Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu. Sayansi na Teknolojia

Hon. Catherine Nyakao Ruge

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu. Sayansi na Teknolojia

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwanza ninapenda kutoa pole kwa Mwenyekiti wangu wa Kanda na Mbunge wa Tarime Vijijini Mheshimiwa John Heche kwa msiba wa mdogo wake ambaye alifariki kwa kuchomwa kisu mikononi mwa polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naomba niende moja kwa moja kwenye hoja zangu. Mheshimiwa Waziri Profesa Ndalichako nimesoma hotuba yako na nimegundua mapungufu makubwa matatu. Pungufu la kwanza bajeti hii haina jicho la kijinsia (it is not a gender responsible budget). Nasikitika kwamba wewe ni mwanamke ni Mama lakini umeshindwa kuliona hili. Umeonesha takwimu mbalimbali mfano udahili wa wanachuo, wanafunzi waliopata mikopo elimu ya juu, kwamba unaenda kujenga mabweni, kuboresha miundombinu lakini huonyeshi beneficiaries (wanufaika) kwa kuangalia jinsia. Tunataka kuona rasilimali za nchi hii zikitumiwa sawa na zikiwafaidisha sawa watu wote bila kujali jinsia kwa maana ya jinsia ya wanawake na wanaume lakini huoneshi, kwa hiyo tunashindwa kujua beneficiaries wanawake ni wangapi na wanaume ni wangapi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pungufu la pili bajeti yako haina consistency kwa maana kwenye takwimu ambazo unazionesha ukurasa huu unaweka asilimia, kurasa nyingine hauweki asilimia, pale ambapo Serikali imefanya vibaya kwa maana ya Wizara hujaonesha kabisa takwimu. Uki-compare na hotuba ya Kamati wamefanya vizuri kuliko bajeti ya Wizara, wakati Wizara ina Wataalam. Wameweza kuonesha asilimia kwenye takwimu zao zote mpaka wametuwekea bar chart na tunaweza kuona ulinganifu wa performance indicators tofauti tofauti. Mpaka natia shaka inawezekana Waziri hii hotuba umekuja kukutana nayo hapa Bungeni kama Wabunge na hukuipitia. Siamini kama kwa umakini wako Madam Professor uliweza kuipitia na ukaliacha hili likaja hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pungufu la tatu bajeti hii haina continuity kwa maana ya muendelezo. Bajeti ya mwaka 2017/2018 na 2019 vitu ulivyoviandika 2017/2018 ambavyo unaona kabisa vinatakiwa kwenye bajeti hii vionekane vinaendelea havina mwendelezo.

Naomba nikupe mfano, ukienda ukurasa wa 10 wa kitabu chako unaelezea kuainisha mahitaji ya nchi katika ujuzi na kuendeleza na ukataja huo mradi ambao unaitwa Education Skills for Productive Job na ukataja maeneo ambayo unaenda kuendeleza stadi za kazi na ujuzi ukasema kilimo, TEHAMA, nishati, ujenzi, uchukuzi na utalii, lakini Madam Professor hakuna statistic, where the statistic Madam? Ukienda ukurasa wa 76 umeenda kuelezea jambo hilo kwamba kuainisha mahitaji ya nchi katika ujuzi na kuendeleza, lakini vile vipaumbele, ukija ukurasa wa 76, 77 kuainisha mahitaji ya nchi katika ujuzi na kuendeleza huku ametaja maeneo ambayo anaenda kuendeleza kwa maana ya elimu, TEHAMA, nishati na kadhalika, lakini huku hicho kitu hakijatajwa kabisa na hamna takwimu. Kwa hiyo, ina maana hii programu imeisha au? Sielewi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ningependa kuzungumzia ni usajili wa watoto wa kike vyuo vikuu. Ukisoma ukurasa wa 35 wa hotuba ya Kamati imeonesha idadi ya watoto wa kike wanaosajiliwa vyuo vikuu ni ndogo sana na wametoa takwimu hapa kwa mfano, Chuo Kikuu cha Mbeya mwaka wa masomo 2017/2018 jumla ya wanafunzi ambao wanafanya Shahada ya Kwanza ni 1,759 lakini kati ya hao ni wanafunzi 344 tu ambao ni wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunasema tunajenga uchumi wa viwanda na kama tunajenga uchumi wa viwanda haiwezekani, huwezi kumuacha mwanamke lazima mwanamke ata-contribute kwenye uchumi wa viwanda kwa maana ya nguvu kazi kwa kuajiriwa au kwa kujiajiri. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri wakati unakuja ku- wind up utuambie mkakati mahsusi wa Serikali wa kuhakikisha tunaongeza namba ya watoto wa kike wanaosoma masomo ya sayansi kuanzia shule za Awali mpaka vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ningependa kuchangia kuhusu ubora wa elimu nchini, bado unazidi kuporomoka kwa miaka Sita mfululizo bado Serikali inazidi kufanya vibaya kwa maana ya shule za Serikali uki-compare na shule binafsi. Ukiangalia ukurasa kuanzia wa 21, 22, 23 wa kitabu cha Kamati wameonesha indicators tofauti za ubora wa elimu. Kwa mfano, asilimia 37.8 ya Walimu ndiyo wana hamasa. Mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 159 upungufu wa walimu bado uko juu, lakini ukiangalia matokeo ya mwaka 2016 katika ukurasa wa 23 wa kitabu cha kamati inaonekana asilimia 73.3 walipata division four na division zero. Napata shaka kwamba miaka 10/20 ijayo tutakosa nguvu kazi, tutakosa watu ambao wanaenda kuajiriwa kwenye hiyo Tanzania ya viwanda kwa maana ya viwanda. Nasikitika pia kwamba tunaweza tukakosa maprofesa, madaktari kama tutaenda kwa mtindo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mwanafalsafa mmoja anasema if any organization want to be successful it must invest in people. Kwa hiyo, kama tunataka kuboresha elimu yetu ni lazima tu-invest kwa walimu, whether tunataka hatutaki ni lazima tu-invest kwa walimu kwa maana ya kuboresha maslahi yao, kwa maana ya kuongeza namba ya walimu wanaofundisha watoto tufuate ile ratio ya moja kwa 25, kwa maana ya kulipa malimbikizo ya madeni yao, kuwapandisha madaraja kwa wakati na maslahi mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Mwanafalsafa anasema kama unataka kupata matokeo tofauti lazima ufanye kitu tofauti. Tumeona miaka sita iliyopita bado ni business as usual lazima kama Serikali tu-take initiative ya kufanya vitu tofauti kabisa ili tuweze kupata matokeo bora na kukuza elimu ya watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuiomba Serikali kujenga shule ya watoto wa mahitaji maalum Mkoa wa Mara kwa sababu mkoa ule hauna shule ya watoto wa mahitaji maalum na wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda kutafuta elimu. Kwa hiyo, hii inawanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu, naomba uliangalie hilo na Mkoa wa Mara tunaomba shule ya watoto wenye mahitaji maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nipende kuzungumzia jinsi mvua ambavyo imeharibu miundombinu mbalimbali ya shule katika nchi hii. Mvua zilizokuja zilikuwa kubwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)