Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu Subhuhana – Wataala ametuamsha salama. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri mnayoifanya, Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nitazungumza kuhusu huu mradi wa Education Programme For Results (EP4R). Niwapongeze sana Wizara kwa kweli kwa sababu kwa kupitia programu hii tumeona mabadiliko makubwa sana kwenye shule za zamani au shule kongwe vilevile katika baadhi ya shule ambazo zilikuwa na hali mbaya, kwa hili kwa kweli nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yako yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukipita ukienda katika shule zilizokuwa zamani mfano Mpwapwa, Sengerema kule ambapo na mimi nilisoma ukienda Pugu, shule zimebadilika kutokana na kazi nzuri mnayoifanya. Hizi hela ni za wafadhili na mfadhili anatoa fedha anapoona unafanya vizuri lakini nasikia TAMISEMI wanataka sasa ziende kwao, Serikali ni moja tu mnagombea nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wizara ya Elimu wanashughulika na elimu, wanatengeneza miundombinu bado TAMISEMI wanataka nao hizo fedha ziende kwao, mnataka nini? Wakati mwingine hata mfadhili anaweza tu aka-doubt kwamba kwa nini hizi fedha mnataka ziende kule TAMISEMI wakati huku pia zinasimamiwa vizuri, Serikali ni hiyo moja tu.

Nashauri Serikali kwa kuwa ni moja, acheni Wizara ya Elimu wasimamie na wanafanya vizuri tu na isitoshe hata fedha zinapokwenda kwenye Halmashauri kwenye shule zetu bado maelekezo yanatoka TAMISEMI kwamba watumie force account, hizi fedha zisimamiwe vizuri na matunda yake tunayaona, ulikuwa ni ushauri wangu wa kwanza, msigombee fito mnajenga nyumba moja, nadhani Mheshimiwa Kakunda umenielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nizungumzie hizi shule za private, amesema pale kaka yangu James Mbatia kwamba shule hizi zimetoa mchango mkubwa sana. Bahati mbaya tu mimi sikusoma private, lakini watoto wangu wanasoma private. Hawa watu wa private ni Watanzania na wanaosomeshwa ni Watanzania wenzetu, tusiwaone kama competitors, hawa ni partner wa elimu ya Tanzania. Hii ni kwa sababu hata ukiangalia kodi zao ni nyingi sana lakini kodi zinazotozwa kwenye private sector kwenye elimu wanaoumia ni wazazi ambao ni Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba Mheshimiwa Waziri tafuteni muda muwe mnakaa na hawa private sector ya elimu mara kwa mara, ni vizuri kushauriana kwa sababu wanatoa mchango mkubwa sana kwa kweli. Wakati mwingine pia ni vizuri kumsikiliza tatizo lake na ukilisikia vizuri inawasaidia, kwa sababu utaona hata Mheshimiwa Rais anakutana na wafanyabiashara wanajadiliana, wanafikia muafaka na wakati mwingine maamuzi yanatoka palepale. Kwa hiyo, nilikuwa nadhani ni jambo jema mkaliangalia hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata ufunguaji wa shule, mimi nina mtoto wangu mdogo ana miaka 10 mtoto wa mwisho, anasoma private school lakini anaamka saa kumi basi linalomchukua yule mtoto linapita saa 11 alfajiri kwa sababu madarasa yanaanza saa mbili, lakini huwa najiuliza hivi hawa watoto wanaenda kusoma au wanaenda kulala?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu angalieni hata uwezekano, kwa sababu Kamishna wa Elimu anapotoa kwamba shule zifunguliwe tarehe fulani na zifungwe tarehe fulani, hii ni changamoto kubwa sana. Hivi kuna haja ya kuanza madarasa saa mbili? Hebu angalia kwa mfano Dar es Salaam ile, mtoto anachukuliwa Mbagala anaenda kusoma Masaki au Tegeta kwa mfano, anachukuliwa saa kumi alfajiri, akifika darasani analala tu huyu. Kwa hiyo, nilikuwa nadhani hata hii mihula muiangalie pia halafu kwani ni lazima shule zifunguliwe siku moja na zifungwe siku moja, kila mtu na utaratibu wake! Nilikuwa nadhani ni jambo ambalo Mheshimiwa Waziri mliangalie, kwa sababu hata hiyo private school ukiangalia asilimia 80 ya wanafunzi wanaokwenda katika university wanatoka kwenye private school, almost 80 percent. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye form four asilimia 80 ya wanafunzi wanaokwenda A - Level wanatoka private school. Tuwajengee mazingira hawa kwa sababu wanafanya vizuri na wakati huo huo Serikali tunafanya vizuri pia katika shule zetu. Nilikuwa nadhani nitoe ushauri kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwisho, shule hizi wakati mwingine michezo ni kivutio kikubwa sana kwa watoto wetu kusoma, lakini michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA tumeishusha sana hadhi na heshima yake. Leo akina Zamoyoni Mogella, Mkweche, Makumbi Juma na Abeid Mziba tuliwatoa huko kwenye UMISETA, lazima tuwekeze huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu ishirikiane na TAMISEMI na Wizara ya Michezo ili tuwatengeneze vijana wawe wazuri. Leo tusishangilie tu kwamba timu yetu imefanya vizuri vijana hawa, lakini baada ya pale hatuna tunachokifanya, watoto wanasambaratika, hatujengi Taifa bora. Mimi nadhani na bahati nzuri Mheshimiwa Kakunda wewe ni mtu wa michezo hebu tengenezeni mazingira ili vijana hawa wa shule zetu, UMISETA na UMITASHUMTA wafanye vizuri kwenye michezo na Taifa liweze kuwekeza zaidi, kwa sababu michezo ya UMISETA ndipo unapopata vijana watakaokwenda kucheza kwenye national teams zetu, iwe riadha, iwe football, huko ndiko tunakowapata, lakini tukisubiri kuokoteza mitaani bila kuweka msingi tutakuwa tunafanya makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba Mheshimiwa Rais alipokuteua Mheshimiwa Kakunda kwenda Wizara hii nadhani pia aliona kwamba una uwezo mkubwa sana wa kushawishi namna gani michezo ya UMISETA iwe na tija na iwe na nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya ninashukuru sana na nirudie kusema Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana, endelea kusimamia huu Mradi wa EP4R.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.