Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kabla sijachangia, naomba nimtangulize Mungu mbele kwa kumshukuru sana kwa kunipa afya na hekima. Kwa kuwa natambua kwamba maandiko yanasema katika mambo yote tutangulize dua na sala na Bunge lako huwa tunaanza na dua na sala na mahali popote unapomtaja Mungu tunasema lazima umtaje katika roho na kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mbunge unapotoa mchango wako ni lazima umtangulize Mungu ili akupe hekima uweze kuchangia vitu ambavyo vitatupeleka mbele. Kwa hiyo, naomba sana nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wake kwa namna walivyoleta hoja hii. Hoja imeandikwa vizuri sana, inatoa matumaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuamua kwamba ili tuweze kufikia uchumi wa kati lazima tuweke nguvu yote kwenye uchumi wa viwanda. Kwa hiyo, ni jambo moja zuri, lazima tumuunge sana mkono Rais wetu ili tufikie azma hiyo ya uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niseme tu kwamba katika viwanda ambavyo tunavizungumza, kweli vipo vingi; nimejaribu kuangalia karibu nusu ya kitabu ina orodha ya viwanda lakini unaweza ukaona uhalisia wa uchumi wa viwanda na uchumi wa kipato cha mtu mmoja mmoja. Tanzania wananchi walio wengi ni wakulima na tunaweza tukawasogeza mbele kama tutawekeza viwanda ambavyo vitasaidia sana wao kuuza mazao yao ili waweze kuwaongeza kipato walichonacho. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Mwijage katika orodha kubwa aliyokuwa nayo hapa, ajaribu kuangalia na kuweza kulea viwanda vile ambavyo vinasaidia sana wakulima wetu kuuza mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Wanging’ombe asilimia 90 ni wakulima wa mahindi na viazi mviringo. Wakulima hawa hawana soko la kuuza mazao haya ya viazi. Katika viazi kuna tatizo sana la vipimo. Kuna Wakala wa Vipimo, nimesoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, wanasema wanashughulikia namna ya kusimamia vifungashio. Wakati wa mwanzo walikuwa na vifungashio vikubwa ambavyo wanajaza vile viroba vikubwa vya lumbesa ambapo ukipima kwenye kilo ni zaidi ya kilo 100 ambayo ipo kwenye sheria. Hata hivyo, usimamizi wake ni mgumu sana kwa sababu wafanyabiashara wanatanguliza mawakala ambao wanakwenda kuwarubuni wakulima kule mashambani. Naomba hii Wakala itafute mbinu za kusimamia jambo hili, kusiwepo na kurubuni wakulima katika kuuza mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchezo mwingine ambao wanafanya wanasema wewe Wanging’ombe usipouza viazi wanakwenda kununua Mporoto au Arusha ambapo wanaweza kuuza kwa vipimo hivi vya lumbesa. Nafikiri kwa sababu huu Wakala upo basi uwajibike ili wakulima wetu wauze viazi kwa kilo siyo kwa vipimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wameleta viroba vidogo ambavyo vinaweza kujaza debe tano. Sasa ili gunia litimie unajaza viroba viwili na lumbesa yake. Kwa hiyo, unakuta kwa wastani kunakuwa na debe kumi ambazo wanasema hizi sasa ndiyo kilo 100 kwa vipimo. Kwa hiyo, tukiweza kwenda kwa kipimo cha kilo, tutafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vingine ambavyo nafikiri navyo tungevifanyia kazi ni viwanda vya mazao ya pamba, korosho, chai, kahawa, pareto, mahindi, mpunga na alizeti. Kwenye Jimbo langu tuna viwanda viwili; kimoja kinazalisha sembe, kinaitwa Mbomole Investment Company. Kile kiwanda hakizalishi kwa kiwango kikubwa kwa sababu tu TANESCO wameshindwa kutoa transformer ya KVA 200 kwa zaidi ya mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kiwanda kingine kimewekezwa pale cha kukamua mafuta ya alizeti kinaitwa Wende Investment Company. Hiki nacho kimeisha mwaka mzima lakini TANESCO wameshindwa kutoa transformer ya KVA 200. Sasa inawezekana mifano ya namna hii iko maeneo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri kama anavyokimbia hivi, nilifikiri ni vizuri viwanda hivi ambavyo vimeshaanzishwa visaidiwe. Wananchi wetu tumewahasisha wananchi wetu walime sana alizeti kwa sababu kiwanda kipo, najua watapata mahali pa kuuza lakini kama kinakuwa white elephant kwa sababu ya transformer tu, basi Serikali ni moja, uweze kuona namna ya kuwasiliana na Mheshimiwa Dkt. Kalemani tupate transformer, wananchi wangu wapate mahali pa kuuza hiyo alizeti na transformer nyingine kwa ajili ya wananchi wangu kuuza mahindi ili waweze kuinua kipato chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uuzaji wa mahindi imeoneka ni ngumu sana kwa sababu kipindi fulani Serikali ilikuwa imefunga mipaka lakini nashukuru sasa mmefungua. Hata hivyo, kuna urasimu sana katika kuuza mahindi nje ya nchi au maeneo mengine. Tuwasaidie kwa viwanda hivi ambavyo vinaanza kuibuka kwa kuwezesha mambo kama ya umeme na vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nichangie pia suala la kuinua uchumi. Nchi nyingi ambazo zimeendelea zilianza na viwanda vinavyohusiana na chuma. Tanzania tumezungumza habari ya Liganga na Mchuchuma kwa karne, kuanzia awamu ya kwanza ya Serikali zetu hizi lakini hakuna kinachoendelea. Unajua ukisema umtegemee Mchina, naye anataka kuinua uchumi wa nchi yake hataweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka uamuzi wa Rais uje kama wa Stiegler’s Gorge kwamba sasa tunaamua kujenga Stiegler’s Gorge, basi tuamue na kujenga Mchuchuma kwa namna yoyote inavyowezekana. Nina uhakika tutakuwa hatulii umaskini kwamba hatuna maji na vitu vingine, tunaweza kujitegemea wenyewe kama tulivyoanza kujenga reli. Nilifikiri kwamba nishauri na ndiyo maana naunga mkono hoja hii ili unisikie vizuri na ukalifanyie kazi kusudi Tanzania kweli ifike azma ya kuwa na uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambalo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni kwamba hapa Dodoma kuna mwekezaji mmoja alianzisha kiwanda cha kutengeneza hizi ceiling boards kwa kutumia gypsum na malighafi yake inatoka Dodoma hapa hapa, kipo hapo Kizota na Mheshimiwa Waziri nilishawahi kumwambia. Mwekezaji yule ameshindwa kukiendeleza kile kiwanda kwa sababu ya ushindani wa soko. Tatizo lipo kwa wafanyabiashara ambao wanaleta semi-finished goods, wanasema hii ni gypsum ghafi lakini kumbe ni finished goods ambazo sasa wao hawalipii kodi. Sasa hiki kiwanda kimefungwa na huyu mtu ameamua kuondoka. Aliwekeza fedha na wananchi wa Dodoma walikuwa wamepata ajira na Serikali inakosa kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri alifuatilie suala hili ili kusudi mwekezaji yule akifungue hiki kiwanda cha Dodoma na kama kuna kodi ambazo zipo kwa mujibu sheria, basi yeye anasema hana tatizo kulipa kodi, lakini kwa nini watu wengine wanasamehewa kodi kwa finished products, wanadanganya kwamba wanaleta malighafi ya gypsum? Tutakuwa tumeendeleza sana Mkoa wetu wa Dodoma ambao sasa ni makao mapya ya Serikali. Kwa hiyo, naomba kumshauri Mheshimiwa Waziri walifanyie kazi jambo hili kiwanda kile kifufuliwe ili kiweze kuleta ajira kwa wananchi wetu na Serikali pia itapata kodi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme, nashukuru sana kwa nafasi na naunga mkono hoja.