Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya na kwa kweli wanaombeza labda hao ni wanga tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa pamoja na Naibu wake wote kwa kazi nzuri ambazo wamekuwa wakizifanya katika Wizara hii. Wamezindua miradi mingi sana ukiwepo ununuzi wa ndege na ujenzi wa reli ya umeme, niwapongeze sana. Kutokana na kazi nzuri ambayo reli imekuwa ikifanya kuna ule mfuko wake pengine wangeachiwa maana unachukua muda mrefu na wao wana kazi nyingi na tunajua kwamba tunataka reli hii ikamilike mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niipongeze Serikali kwa ujenzi wa kiwanja cha ndege, mwenzangu amepongeza na mimi napongeza. Kupitia World Bank Kiwanja chetu cha Nduli kitajengwa ikiwa package mojawapo na ile barabara inayokwenda mbuga za wanyama. Kwa kweli naamini kabisa Mkoa wetu wa Iringa sasa tutapata uchumi wa kutosha na utafunguka kiutalii kwa sababu tukishajenga uwanja na tukishapeleka barabara ya lami Ruaha National Park najua kwamba Nyanda za Juu Kusini na Mkoa wa Iringa pia utafunguka kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee kupongeza Serikali kuhusiana na ujenzi wa mtandao wa barabara nchini ikiwepo barabara ya Dodoma - Mtera - Iringa kilometa 260. Kwa kweli barabara hii imekuwa mkombozi sana kwetu, inatufanya dakika dakika mbili tumefika Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ipo changamoto kubwa pale, ningeomba Mheshimiwa Waziri aangalie na ikiwezekana labda twende akaiangalie vizuri zaidi pamoja na wataalam wake. Wakati wa mvua ile barabara mawe yanadondoka kiasi kwamba kuna wakati magari hayapiti kabisa. Kwa hiyo, tumemwona hata Meneja wa TANROARDS, Ndugu Kindole, karibu siku tatu amefanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo, naomba kabisa barabara hiyo iangaliwe kwa sababu kuna wakati itakuja kuleta ajali kubwa sana na ikiwezekana bajeti ya mkoa iongezwe kutokana na tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Serikali itoe kipaumbele kwa barabara zetu za kiuchumi zilizopo katika Mkoa wa Iringa. Kwa sababu tumeona barabara hizi mara nyingi zimekuwa hazipitiki wakati wa mvua na kusababisha karibu siku mbili au tatu magari hayapiti, kwa hiyo, hilo ni tatizo kubwa. Barabara za Mafinga – Mgololo; Kilolo – Idete –Ipalamwa; Kinyanambwa – Saadani – Madibira na Kalenga – Kiponzelo, hizi ni barabara za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna barabara nyingine za kiuchumi ambazo ziko TARURA, pengine kwa sababu TANROADS huwa inachukua barabara za msongamano wa Dar-es-Salaam ingejaribu kuchukua hata barabara ambazo ni za kiuchumi zilizopo katika mkoa wetu ili huu uchumi wa viwanda sasa kwa sababu malighafi ziko huko, itakuwa matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka nichangie kuhusiana na TAZARA. Ni lini Serikali itarekebisha Sheria ile ya TAZARA kwa sababu imeshapitwa sana na wakati na utaona inawa-favour sana Wazambia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile TAZARA ina madeni, Serikali ililipa milioni 550 lakini bado wanadai milioni 745. Hivyo, tungetaka tujue lini watawalipa hawa wafanyakazi ili waendelee kuwa na moyo wa kuitumikia Serikali yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niendelee kuzungumza kuhusu USCAF, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, niwapongeze wamefanya kazi nzuri, hata mimi nilishawahi kwenda katika ziara zao kwa kweli wamepeleka mawasiliano vizuri. Hata hivyo, kuna baadhi ya maeneo katika Mkoa wetu wa Iringa bado ni matatizo. Kuna Lyamungo, Mfukulembe, Kalenga, Mpanga TAZARA, Lulanda, Mlafu, Mahenge, Ilindi, Magana, Iramba, kote huko bado kuna matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu naona iongeze kasi ya usambazaji wa mawasiliano sehemu ambazo hazina mvuto wa kibiashara, lakini pia iongeze rasilimali watu ili hii kazi iweze kwenda kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.