Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, dada yangu Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya. Naendelea kumpongeza sana kwa sababu mwaka 2011/2012 na 2012/2013 Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda. Kwa hiyo, yupo kwenye nafasi sahihi kabisa. Miongoni mwa hoja nyingi ambazo zimezungumziwa hapa, Engineer anazifahamu. Kwa hiyo, atakuwa kwenye nafasi nzuri sana kumwelekeza Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza ni Mchuchuma na Liganga. Mwaka 2012 pale Mlimani City, Dkt. Cyril Chami akiwa Waziri, Tanzania kupitia NDC tulisaini mkataba wa Liganga na Mchuchuma, mimi nikiwepo na Naibu Waziri alikuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninapozungumza ni takriban miaka sita. Mambo yote ya msingi kwenye mkataba ule tulikubaliana na naamini kwa kiasi kikubwa yametekelezwa. Inasikitisha sana miaka sita imeshapita toka sasa hakuna kitu chochote kilichofanyika kwenye Mchuchuma na Liganga. Kama kweli tunataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda, miongoni mwa maeneo ambayo tutatakiwa tuyaenzi kwa nguvu zetu kubwa ni eneo la Mchuchuma na Liganga ambapo malighafi za uhakika za umeme na chuma zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, makaa ya mawe ya Mchuchuma na makaa ya mawe ya Ngaka yanaweza kuzalisha umeme wa megawatt 120. Tulikuwa tuna tatizo kubwa la transmission line, lakini kwa bahati nzuri tumepata hela kwa wafadhili na transmission line ile inajengwa. Kwa
hiyo, umeme umeshapatikana, sasa kigugumizi kinatoka wapi cha kutoanzisha mradi wa Mchuchuma? Naamini kabisa Mheshimiwa Waziri akija hapa atatuambia ni sababu zipi zinapelekea leo mpaka miaka sita imefika hatujafanya chochote kwenye mradi mkubwa huu wa Liganga? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Tano, tumejielekeza kwenye uchumi wa viwanda. Tunapotaka kuzungumzia habari ya viwanda kuna baadhi ya mambo tunatakiwa tuyaangalie kwa karibu zaidi. Malighafi kubwa ambayo inatakiwa ipatikane kwenye eneo hili inatakiwa itoke kwenye kilimo. Tumejipanga vipi ku-invest kwenye kilimo kusudi tuwe na uhakika wa kupata raw materials za kutosha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa viwanda unakwenda simultaneously na uchumi wa kilimo. Tunaweza tukajenga viwanda vikubwa hapa nchini lakini kama malighafi hakuna, tutakuwa tuna hadithi, tutakuwa na viwanda ambavyo haviwezi kufanya uzalishaji. Kwa hiyo, tujiangalie, tunapotaka kujenga viwanda, tujiulize, hiyo malighafi inatoka wapi? Kwa hiyo, nashauri, tunapojiangalia kwenye uchumi wa viwanda, tujiangalie na namna ya kuandaa malighafi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka kulichangia na kumwomba Mheshimiwa Waziri aje kuniambia ni suala la Kurasini Logistic Center. Tumelipa fidia zaidi ya shilingi bilioni 90 kwenye Kurasini Logistic Center na tulisaini mkataba wa mwaka 2013 na Wachina kwa ajili ya kujenga logistic ile lakini leo ni miaka mitano hatujafanya chochote na shilingi bilioni 90 imeshakwenda pale. Kwa hiyo, tusije kuwa tuna matumizi ambayo siyo sahihi. Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakuja, aje atueleze kwa nini mpaka leo logistic center haijaanza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda kwa kazi na juhudi kubwa anayoifanya katika eneo lake, lakini pamoja na kazi kubwa anayoifanya, tunatakiwa sisi kama Tanzania tujipange namna ya kuvi-protect viwanda vyetu vya ndani. Kwa mfano, tuna viwanda vikubwa tu vya maziwa hapa nchini na maziwa mengi tunayotumia hapa nchini yanakuwa-imported kutoka nje, matokeo yake tunashindwa kuvisaidia viwanda vya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye taasisi nyingi za Serikali utakuta maziwa yanayotumika ni ya nchi za nje. Ukiuliza sababu zipi zimesababisha kutumia hizo Lactogen na maziwa mengine kutoka nchi za nje, hupati majibu. Kwa hiyo, kama tulivyofanya kuzuia importation ya furniture za nje, ifike wakati na Serikali izuie importation ya maziwa kutoka nchi za nje. Sisi kama Watanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na ng’ombe wengi katika Afrika. Kwa hiyo, tutumie utamaduni huo na rasilimali tuliyonayo kuhakikisha tunafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pamba huwa linaajiri watu wengi sana. Ukienda Cambodia pamoja na kwamba hawalimi pamba lakini watu wengi wameajiriwa katika industry ya textile. Kwa hiyo, ifike wakati sasa tuanzishe viwanda vingi hapa nchini vya nguo, naamini vitaajiri watu wengi kuliko kujielekeza kwenye kuuza rasilimali yetu ya pamba tutakuwa hatuitendei haki. Tuko tayari kumuunga mkono Mheshimiwa Waziri kwa kuhakikisha raw material zinazopatikana kwenye maeneo ya pamba, nyingi zinatumika ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo wenzetu wa viwanda wamefanya vizuri sana. Kwa mfano, eneo la BRELA (Msajili wa Makampuni), siku za nyuma palikuwa na shida sana, lakini sasa hivi wamefanya vizuri sana. Usajili unafanyikia online na unafanyika kwa kipindi kifupi. Kwa namna ya kipekee, tumpongeze Mheshimiwa Waziri na Mtendaji Mkuu wa BRELA kwa kazi nzuri anayoifanya katika maeneo yake. Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni, kama anafanya vizuri, naomba tumpongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naomba kuunga mkono hoja.