Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuishauri Serikali katika Hotuba ya Bajeti ya Mwaka 2018/2019. Mwaka wa fedha 2016/2017, nilipokuwa nachangia Hotuba ya Bajeti, nilisema kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ilivyokuja na malengo yake inaonekana kama vile si Serikali ya CCM iliyokuwa inaongoza nchi hii kwa miaka yote. Nikasema kwamba kama watakwenda na spirit hiyo basi kutakuwa na mabadiliko tutakayoweza kuyaona.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo kwa sababu niliamini kwamba watu wanaoiongoza Serikali ya Awamu ya Tano ni wale wale ambao wameongoza nchi hii kwa miaka yote tuliyonayo ya uhuru wa nchi hii, niliamini kwamba kusingekuwa na mabadiliko makubwa kama ambavyo inaonekana leo. Kwamba baada ya miaka mitatu bado hali ya maisha ya Watanzania yamezidi kuwa magumu sana, watu wameendelea kuishi katika shida na matatizo ambayo walikuwa wametegemea kwamba yangemalizwa katika Serikali hii ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Spika, Serikali hii imeendelea kuwa un- popular kwa wananchi kwa siku zinavyoendelea kuliko hata ilivyokuwa huko nyuma. Kama hali hii itaendelea, kama uchaguzi utakuwa huru na haki 2020 nafasi yenu ya kushinda ni ndogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, angalau katika bajeti hii kuna harufu ya kuonesha kwamba kuna mambo wanataka kuyashughulikia ambayo ni ya msingi sana kwa jamii na hasa katika eneo la kodi. Jambo ambalo tumelizungumza sana kama Kambi Rasmi ya Upinzani lakini wakati wote mmekuwa hamko tayari kusikiliza; na imekuwa ndio traditional ya Serikali hii. Kwamba kama jambo Mheshimiwa Rais hataamka alizungumze alitilie uzito basi wengine wakilishauri utekelezaji wake unakuwa ni mgumu sana.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu Mheshimiwa Rais alikaa na wafanyabiashara angalau ukiangalia bajeti hii kuna vitu unaanza kuviona angalau vinaanza kutekelezwa. Hata hivyo, naona kama muda umechelewa sana wa kujenga confidence ya wafanyabiashara na wananchi kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Spika, nashauri mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza, Serikali ya Awamu ya Tano ijaribu kuondoa hofu wanayokuwa nayo wafanyabiashara na wawekezaji katika nchi hii; hakuna kabisa confidence ya kuwekeza. Mtu anapowekeza katika nchi hii uhakika wake wa kufanya biashara yake mpaka ifike mwisho umekuwa ni mgumu sana. Hana uhakika kwamba kesho kutaamka na nini, keshokutwa kutakuwepo na nini. Imekuwa kama vile kufanya biashara katika nchi hii ni kitendo kiovu. Mfanyabiashara anakuwa anaandamwa kwa kiwango ambacho ni cha kutisha, wala kufanya biashara tena katika nchi hii siyo baraka.

Mheshimiwa Spika, sasa nadhani ni vizuri Serikali ibadilishe huo mtazamo, ifanye kwamba wafanyabiashara ni sehemu ya wadau muhimu sana katika Taifa hili na hasa kwa Serikali ambayo inategemea kodi. Iwafanye wafanyabiashara kuwa ni watu ambao ni kama ng’ombe unaowakamua ambao kimsingi unapaswa kuwalisha majani ili upate maziwa kuliko kufika mahali ambapo wafanyabiashara wanaonekana kama ni maadui katika Taifa.

Mheshimiwa Spika, mtazamo kwamba wafanyabiashara wote ni wakwepa kodi si sahihi, wako wachache ambao wanaokwepa kodi lakini wafanyabiashara wengi katika nchi hii ya Tanzania hasa Watanzania kwa tabia zao na malezi yao hawapendi kusumbuana na Serikali katika suala la kodi; wanahitaji tu maelekezo sahihi, uongozi bora wa namna ambavyo wataongozwa katika kulipa kodi.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri, kama ambavyo leo tunaleta Tax Amnesty katika maeneo mbalimbali, sheria za namna ambavyo tunafikiri kwamba riba na faini ambazo zimejilimbikiza angalau ziangaliwe. Tuangalie pia utaratibu ambapo kama mfanyabiashara amefanyiwa auditing na akaonekana kodi yake ni kiasi fulani apewe muda wa kuilipa taratibu. Haiwezekani mfanyabiashara apewe kodi ya milioni mia moja umtake alipe wakati huo huo, anaipatia wapi hiyo fedha? Unless awe ni mwizi. Apewe muda taratibu hata wa miaka miwili, mitatu alipe hiyo fedha taratibu huku akiwezeshwa kuendelea kufanya biashara ili aweze kuisaidia Serikali na kuweza kusaidia mambo mengine ya maendeleo ya nchi hii yaende.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nafikiri ni vizuri sana Mheshimiwa Waziri akaliangalia hilo. Kukawa kuna roho ya huruma ambayo anatakiwa awe nayo na hasa kwa watu ambao wame-comply kulipa. Wale ambao wanakataa kulipa ndio waadhibiwe, lakini mtu amepewa demand note leo, baada ya siku mbili anafungiwa biashara yake, akaunti zake zinaanza kufungwa, fedha yote inachukuliwa na TRA, huyu mtu ana mikopo ya benki, ataendeleaje na biashara? Matokeo yake mambo yafuatayo yanatokea; wafanyabiashara wanakufa kwa presha, wanafilisiwa na matokeo yake na ninyi hampati chochote katika Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni vizuri sana tuangalie namna gani; kwa sababu Taifa hili la Tanzania hakuna njia nyingine ya kuishi zaidi ya kukaa vizuri na wafanyabiashara na wawekezaji, maana hawafanyi biashara wao, wanataka kujitahiditahidi kuanza kuingia kwenye biashara ambako kimsingi tulishatoka huko. Automatically naona kama wameshindwa na hawataweza kabisa kwa sababu tulishatoka huko kwa karne ya sasa hivi. Sasa watu ambao wanaweza kuwasaidia ni wafanyabiashara na wawekezaji, wasaidieni hao watu. Nadhani hilo ni eneo la kwanza la muhimu sana, naishauri Serikali iliangalie kwa makini.

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba hii wamesema mojawapo ya shida inayowasumbua ni sekta isiyo rasmi. Naamini bajeti hii waliyonayo TRA wana uwezo wa kukusanya kabisa hizi fedha, naamini kabisa, lakini inahitaji umakini katika kusimamia hili. Sekta isiyo rasmi lazima waigawanye katika makundi, sekta isiyo rasmi wanapoizungumzia kwamba ni Wamachinga tu siyo maana yake. Kuna watu ambao wana maeneo kabisa wana-settlement vizuri, wako mahali pazuri, wanafanya biashara zao lakini hawajaingizwa kwenye mfumo wa kodi.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa tulilonalo ni kwamba tuna wafanyakazi wachache wa TRA ambao hawawezi kuwafikia hao wafanyabiashara na wa bahati mbaya hawaoni umuhimu wa wajibu wa halmashauri zenu, hawataki kuzitumia halmashauri zao. Wangetumia halmashauri zao vizuri wakaamini kwamba halmashauri ni chombo muhimu cha kuwasaidia zingewasaidia ku-trap hawa wafanyabiashara ambao wapo na hawana leseni lakini wanafanya biashara, wamejificha kwenye kivuli cha kutokuwa wafanyabiashara wasio rasmi, leo wangekuwa wameweza kuongeza mapato yenu.

Mheshimiwa Spika, sasa ushauri wangu kwa Serikali waongeze wafanyakazi wa TRA, kwa sababu ni investment. Kumwongeza mfanyakazi wa TRA si sawa na kumwajiri Mwalimu. Ni investment ya haraka ambayo pesa yako ipo ili waweze kufikia walipa kodi wengi. Sasa matokeo yake wanabaki na walipa kodi wachache ambao kila wakiamka ndio hao wanapambana nao.

Mheshimiwa Spika, walio wengi wamewaacha wako barabarani na bahati mbaya wamejifunika kwenye kigezo kwamba wao hawajafikia kwenye pato la mauzo ghafi ya milioni 20 kwa mwaka, kwa hiyo wanabaki hapo hapo wao hawaguswi, wala hawapo kwenye VAT, hawapo popote wapo tu. Siku zote wamezidi kuwapotezea mapato na wao hawawezi kulisukuma hilo. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aongeze wafanyakazi wa TRA ili wafikie walipa kodi wengi ili waweze kufikia haya malengo waliyotarajia.

Mheshimiwa Spika, suala la tatu ni suala la halmashauri. Mheshimiwa Waziri a-revisit uamuzi wa kuchukua vyanzo vya mapato vya halmashauri. Watajidanganya sana wakiendelea kuamini kwamba vyanzo vya mapato vya halmashauri vitasaidia Serikali Kuu. Serikali Kuu wana vyanzo vingi, wazifanye halmashauri ziweze kukusanya mapato ili zitoe huduma kwa wale watu wa chini, watu wengi wako chini.

Mheshimiwa Spika, Rais atakuwa na nafasi na wao ya kupanga mambo ya Bomberdier, mambo ya reli na mambo mengine kwa sababu ya fedha zao za Serikali Kuu, lakini waache halmashauri zikusanye fedha kwa mambo yale ya maji, afya, elimu na kadhalika. Kama watajidanganya kwamba walioanza huko nyuma walikuwa hawaelewi wakaona wao wanaelewa zaidi wakaanza kuturudisha kwenye centralization wanapotea katika mwelekeo. Nishasema hili narudia kulisema hili, hakuna kosa kubwa wanalolifanya Serikali ya Awamu ya Tano kama kuua halmashauri, kama kuua Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri katika nchi ambayo ina muundo mzuri wa Serikali za Mitaa, Tanzania ni mojawapo, lakini bahati mbaya katika nchi ambayo haitimizi wajibu wake vizuri kwenye Serikali za Mitaa, Serikali ya Awamu ya Tano ni ya kwanza. Sasa ni vizuri waone ni namna gani wanavirudisha vyanzo vya halmashauri ili ziweze kutengeneza barabara zake, halmashauri zitengeneze vituo vya afya, zitengeneze zahanati. Sasa wasipofanya hivyo kila pesa wakitaka tupige magoti kuwaomba mpaka lini?

Mheshimiwa Spika, haya yalikuwa maoni yangu na ushauri wangu kwa Serikali. Nashukuru sana.