Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Mwanne Ismail Mchemba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami nichangie machache kwenye bajeti hii ya Wizara ya Fedha, lakini pia nichukue nafasi hii pekee kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri anayoifanya. Uongozi wa Awamu ya Tano umejipanga na umejipanga kwa mambo mazuri matupu na yenye kufanikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Dkt. Mpango, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Kijaji, nina sababu zangu. Nawapongeza kwa sababu muda hautoshi, lakini nampongeza na Katibu Mkuu wa Wizara hii kwa kazi nzuri waliyofanya kwenye Kamati ya Uongozi na Bajeti (Kamati ya Bajeti). Wamefanya kazi nzuri miongoni mwa kazi nzuri kwa sababu kwa mara yangu ya kwanza nimeweza kukaa nao meza moja na kuona wanafanya nini. Mheshimiwa Waziri amekuwa mtiifu na amekuwa kiongozi pekee kwa ufafanuzi wa Wizara yake; hiyo nafasi nampongeza sana na amekuwa mtiifu sana.

Mheshimiwa Spika, niombe yale yaliyokuwa yamezungumzwa na maombi yaliyotolewa kwenye Kamati Mheshimiwa Waziri wa Fedha ayazingatie kwa sababu ni Kamati ya Uongozi na Kamati ya Bajeti. Sasa Kamati ya Uongozi maana yake Mheshimiwa Spika alikaa kwenye kiti hicho na akabariki yale aliyokuwa ameyaahidi.

Mheshimiwa Spika, lakini la kwanza tulikuwa na ombi la Kamati ya Bajeti kwamba ajitahidi katika utaratibu wake na mipango yake kuhakikisha kwamba hii Sh.50 iongezwe kwenye petrol na diesel kwa ajili ya maji. Mfuko wa Maji ni muhimu sana, kero yote hii, mazunguzo yote haya, yanajitokeza na lawama kwake ni kwa sababu hiyo kwamba bajeti ya maji ni ndogo, kama hataongeza basi atafute vyanzo vingine vya kuhakikisha kwamba anaongeza kwenye bajeti ya maji ili tuondokane na matatizo la maji.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo alikubali yeye mwenyewe kwenye Kamati ya Bajeti ni kupeleka fedha kwenye miradi ambayo wananchi wamejitokeza na wameifanyia kazi kubwa, miradi ya afya, maji, elimu ambayo haijakamilika. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango kwamba anapokuja sasa ahakikishe pesa zinapelekwa kwa wakati; hilo ndilo tatizo. Pesa zipo kidogo lakini haziendi kwa wakati. Kuna fedha ambazo zilitakiwa kukidhi bajeti iliyopita ya 2017/2018, lakini mpaka sasa kwa bahati mbaya au kwa makusudi au bahati mbaya hasa mimi nasema kutokana na makato kutokamilika kwa wakati basi amepeleka asilimia kidogo.

Mheshimiwa Spika, kuna suala zima la TARURA na TANROAD, ile asilimia 30 kwa 70 bado TARURA wana kazi kubwa sana. Kwa hiyo, niombe kama hatapunguza kwenye TANROAD, basi ni vizuri akaangalia jinsi gani ya kuibeba TARURA kutoka kwenye vyanzo vingine ili angalau wapate asilimia 40. Kwa sababu kwa mwaka huu mvua imeharibu asilimia kubwa ya miundombinu vijijini. Kwa hiyo barabara ambazo ni mbaya ni vijijini na barabara pia za mjini ambazo ni barabara kuu pia zimeharibika. Kwa hiyo, ingekuwa ni vizuri zaidi zote zikaangaliwa ili pesa ziende kwa usawa.

Mheshimiwa Spika, pia niombe pia kuhusu suala la kuongeza fedha kwenye Mifuko hii ifuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kuna mfuko wa Rais wa Kujitegemea, TASAF na MKURABITA. Mheshimiwa Dkt. Mpango haya mambo sisi tumeyaona kwa sababu ni Kamati yangu ya Utawala na Serikali za Mitaa, mimi kama Makamu. Mifuko hii inafanya kazi vizuri sana. Mfuko wa Kujitegemea wa Rais unaweza ukasaidia ukaitoa hata ile milioni 50 ambayo inakwenda kila kijiji ingepitia kule. Tumejifunza mengi kwenye Mfuko wa JK ambao ulikwenda hovyo; sasa huu asikurupuke, asifanye haraka wala asikosee tena.

Mheshimiwa Spika, ziende kwenye TASAF na MKURABITA, kwa sababu uelewa sasa hivi wa wananchi kuhusu msaada wa Mfuko wa Rais wa Kujitegemea ni mkubwa na sasa hivi wameenea nchi nzima mpaka vijijini. Kwa hiyo hawa tukiwalea nadhani Mheshimiwa Mpango ataondokana na hii kadhia ya milioni 50; kwa hiyo awe na utaratibu wa kupeleka fedha kwenye Mifuko hiyo. Pia hata asilimia 10; akiiweka vizuri hii asilimia 10 ikapita mle, wananchi wengi sana watanufaika, kwa sababu sisi tumekwenda moja kwa moja na Kamati yangu kwenye maeneo hayo na tumeona nini wanachokifanya, kwa hiyo mafanikio ni makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, lakini lingine ni suala zima la korosho, ila mimi sitaunga mkono kwa kuandamana, alishatupa ufafanuzi wa deni hilo la korosho. Niiombe Serikali, mimi naweka msisitizo tu, niiombe Serikali ione jinsi gani ya kusaidia hili zao la korosho kwa sababu imekuwa ni kero, kero hiyo itatuathiri. Mheshimiwa Mbunge aliyemaliza tunaona kama ana dhihaka lakini ana maana ya kulizungumzia ndani ya Chama cha Mapinduzi tatizo hili.

Kwa hiyo, hili tatizo ningeomba; kwenye Kamati alizungumzia kwamba kunatakiwa uhakiki, kuna mambo mengi wameyaona. Sasa yale ambayo wameshahakiki basi hizi pesa zipelekwe kwa wakati angalau surphur basi ipelekwe kwa wakati ili waweze kuokoa zao hilo.

Mheshimiwa Spika, lingine la mwisho, Mheshimiwa Dkt. Mpango, nimejitahidi sana pamoja na Naibu wake nimepeleka taarifa nyingi sana za kuhusu TRA na kuhusu jinsi makusanyo ya Serikali yanavyopotea. Nimempelekea na nashukuru ndiyo maana nimesema ni watiifu kwa sababu walitekeleza na waliona. Kwa hiyo, ningeshauri kuitegemea TRA peke yake si mbadala, ni vizuri tukajipanga tukaanzisha pia kitengo maalum cha kufuatilia hizi mashine za EFDs; kwa sababu watu kweli hawazitumii kwa neno la kusema kwamba mashine mbovu kwa sababu walishatangaza kwamba hizi mashine zinasumbua, kwa hiyo watu wengi wanachukulia advantage hiyo kwamba mashine ni mbovu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni vizuri sasa ufuatiliji uwe ni wa makini na zile barua ambazo wanaandika baada ya mashine kuharibika, nadhani sasa atoe mkakati maalum, atoe agizo maalum kusiwe na zile barua ambazo wameweka kwenye lamination wanazungumzia tu kwamba tumeambiwa wanabadilisha tu.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi Tanzania hii tena wameelimika ujanja ni mwingi, matapeli ni wengi, kwa hiyo tunapokwenda kwenye maeneo ya biashara mtu anapiga magoti kuomba kwamba apunguziwe. Kwa hiyo niombe Wizara ya Fedha, niiombe kwa msisitizo mkubwa iendelee kutoa elimu ya maana ya ulipaji kodi kwa wananchi wote kwa kutumia local radios kutumia TV, vipindi maalum. Mheshimiwa Waziri asione ubahili wa kutumia vipindi maalum.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka kuishauri Serikali ijitahidi itoe elimu, Watanzania hatukuwa na tabia hiyo ya kulipa kodi. Kwa hiyo wengi watakwepa kwa lolote atakalotaka kwa ajili ya kuongeza mapato ya Serikali. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana kwa kazi nzuri anayoifanya, ni wakati mgumu lazima atapata matatizo mengi, lakini lazima tujipange, tushirikiane katika ulipaji kodi na matumizi yake. Tukifanya hivyo vikaenda pamoja Serikali itakwenda juu na tutatoka hapa tulipo. Nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.