Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JOEL M. MWAKANYAGA: Mheshimiwa Spika, naomba kushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hotuba ya bajeti kuu ya Serikali iliyowasilishwa na Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango tarehe 14 mwezi huu.

Mheshimiwa Spika, pili, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, nitaendelea kumpongeza kila nikisimama kwa sababu kazi yake anayoifanya tunaiona ni nzuri na moja kati ya vigezo kwamba kazi inayoyofanywa ni nzuri tunaona, bajeti hii imetolewa katika kipindi chake akiwa Rais. kwa hiyo, hii ni bajeti ambayo ina mwongozo moja kwa moja toka kwa Mheshimiwa Rais na ni bajeti nzuri kama tunavyoiona, nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango yeye pamoja na Naibu wake, lakini pamoja na Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara ile kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuiandaa hotuba hii na bajeti hii ambayo sasa tunaijadili hapa Bungeni. Mwisho, nimpongeze yeye binafsi kwa uwasilishaji mzuri sana wa bajeti alioutoa siku ile ya tarehe 14 hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kwamba mpango ni mpango na mipango tunayo sisi sote, majumbani mwetu tuna mipango mingi na hakuna mtu anayepanga na mipango yake ikatimilika asilimia 100, si kawaida. Utapanga kufanya vitano, utatekeleza vitatu au vinne mpango ni dira, dira inapokuwa nzuri una hakika kwamba wewe unapiga hatua nzuri; mipango yetu ni mizuri na ndiyo maana tunasema bajeti hii ni nzuri sana. Bajeti hii ni nzuri kwa sababu imelenga kwa wananchi wa kawaida, wananchi wa chini kabisa. Kwa nini nasema hivyo, tukienda kwenye kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa kuanzia 42 kuendelea hadi 46 yako mambo mengi yaliyozungumzwa pale.

Mheshimiwa Spika, nijikite kwenye misamaha na mfumo wa kodi ambao baadhi umejionesha pale. Serikali imesamehe kodi ya ongezeko la thamani kwa baadhi ya malighafi muhimu zinazokuja kutumika viwandani kuzalisha bidhaa zinazotumika kwa Watanzania. Pia Serikali hiyo hiyo imeongeza ushuru wa bidhaa za kutoka nje kwa bidhaa ambazo pia zinazalishwa hapa nchini, lakini pia tumeona Serikali safari hii haijagusa kabisa kuongeza kodi kwenye bidhaa zote za mafuta ikiwemo diesel pamoja na petrol.

Mheshimiwa Spika, hatua hizi ni muhimu sana, hatua hizi zitasaidia sana kupunguza mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali zinazozalishwa hapa nchini. Tunapopunguza gharama za uzalishaji maana yake bei za bidhaa zetu ama zitabakia constant, ama zitashuka chini kidogo. Kwa hiyo basi, kama tulivyoona kwenye punguzo na ongezeko ya kodi mbalimbali ambazo tumezitaja hapo nyuma kwa mfano, madawa ya binadamu, vyakula vya binadamu, vyakula vya mifugo, hivi ni vitu ambavyo moja kwa moja vinamgusa Mtanzania wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, vilevile hatua hizi zinalenga kulinda viwanda vya ndani jambo ambalo ndilo kipaumbele kikubwa cha Serikali yetu ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya viwanda. Tunapolinda viwanda vya ndani maana yake tunakuza ajira kwa Watanzania. Suala la uchumi wa Tanzania limejitokeza wazi kabisa kwamba linakua kwa kasi kubwa sana, lakini ukiangalia upande wa pili wa mwananchi wa kawaida, uchumi wa mwananchi wa kawaida hauonekani kukua kwa kasi sambamba na kasi ya uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, hili ndilo kipaumbele cha nchi yetu cha Serikali ya Awamu ya Tano kwamba Tanzania ya viwanda inalenga kuwe na viwanda vingi, viwanda vinavyotegemea sana mazao ya kilimo. Kwenye kilimo ndiko kunaajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania, sasa ukiwezesha kuwa na Tanzania ya viwanda maana yake unatengeneza soko kwa ajili ya mazao yetu yanayozalishwa hapa Tanzania, maana yake unawawezesha Watanzania wa kawaida kupata kipato kitakachowasaidia kukuza uchumi wao. Katika kilimo utakuta Watanzania wote tupo, wapo Watanzania wa kawaida lakini wako vijana sehemu kubwa, wako akinamama na hata walemavu wako humohumo ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili mipango hii iweze kuwa na tija, Serikali inatakiwa ijizatiti. Ijizatiti kweli katika kukusanya mapato yake, ihakikishe kwamba taratibu zote za ukusanyaji wa mapato, tumesikia baadhi ya Wajumbe wakichangia hapa wasiwasi unaokuwepo juu ya nani anasimamia nini katika ukusanyaji wa mapato haya. Ni vizuri tukajihakikishia kwamba tuko kwenye mikono salama, pesa yetu isichopoke chopoke huku na huko ili moja kwa moja itumike katika kuitekeleza hii Bajeti ya mwaka wa bajeti 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, niombe sana, pesa hii inapopatikana ielekezwe kule kunakohusika. Wizara mbalimbali zimeleta bajeti zao na ndiyo hii sasa imeletwa kwa ujumla, imeletwa kama Bajeti Kuu ya Serikali. Kama Wizara hazitapewa bajeti zao walivyoomba basi suala zima la Bajeti hii kutokuwa na manufaa sana kwa wananchi litakuwa limeleta shida.

Mheshimiwa Spika, nije kwa upande wa ardhi, bajeti hii inahitaji wananchi wafanye kazi. Wananchi wanatakiwa kuwa na peace of mind katika kuzifanya kazi zao. Kama wananchi watakuwa na hali ya migogoro ya hapa na pale ya ardhi maana yake ni nini? Zoezi zima la uzalishaji kwao litakuwa siyo la ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana ndugu yangu Waziri wa Ardhi, kuna migogoro mingi ambayo unaishughulikia, naomba uishughulikie kwa kasi kubwa. Nakuamini sana Mheshimiwa Lukuvi kazi unayoifanya, lakini nikuelekeze pia, hata hapa Dodoma kuna migogoro ya ardhi, hata kule Chamwino kuna migogoro ya ardhi na bahati nzuri wewe ulishawahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma unafahamu nini ninachokizungumza, unayafahamu maeneo ya Wali kule kuna mgogoro wa ardhi kati ya Wilaya ya Chamwino na Wilaya ya Kongwa. Inafika mahali wananchi wanakimbia maeneo yao, kipindi cha kulima wanakimbia maeneo yao wanashindwa kufanya kazi inavyostahili. (Makofi)

Mheshimiwa pika, ahsante sana, labda nimalizie moja tu kwa upande wa viwanja kwako, Mheshimiwa Lukuvi viwanja pale Buigiri vimepimwa siku nyingi lakini zoezi zima la kuvigawa vile viwanja limekuwa tatizo. Mheshimiwa Waziri alikuja pale Wilayani akaotoa maelekezo lakini maelekezo hayo yajafuatwa. Naomba sana alitekeleze hili ili wananchi wafanye kazi kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache, naomba kuunga mkono hoja.