Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu muweza wa yote kwa kuniwezesha kuwepo mahali hapa. Nami niungane na wenzangu kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hotuba hii imekuja na majibu ya kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya habari, utamaduni, sanaa na michezo. Hotuba hii inakwenda kutekeleza Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi katika nyanja zote muhimu zinazohusika katika Wizara hii, naipongeza Wizara kwa hotuba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali kwa kuendelea kuhakikisha masuala mazima ya michezo yanakwenda vizuri na kuhakikisha timu zetu za michezo mbalimbali zinashiriki mashindano ya kimataifa na kupata ushindi. Hata hivyo, kuna changamoto mbalimbali katika sekta ya michezo, naomba kuzungumzia uwakilishi wetu katika mchezo wa soka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika matokeo ya uwakilishi wetu kimataifa katika soka umekuwa si wa kuridhisha kabisa. Timu zetu kuanzia kwenye vilabu na timu ya Taifa tumekuwa ni wasindikizaji katika mashindano ya kimataifa. Serikali imekuwa ikijitahidi sana kuwekeza katika
mpira wa miguu lakini bado tumeshindwa kuwa na matokeo chanya pindi tunapokwenda katika mashindano hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuja na mkakati kabambe wa kuanzisha shule za mpira wa miguu na michezo mingine kuanzia mashuleni mpaka vyuo vikuu. Hii itatusaidia kupata na kukuza vipaji tangu vijana wetu wakiwa bado wadogo na kupelekea kupata wanamichezo wa michezo mbalimbali ambao sasa watakuja kuwakilisha nchi na kutuletea vikombe mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirikisho letu la Mpira wa Miguu liangaliwe kwa jicho la karibu ili kuondoa dhana ya viongozi wake kuona kwamba ni mahali pa kwenda kujipatia fedha zisizokuwa halali yaani fedha chafu. Wajikite katika masuala ya mpira wa miguu kuhakikisha wananyanyua kiwango cha mpira kwa namna ambayo itatutangaza kama Taifa, lakini siyo kila kukicha ni migogoro tu inatokea kwa kutofautiana kati ya kiongozi na kiongozi na kuacha dhana nzima na malengo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu. Serikali kupitia Wizara ichukue hatua kali pale inapoona kuna upungufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufike mahali sasa tuangalie michezo mingine au kitu kingine kitakachotutangaza kimataifa kwa upande wa sanaa, utamaduni au sanaa ya muziki ama inavyoitwa na vijana wetu wa sasa Muziki wa Kizazi Kipya. Tumejionea baadhi ya wasanii wakifanya vizuri kimataifa na kulitangaza jina la nchi yetu Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana hawa wanavyofanya vizuri kimataifa wanaitangaza nchi na kuiwezesha kupata wageni kwani wageni hutaka kuijua zaidi nchi husika baada ya kuona wimbo au msanii husika katika nchi zao akipewa heshima na taasisi mbalimbali. Hata hivyo, tumeshuhudia wasanii wetu wakikosa kuungwa mkono, baadhi ya watu kutokuona yale mazuri yote wanayoyafanya tena kwa juhudi zao wenyewe kulitangaza Taifa na Wizara kuja na kuwafungia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kupitia Wizara wakumbuke kuwa vijana hawa wanatumia nguvu nyingi na gharama kubwa kujitangaza na kulitangaza Taifa. Ni vyema wawe wanakaa nao na kuwashauri, Wizara igeuke kuwa mlezi wa wasanii wetu na siyo kuwa mkandamizaji. Leo wasanii wetu wanapata nafasi ya uwakilishi wa ufunguzi wa Kombe la Dunia kule nchini Russia kwa kwenda kutumbuiza. Mashindano yale ni makubwa duniani, dunia nzima watakuwa wanatazama na watataka kujua msanii huyu anatokea wapi. Wakijua Tanzania watataka kujua Tanzania kuna nini mpaka Shirikisho la Soka Duniani liweze kumchagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mwanzo mzuri wa kuanza kupokea wageni kuja nchini kwa shughuli mbalimbali za kiutalii, hata uwekezaji. Je, wasanii wetu kama hawa ambao wanapambana kwa hali na mali na kupata fursa kama hizo tunawaunga mkono kwa kiwango gani? Ni lazima Wizara itambue ni wapi kuna fursa ya nchi kutambulika kisanaa, kimichezo na kadhalika na kuhakikisha inashikamana na wahusika katika kuleta malengo chanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kupitia Wizara kuendelea kuvisimamia vyombo vya habari kwa mujibu wa sheria ili vitekeleze majukumu yao kwa utaratibu uliopangwa, kanuni na maadili ya uandishi wa habari. Kufanya hivyo kutasaidia sana kuwa na vyombo bora vya habari na uhakika wa habari zenyewe kwani tunajua umuhimu wa vyombo vya habari na waandishi wa habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tasnia ya habari inapotumika vizuri katika kutoa habari basi Taifa hubaki salama, lakini pale itakapopotoka na kutoa habari za kichochezi basi Taifa lazima litaingia katika machafuko na amani kutoweka. Wizara iwe inavikumbusha vyombo vya habari wajibu wao ili navyo vitekeleze majukumu yao kwa uhuru na haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.