Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa namna ambavyo wameweza kufanya kazi vizuri na hasa Mheshimiwa Rais kwa sababu katika hotuba ya Waziri ameweza kutueleza mambo 10 ambayo kimsingi Mheshimiwa Rais ameweza kuyafanya vizuri kabisa.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na kwenye Kitabu cha Hotuba ya Waziri ya mapendekezo ya bajeti. Kwa upande wa mapato ya ndani amezungumzia kwamba kuna changamoto ambazo zimekuwepo au matatizo ambapo yamepelekea makusanyo yetu ya ndani hatufikii malengo katika utekelezaji wa bajeti ya 2017/2018 ambayo makusanyo ya ndani trillioni 19.9 lakini kwa mpaka Aprili tumekusanya trilioni 14 na point; ila ukichukulia miezi miwili mpaka kufikia mwezi Juni huu tarehe 30 tunaweza kufikia labda kwenye trilioni 16.

Mheshimiwa Spika, katika matatizo ambayo ameweza kuyaeleza la kwanza ni suala la ukwepaji kodi. Ningependa matatizo ambayo ameyaeleza yote, ukwepaji kodi, sekta isiyo rasmi ambayo haijaweza kurasimishwa, mazingira siyo rafiki, masuala ya EFD, udhaifu katika kuvuna maliasili na utegemezi wa mashirika ya umma, kiujumla haya matatizo Mheshimiwa Waziri hajatueleza sasa haya matatizo anaenda kutatua kwa njia gani; ningeomba Serikali itusaidie.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kwenye suala kwanza la ukwepaji kodi. Siku zote Serikali imekuwa ikifuatilia na inaweka jitihada mbalimbali na hasa kwenye TEHAMA lakini bado kuna udhaifu sana katika maeneo hayo. Kwa hiyo tuombe Serikali iangalie kwa undani na kikubwa zaidi katika kuweza kudhibiti ni suala la kuwa na takwimu. Bila kuwa na takwimu huwezi ukaingia kwenye namna bora ya kudhibiti. Kwa mfano, tumekuwa tukipata malalamiko kwenye suala la flow meter kwa upande wa mafuta, kwamba kumekuwa na wizi sana na Serikali inapoteza sana mapato.

Mheshimiwa Spika, ningeomba hebu Serikali ijaribu kuangalia; kwa mfano tukiweka kwenye hizi kodi kwa upande wa mafuta twende kwa capacity ya meli kama inabeba lita 10,000 au lita milioni mbili basi tuchaji kodi kutokana na capacity ya meli ambavyo imeleta hayo mafuta. Kwa hiyo mtu akibeba under capacity au full capacity itamlazimisha aijaze meli yote mafuta na sisi tu-base kule na kwa hiyo huu wizi unaotokea kwenye flow meter tutakuwa tumeukwepa.

Mheshimiwa Spika, tuna suala la sekta isiyo rasmi, hawa Machinga; mwaka jana Serikali iliahidi kwamba itafanya usajili na vitambulisho watapewa na tuweze kuweka tozo; na Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba utekelezaji wake bado ni hafifu. Sasa je, ni lini itafanyika kwa haraka ili sekta isiyo rasmi iweze kuchangia katika mapato ya Serikali na tuweze kukidhi katika kufanya kazi za maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la EFD’s; mwanzoni kwa juhudi za Mheshimiwa Rais aliwahi kuibua kwamba kuna watu walikuwa wanacheza na hizi EFD’s ripoti haziendi TRA, wanatoa risiti na wanaiba pesa nyingi. Je, Serikali kwa sasa hivi ina mkakati upi wa kuhakikisha kwamba record za hizi EFD’s zinasoma huko katika mitambo yetu ya TRA na ziko sahihi? Je, wamewahi kulinganisha na kama kuna utofauti wowote umetokea nini ambacho kimeweza kufanyika ili kuweza kuboresha ukwepaji wa mapato?

Mheshimiwa Spika, kwenye halmashauri zetu tunatumia PoS lakini maeneo mengine hizi PoS hazitumi ripoti katika mfumo, ni eneo lile ambalo tayari lina udhaifu. Kwa hiyo watu wanakusanya ripoti haziingii katika mfumo na wanasingizia network. Kwa hiyo hapa ni mahali ambapo tunapoteza mapato, tumeona kwamba tunadhibiti lakini bado tunatakiwa tuongeze juhudi katika kusimamia.

Mheshimiwa Spika, kuna udhaifu katika uvunaji wa maliasili, kama ni udhaifu je, ni udhaifu wa mfumo, tatizo ni mfumo au tatizo ni watendaji? Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri aje atueleze kuhusu haya udhaifu katika uvunaji wa maliasili na tumepoteza mapato, tatizo ni mfumo au tatizo ni watendaji.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la mashirika. Waziri amesisitiza sana kwamba Ofisi ya Hazina itasimamia mashirika ambayo Serikali inapata gawio. Niombe tu, kwamba juzi hapa Mheshimiwa Rais ameteua Msajili wa Hazina, basi staff waongezwe katika hiyo ofisi na kuweza kusimamia vyema ili Serikali ipate mapato ambayo hayatokani na kodi kutokana na hisa zilizokuwa kwenye makampuni au na mashirika mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, vile vile ipo pia chini ya Kamati yako ya Uwekezaji wa mitaji ya Umma (PIC). PIC inahitaji ipate muda mzuri ambao wa tofauti ili kuweza kusimamia hayo mashirika 270 na tuweze kuishauri Serikali namna bora ambavyo itaweza kuongeza zaidi mapato yasiyotokana na kodi kutokana na hizi dividend za sehemu mbalimbali. Kwa hiyo tutaomba Kamati yako ya PIC uiwezeshe zaidi kwa muda ili iweze kufanya kazi ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mabadiliko mbalimbali ya sheria ambayo Waziri aliyapendekeza katika hotuba yake. Kwanza kuna suala la tozo kwenye mvinyo HS code 2206.00.90. Mvinyo unaotokana na ndizi mwanzoni walikuwa hawa hawalipi, lakini sasa mapendekezo kwa lita moja watalipa Sh.200.

Mheshimiwa Spika, baada ya kupiga vita suala la viroba watu wetu ambao walikuwa wanatumia zaidi viroba wamehamia kwenye banana wine ambayo ni very cheap lakini imewekewa tozo ambayo ni kubwa ukilinganisha na kwa lita. Kwa hiyo, tutaomba Waziri uone namna ya kuipunguza hii badala ya Sh.200 iwe ndogo ambayo itaweza kukidhi, kwa sababu hizi banana wine zinauzwa Sh.2,000/= elfu moja na, tofauti na hizi zingine ambazo zinauzwa karibuni Sh.8,000/= mpaka Sh.12,000/=, Sh.15,000/=. Kwa hiyo hii tutaomba, nami naweza kuweka hata schedule of amendment tutakavyoweza kukubaliana.

Mheshimiwa Spika, kwenye mabadiliko ya kodi kuna suala la asilimia 10. Awali mapendekezo wameweka tu kwamba ni youth and women, lakini tulikuwa tuna vijana, wanawake na walemavu, kwa hiyo ilikuwa ni four, four, two. Kwa hiyo nitaomba hii ibadilishwe iendane na haya mapendekezo kama ilivyokuwa awali.

Mheshimiwa Spika, pia tulifanya mabadiliko ya produce cess, mwaka jana kutoka asilimia tano mpaka tatu. Hii imepunguza sana mapato kwenye halmashauri zetu ambapo kwa mfano wanunuzi wa tumbaku halmashauri mapato yameshuka. Sasa kwa nini wasiangalie kwa sababu haijamfaidisha mkulima na imefaidisha zaidi hawa wanunuzi wa haya mazao kama ya tumbaku.

Mheshimiwa Spika, vile vile katika mabadiliko ya sheria hapa kwenye Amendment of Local Government Finances Act, clause 35; kwamba corporate entity ambayo ina-produce hizi agricultural crops na hai-add value ndiyo ambayo itaenda kulipa zile produce cess. Hata hivyo, tuna wakulima ambao wengine wakubwa hawapo kwenye corporate, sasa hawa wanaenda kuchangia vipi katika kuweza kulipia mapato? Mtu anaweza akawa analima takribani heka 500, heka 200; sasa hapa wamesema tu ni corporate na mtu hayuko kwenye corporate. Hilo eneo nalo ni bora kuangalia.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kwamba katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri alizungumzia kuhusu balance of payment (Urari). Tumeona kwamba tunaagiza sana ngano nje na mafuta ya kula na tumeona kwamba katika hotuba yake mwaka mmoja wameweza kuongeza tozo kwenye mafuta ya kula ili tuweze ku-promote zaidi ukulima wetu wa ndani. Hata hivyo, naona tatizo hapa, kwamba ni jinsi gani tunawezesha na kuvutia wakulima wakubwa ambao watakuwa kwenye economies of scale na wanalima kwenye large scale ili tuweze kupunguza ulipaji wa fedha zetu za kigeni nje kwa ajili ya kuagiza malighafi za ngano na mafuta ya kula.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusiana na mambo mazuri ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya. Sisi Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Katavi umeme awamu wa tatu REA III bado mpaka tunavyozungumza hivi haujaingia; na tunamwangusha sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ya matatizo ambayo yametokea katika tender ambazo zimekuwepo, kesi inapigwa dana dana kila siku. Wananchi wetu wanaendelea kuulizia kuhusu huu umeme. Kwa hiyo niombe Serikali ifikie mahali sasa jambo hili liweze kukamilishwa na wananchi wakaweza kupata huduma ya umeme ambayo tayari tunaitegemea sana kwa maendeleo yetu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.