kilometa 460. Barabara hii mara nyingi nimekuwa nikiizungumzia sana kwamba ina umuhimu mkubwa sana. Bahati nzuri kwamba barabara hii ndipo ambapo bomba la mafuta linalotoka Uganda hadi Tanga linapita. Nimeona wametutengea shilingi bilioni moja hapa, lakini niombe Waziri mwenye dhamana na uongozi mzima wa Wizara hii watutafutie pesa kwa sababu wanasema wanatafuta pesa lakini nasema watutafutie pesa wajenge barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ukiacha suala la mafuta ina shughuli nyingi sana za kiuchumi kwa sababu inaunganisha mikoa minne kwa maana ya Mkoa wa Tanga, Manyara, Dodoma na Singida. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, afanye atakachoweza ahakikishe kwamba anatupatia pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni kwamba barabara hii itakuwa na umuhimu kwa sababu upanuzi wa Bandari ya Tanga unakwenda sambamba na hilo. Kwa hiyo, mizigo ambayo itakwenda bandarini pale itatumia barabara hiyo, kwa hiyo, barabara hii ina umuhimu mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, naomba nizungumzie sana suala la reli ya kutoka Tanga – Moshi - Arusha - Musoma. Reli hii ni muhimu sana kwa sababu pia inalenga kuinua kipato cha nchi hii. Naamini kabisa hata mafuta yale yatakayokuwa yanakuja Bandari ya Tanga yataweza kutumia reli hii. Nimwombe Waziri mwenye dhamana ahakikishe kwamba wanaitengea kiasi cha pesa cha kutosha reli hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwa ndugu yangu Waziri mwenye dhamana. Nimeona Wabunge wengi wakisimama hapa kila mmoja anazungumzia kuhusu barabara, lakini naamini kabisa nchi hii ni kubwa sana kwa maana kwamba siyo rahisi kwa Serikali kutenga pesa kwa kila barabara. Najiuliza kwa nini tusitumie sekta binafsi kwa maana ya PPP (Public Private Partnership)?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iweke mpango maalum ikiwezekana i-train watu wetu waje na taarifa hapa Bungeni namna gani hii PPP inaweza ikafanya kazi na siyo katika barabara peke yake, tunaweza kwenda pia katika maeneo mengine. Tumeona nchi nyingi duniani wametumia PPP katika kufanikisha maendeleo hususan katika sekta ya barabara. Naomba Waziri mwenye dhamana alichukue hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la pongezi. Nimeona barabara zangu nyingi sana za Wilaya ya Kilindi zimetengewa pesa. Kwa niaba ya Wanakilindi nawapongeza sana Waziri na Naibu Waziri kwa sababu naamini kabisa mazingira ya Jimbo langu la Kilindi kwa kweli yana changamoto nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nina ushauri, wale wakandarasi ambao huwa wanapewa tenda za kutengeneza barabara, kwa mfano barabara hii ambayo nimeizungumzia kipindi cha wiki nzima iliyopita magari hayakupita kwa sababu wakandarasi hawa wanapotengeneza barabara hawatengenezi mitaro, magari yanakwama. Kwa hiyo, naomba Wizara iwasimamie wakandarasi hawa wanapowapa tenda hizi wahakikishe kwamba wanatengeneza katika viwango vinavyokubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni mawasiliano. Mara nyingi nimewasiliana sana na ndugu yangu Mheshimiwa Nditiye pale kwamba Wilaya ya Kilindi hususan katika Kata za Sauji, Kilwa, Lwande, hazina mawasiliano kabisa. Nimeona kuna taarifa imepita hapa kwamba kupitia Mfuko wa Mawasiliano wataweza kutujengea minara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri jambo hili walichukue kwa sababu kuna maeneo ambayo kabisa wananchi hawana mawasiliano. Jambo hili ni muhimu na ni haki ya Watanzania Wanakilindi kuhakikisha kwamba wanapata mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni Mfuko huu wa Barabara. Mfuko wa Barabara ni muhimu sana, najua nilizungumzia kwenye TARURA lakini bado napenda nizungumzie kwamba Waziri mwenye dhamana lazima ahakikishe barabara hizi zinapitiwa mara kwa mara kwa sababu utengenezaji huu haukidhi viwango. Hili tumeona hata katika maeneo ya Mkoa huu wa Dodoma hapa, barabara nyingi haziko katika viwango vinavyotakiwa. Serikali inatenga pesa, ni lazima pesa hizo ziwe na thamani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.