Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kupata fursa hii niweze kuchangia bajeti kuu. Wakati Mheshimiwa Waziri anawasilisha bajeti hii, nilikuwa najaribu kumwangalia sana hata usoni kwamba anachozungumza na kilichomo ndani ya moyo wake kinaonekana ni tofauti kabisa. Nina wasiwasi sana kama Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha haya hivi anakwenda field au anatuletea tu taarifa hapa ambazo hajui hali halisi ya uchumi wa nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri anatuletea taarifa ambayo Deni la Taifa ni shilingi trilioni 46, sisi tunakusanya shilingi trilioni 32, hawa watu wanaotudai wakicharuka, kitakachofanyika ni kwamba nchi itauzwa na sisi tutauzwa. Kwa maana hiyo, sioni realistic ya bajeti yake hapa. Tulitegemea kwamba angekuja na mipango ambayo inatuonesha ni jinsi gani tunakwenda kupunguza hilo deni na kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati bajeti inawasilishwa tulikuwa tuki-observe pia nchi nyingine zinavyowasilisha bajeti zake. Ukiangalia Kenya, Uganda, Mawaziri wako serious wanaonesha ni jinsi gani wamejipanga kuhakikisha bajeti wanayokwenda kuiwasilisha inakuwa na impact kwa wananchi wao. Ukija ukiangalia kwetu huku, bajeti siasa, Waziri ashukuru na wananchi wake na majirani zake wa Zuzu na kadhalika. Hakuna mwaka ambao bajeti imekosa mvuto kama huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata waliokuwa wanafuatilia kwenye televisheni, wananchi unawauliza hivi kwa nini hamfuatilii bajeti? Wananchi wanasema aah, ni business as usual, hakuna jipya, maisha ni magumu. Hawana hata muda watu wa kutoka maofisini wakakae waangalie bajeti ya Serikali inasemaje, kwa sababu hawategemei kuongezewa hata senti tano ya mshahara. Kwa hiyo, lazima tujiulize ni kwa nini wananchi hawako na sisi wakati tunawasilisha vitu muhimu vya Taifa hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Waziri anasema kwamba pato la Taifa limepanda. Hivi, kweli limepanda kwa watu gani? Mheshimiwa Waziri aende field aone kwa macho yake mawili, pato la Taifa limepanda unapita kila nyumba unakuta imeandikwa inauzwa kwa mnada wa benki fulani? Pato gani hili ambalo limepanda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapita huko mtaani, maduka yamefungwa, pato la Taifa limepanda! Mheshimiwa Waziri atuambie, pato la Taifa limepanda, benki zinashusha riba! Namwambia hata zikifikisha asilimia mbili, Watanzania hawana nguvu ya kukopa. Kwa nini? Biashara hazifanyiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata mabenki yakazane kushusha riba, kama huu uchumi haujarekebishwa, bado namna ya wananchi kurudisha fedha hizo hawana, wataendelea ku-default na ndiyo maana wanaogopa. Ndicho kilichobaki kwa mabenki sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pato la Taifa limepanda, sasa hivi mpaka Benki za Serikali zenyewe zinashindwa kufanya kazi. Twiga Bankcorp juzi wame-merge na Postal Bank, haina mtaji, imefilisika. Benki ya Wanawake hivi sasa inachechemea, hata kulipa mishahara haiwezi. Pato la Taifa limepanda! (Makofi)

Mheshimimiwa Mwenyekiti, tunataka Mheshimiwa Waziri atuambie, hivi hili pato la Taifa kupanda, kuna impact gani kwa mwananchi wa kawaida? Tuwe na huruma na hawa wananchi ambao wanakamuliwa, sisi tunapata kulipwa mishahara, kama kweli hatuwezi kuwasemea na kuangalia ni namna gani ya kuwasaidia wananchi hawa wakanyanyuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri anasema, katika mipango yake, kwenye bajeti hii TRA wakakusanye shilingi trilioni 20. Hivi, shilingi trilioni 20 zinakwenda kupatikana kwa namna gani? Nimeangalia kama kuna vyanzo vipya ambavyo wame-identify, hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyanzo ni vile vile, watu ni wale wale; hii tunakwenda kuwakamua wananchi mpaka jasho la damu. Kwa sababu ukiangalia TRA sasa hivi; namwona Kamishna wa TRA anazunguka kama pia; yuko Dodoma, wapi na wapi, eti anaenda kuvizia na yeye watu gani wamenunua bidhaa bila risiti? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Kuna shida somewhere. Hakuna hela! Kwa hiyo, anatoka ofisini hakukaliki, anakwenda mikoani naye anakaa vichochoroni kama hawa junior officers wanavizia wananchi ambao ni wateja wametoka kununua bidhaa. Haiwezekani! Lazima wafike mahali waone hili kwamba hali ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika watu wanao-frustrate wafanyabiashara ni pamoja na TRA.Hivi siku wafanyabiashara wakiamua sasa hawafanyi tena biashara, wanauza kunde kwa sababu hazina kodi; hivi watapata wapi mapato? Ndipo wanakoelekea hivi sasa, kwa sababu TRA sasa hivi wanazunguka na mifuko ya sulphate imejaa makufuli kwamba wakikukuta na kikosa kidogo wanafunga kwa sababu wamepewa majukumu kuhakikisha wanakusanya. Kwa hiyo, wafanyeje? Wanatumia nguvu! Kwa hiyo, wanakomoa ili kuhakikisha kwamba makusanyo yanapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna tena kuelimisha wafanyabiashara kuhusu TRA. Mfano mzuri, wengine nasi ni wafanyabiashara, tunajua. Maofisa wa TRA wanakuja kwenye biashara yako, asubuhi wanakwambia print Z Report na Waziri anaelewa, Z Report inatolewa baada ya mtu kuwa amemaliza mauzo yake, anafunga siku. Sasa wewe saa mbili unataka Z Report. Kwa maana hiyo unaua system nzima ya makusanyo. Halafu wanafungua draw wanaangalia una shilingi ngapi? Wana compare na Z Report. Hivi tunapeleka wapi wafanyabiashara hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anaelewa mfumo wetu wa kutoa risiti za EFD machine uko slow. Imefika mahali TRA mpaka wanapandikiza watu. Wanawaleta purposively ili kuhakikisha kwamba akishanunua bidhaa, kwa sababu mfumo wetu siyo kama petrol station kwamba ukijaziwa mafuta inatoka, hapana, lazima utumie mikono, dakika tano wakati mwingine system iko down, uweze kupata risiti. Wanachokifanya, anachukua bidhaa anaondoka, wanakuja Maofisa wanakwambia hujatoa risiti. Kwa hiyo, huu ni uonezi wa hali ya juu. Kama kweli Serikali imeamua kukusanya mapato siyo kwa kuwaonea wafanyabiashara kwa kiwango hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la importation na exportation, nimesikia eti wanataka ku-discourage importation ili kulinda viwanda. Viwanda vipi? Leo tunasema kwamba mafuta, mtu anakaa kwenye gari hawazi, anasema, kuanzia leo hakuna kuingiza mafuta nchini. Uzalishaji wetu wa mafuta ya kula ni asilimia 30. Asilimia 70 tunaipata wapi? Tunategemea watoe kauli hizo wakati wameshapandisha uzalishaji kwa asilimia 100, ndiyo watuwekee hizo restrictions kwamba mafuta yasiingie nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la importation na exportation ni la kimahusiano zaidi kwa Mataifa na Taifa. Hivi leo tunaweka restriction, bidhaa zetu huko nje zinakoenda, zisipopokelewa inakuwaje? Kwa maana hiyo kama mtu anaamua kwamba sasa hakuna kuingiza mafuta kutoka asilimia 25 wamepandisha mpaka 35 mafuta hakuna, nchi ina uwezo asilimia 30, hivi wanataka kuwarudisha wananchi kula chakula bila mafuta? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza, hivi traffic kwenye makusanyo, wako upande upi? Kwa sababu traffic speed waliyonayo wanawazidi hata TRA. Hizi tochi zilikuja kwa lengo la kupunguza ajali au kuongeza mapato, watuambie! Kwa sababu tangu tochi zimekuja, nashangaa unawasikia ma-RTO wanaeleza tumekusanya kiasi hiki, si kutuambia ajali zimepungua kwa kiasi hiki, wanatuambia tumekusanya kiasi hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi lengo la tochi watuambie kumbe siyo kupunguza ajali ni kukusanya! Labda ni indirect way ya kukusanya, atueleze Mheshimiwa Waziri. Maana inafika mahali sasa Traffic wanapanda juu ya miti, wanatokea porini, ni fine. Imefika mahali madereva wanasema; ah, mimi sasa nalazimika ninunue tochi. Maana ya kununua tochi ni nini? Unaweka pesa mfukoni, kila unapokutana nao Sh.30,000/= unatoa unaendelea.