Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Dr. Susan Alphonce Kolimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na uzima na kuweza kusimama mbele yako na kuchangia katika hoja hii ambayo Waziri wangu ameiwasilisha leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi hii ya kipekee kama wenzangu walionitangulia kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake madhubuti. Vilevile nimpongeze pia Waziri wangu ambaye nafanya naye kazi kwa karibu kwa kazi nzuri anayoifanya kuitetea Tanzania kuisemea, kujenga mahusiano kati ya nchi mbalimbali na kuhakikisha kwamba diplomasia ya kiuchumi inatekelezwa ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwa sababu ya muda nimshukuru kwa namna ya kipekee mume wangu mpendwa Dkt. George Ayese Mrikalia kwa uvumilivu wao kwangu pamoja na familia yangu watoto wawili wanajua kwamba nimepewa kazi na mimi nimekubali, tutapambana mpaka kieleweke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda naomba niende moja kwa moja kwenye hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge najua kwamba hatutaweza kuzijibu hoja zote, lakini tunaahidi kwamba kwa niaba ya Wizara tutaweza kuzijibu kwa maandishi na kuzikabidhi kwao. Nikienda kwenye hoja ambazo zilikuwa zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge hasa kwenye Kamati nitajibu tu baadhi ya hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna suala la Kamati kutushauri kuhusu kuandaa sera ya Taifa ya diaspora. Nasema kwamba Wizara imeunda timu mahususi ili kufanikisha uandaaji wa sera hii ya Taifa ya diaspora itakayoainisha mikakati na kutoa mwongozo kuhusu ushiriki wa diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi. Timu hiyo tayari imekwishaanza hatua za awali za maandalizi ya sera hiyo. Pia Wizara imetenga fedha kwa mwaka huu kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa ajili ya zoezi hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu kuongeza kasi ya kukamilisha mchakato wa sera mpya yaani Revise Foreign Policy, niseme tu kwamba Wizara imekamilisha kuandaa rasimu ya Sera hiyo Mpya ya Mambo ya Nje ya Tanzania, lakini hatua inayofuata sasa ni kuandaa mkakati wa utekelezaji ambao pamoja na rasimu ya sera hiyo vitawasilishwa kwa wadau kwa maana ya Serikali na sekta binafsi ili kupata maoni yao na Wizara imetenga fedha kwa ajili ya zoezi hili ya bajeti ya 2018/2019 kwa ajili ya kukamilisha sera hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niruke kidogo niende kwa Mheshimiwa Masoud ambaye alizungumzia kuhusu wale wafungwa 11 ambao wako kwenye gereza lile la BEO kule Msumbiji niseme tu nimeshakwisha wasiliana na Mbunge wao ambaye alikuwa anafuatilia hilo na tumewasiliana na Balozi wetu kule Msumbiji. Alimtuma Afisa kwenda kuangalia wiki mbili zilizopita, pia juzi alienda yeye mwenyewe na anasema tu kwamba anasubiria taratibu za kimahakama watakavyomaliza process za kuandaa kila kitu tutakuwa tunaendelea kumtaarifu Mbunge husika na kuhakikisha kwamba maslahi ya wale Watanzania yanalindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Masoud kwa kuhakikisha kwamba anafuatilia masuala ya Watanzania wakiwemo Watanzania ambao yeye ni Mbunge wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikienda kwenye suala lingine ambalo pia limetolewa na Kamati kwa kushauri Wizara ambalo linahusu kuhusu upatikanaji wa fedha za ujenzi wa majengo ya ubalozi na makazi katika Balozi zetu. Suala hili limekwishaongelewa sana kwenye hotuba ya
Mheshimiwa Waziri na mikakati tuliyokuwa nayo mkakati wa kwanza wa miaka 15 ambao ulikuwa ulioanza mwaka wa fedha 2002/2003 mpaka mwaka wa fedha 2016/2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia sasa hivi tumetengeneza mkakati mpya ambapo tumejaribu kuangalia kuhakikisha kwamba suala la kutengeneza mkakati wa upatikanaji wa fedha na ujenzi pamoja na ukarabati wa Balozi zetu zilizoko nje unafanyika kwa haraka iwezekanavyo. Tutaendelea kulisimamia hilo na kufuatilia kwenye Wizara ya Fedha na kwa vile Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje ni Serikali basi nadhani Mungu atatusaidia na tutaweza kufikia mahali pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie uwezekano wa kuziruhusu Balozi kubakiza angalau asilimia 40 ya makusanyo kwa maana ya maduhuli ili ziwezeshe kutekeleza majukumu yao kwenye Balozi husika; hili suala ni la kanuni na sheria. Tutajaribu kuangalia kukaa pamoja na Wizara ya Fedha na kupata ushauri wao wa kitaalam na kama sheria zitakuwa zinaruhusu basi sisi tuko tayari kupokea ushauri wa Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ni wasikivu kama mnavyoona, tumetekeleza yale ambayo tumefanya, mmesema tufungue Counsel tumefungua, mmesema tufungue Balozi Cuba, tumefungua; lakini mmesema kwamba tuhakikishe jengo letu la Maputo linajengwa na kukarabatiwa na watu wanahamia, tumefanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja ya Waziri wangu. Ahsante sana.