Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia nikiwa mchangiaji wa mwisho. Kwanza kabisa, nampongeza Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa kushika nafasi ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Naibu Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu wake. Sina budi kabisa kumshukuru Mheshimiwa Profesa Mbarawa, kusema kweli wamenisaidia sana mimi katika Jimbo la Nkasi Kaskazini, kwa mara ya kwanza naisifu hii Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninachoomba; mchakato wa ile Barabara ya Kirando – Kazovu mpaka sasa umechukua mwaka mzima na juzi wamekufa vijana watatu kwenye ule mto kwa kuvuka kuja ng’ambo ya pili, mpaka leo maiti moja imeonekana, mbili hazijaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna siku tatu wanafunzi kutoka Katete na Chongo kwenda Secondary School ya Kirando wanashindwa kuvuka ule mto na pesa zina mwaka mzima, mkandarasi yupo, lakini urasimu wa watendaji leo, kesho, mpaka leo daraja halijajengwa wala hakuna mpango wa kujenga daraja hivi karibuni. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri akitoka hapa awahimize watu wake wajenge daraja haraka sana kuokoa maisha ya wananchi wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usafiri Ziwa Tanganyika, leo ni mara ya nne, walituahidi kwanza meli mbili, sasa imekuwa meli moja na hiyo meli moja haijulikani. Cha ajabu Burundi wameshajenga meli kubwa sana, DR Congo wameshajenga meli kubwa sana, wametupiga bao. Sisi tunabaki kwa sababu tuna Bandari yetu ya Kigoma na Ziwa Tanganyika, ni ajabu watu wa Kongo ambao hawana bandari upande wa pili na watu wa Burundi wasio na bandari watatumia ziwa letu kwa ajili ya kusafirisha mizigo. DR Congo wameunda mpaka meli ya kubeba mabehewa, sisi tumekaa tu tunaangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usanifu wa miaka nenda, miaka rudi, haiwezekani. Walitenga bilioni kumi kwa ajili ya ukarabati wa Lihemba lakini mpaka leo hakuna. Watumishi wa Marine Service miezi 23 hawajalipwa mshahara, kusema kweli hii inakuwa meli zetu zinakwenda kizobazoba tu, maana yake watumishi hawana mshahara, hawana chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza TANROADS Manager wa Mkoa wa Rukwa. Ukimpigia simu hata saa saba za usiku kwamba kuna shimo kwenye barabara au barabara imefanya hivi, mara ileile kesho yake tayari alishatuma watu kwenda kutengeneza. Kusema kweli TANROADS Manager wa Mkoa wa Rukwa anafanya kazi, halali usingizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza kabisa Engineer Eliud wa Mfuko wa Barabara, ndio alikuwa chachu kabisa kuisadia Barabara ya Kirando – Kazovu ambayo ndugu zangu wananchi wamenituma kule. Kuanzia sasa vijiji vyote vya mwambao wa Ziwa Tanganyika hawataki kusikia chama cha upinzani, pamoja na Madiwani wa CHADEMA wako kule kwetu, wameniambia kamwambie Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Profesa Mbarawa kwamba kuanzia sasa sisi kura zote ni CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushahidi kabisa, muulizeni hata Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Nditiye, alikwenda Kabwe akamkuta kule Diwani wa CHADEMA, amemhakikishia kabisa kura zote ni kwa CCM. Kwa hiyo, ndugu zangu CCM kusema kweli inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukimfufua mtu aliyekufa mwaka jana akaja leo akaangalia, atashangaa, itabidi arudi kaburini haraka kwa yale maendeleo aliyofanya Mheshimiwa Dkt. Magufuli katika nchi hii. Tuache mchezo, Serikali ya Dkt. Magufuli inafanya maendeleo. Wilaya ya Nkasi naishukuru Serikali, Kabwe leo wametujengea bandari, ilikuwa miaka yote katika vitabu vyote inaandikwa, bajeti ya Bandari ya Kabwe, lakini leo kuna Mkandarasi yuko kazini na asilimia 20 ya kazi ilishaanza kufanywa, unasema huwezi kuishukuru Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, upinzani wapeleke huko huko. Mwaka 2020 ndugu zangu watapata aibu kubwa maana yake vitendo vinaonekana, Mawaziri wanapishana. Mimi kwangu Nkasi ni mbali sana kuliko sehemu yoyote lakini Waziri Mheshimiwa Profesa Mbarawa amefika, Naibu Waziri amefika kuja kuangalia maendeleo yanayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mkurugenzi wa TPA. Mkurugenzi wa TPA ndio chachu ya maendeleo ya Bandari ya Ziwa Tanganyika, amefanya… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)