Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Hassanali Mohamedali Ibrahim

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiembesamaki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI RAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo na pumzi yake kusimama hapa kuchangia bajeti hii muhimu sana katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, pamoja na timu yake nzima kwa jinsi walivyoandaa hii bajeti ya fedha ambayo itatusukuma mpaka 2019. Hongereni sana Mheshimiwa Waziri na timu nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwashukuru wenzetu wa TRA. Unajua tunapozungumzia masuala ya bajeti ya Serikali lazima tuwashukuru na wenzetu wa TRA namna wanavyohangaika kutafuta mapato ambayo yanatusaidia wananchi. Bila TRA kukusanya mapato leo hapa tusingeweza kuzungumzia bajeti hii. Kwa hiyo, nimshukuru sana Kamishna Charles Kichere na timu yake nzima ya TRA kwa jinsi wanavyofanya kazi nzuri ya kukusanya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naweza kusema sasa hivi kwa kiasi fulani TRA wamekuwa marafiki sana kwa wafanyabiashara na wameweza angalau kukaa kwenye meza kumaliza yale matatizo ambayo wafanyabiashara wamekuwa wanahangaika nayo. Kwa hiyo, lazima tuwape sifa TRA tofauti na miaka ya nyuma hawakujenga mahusiano mazuri na wafanyabiashara lakini sasa hivi wamekuwa wasikivu na wenye nidhamu ila baadhi yao bado siyo waaminifu lakini kwa asilimia kubwa wanafanya kazi nzuri. Nawapongeza sana TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu bila nguvu zake tusingefika hapa tulipo. Watu ambao wanataka tusimsifu Rais, hivi jamani kwenye Bunge hili tumsifu Uhuru Kenyata au tumsifu Museveni? Sisi tuko hapa kumsifu Rais John Pombe Magufuli, hatuko hapa kuwasifia Marais wa nchi nyingine, huo ndiyo ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiongozi yeyote anapofanya mazuri usitegemee wapinzani kukusifu sana hiyo ni kawaida. Nchi zote duniani hakuna chama kinachoongoza wananchi halafu wapinzani wakakisifu, si India, Ulaya hata huko Marekani. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Rais asivunjike nguvu, aendelee na katika miaka yake miwili na nusu tumeona mambo makubwa aliyofanya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kushirikiana na Waziri Mkuu na Mawaziri. Mawaziri wa Awamu hii ya Tano wamekuwa ni Mawaziri ambao wanafanya kazi usiku na mchana, kwa hiyo, niipongeze Serikali nzima ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumzie bajeti hii. Kwanza niipongeze Wizara kwa kuondoa VAT katika masuala haya ya taulo kwa sababu kweli yatawasaidia akina mama na wanafunzi kwa kiasi kikubwa sana, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia kuongezea ushuru baadhi ya bidhaa kwa nia ya kuvilinda viwanda vya ndani. Kwa kweli, tulikuwa tunawafanyia biashara kubwa wenzetu wa nchi jirani, wao wanatuletea hapa sisi tunafanya manunuzi tu, tunawachumia wao, ajira zinakwenda nchi za jirani, nchini kwetu viwanda vinaumia na wafanyakazi wakati mwingine wanapunguzwa. Katika kuongeza Ushuru wa Bidhaa katika bidhaa mbalimbali hatua hiyo itavilinda viwanda vyetu vya ndani. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija katika masuala ya nguo zetu za mitumba, naomba Wizara hii iangalie kwa jicho la huruma hizi nguo za mitumba kwa sababu huwa zinatumiwa na wananchi wa hali ya chini kabisa Tanzania hii. Nguo za mitumba zinauzwa rahisi, kila mmoja wetu anajua zinakwenda mpaka vijijini na mikoani. Sasa hivi container moja la mitumba linatozwa shilingi milioni 40. Naomba tu Wizara, kama kuna uwezekano wa kupunguza angalau kidogo tukawapa nguvu hawa wananchi wa chini ambao hawawezi wakanunua shati la Sh.40,000 au Sh.50,000 wajipatie mashati hayo kwa bei rahisi na hii itatusaidia kujenga uhusiano mzuri na watu wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niombe Waziri aangalie sana sekta ya kilimo kwa sababu ni sekta moja muhimu sana katika nchi yetu ya Tanzania na asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo. Kwa hiyo, namwomba sana wakulima wawezeshwe, wapatiwe mikopo, wapewe
initiative ambayo itawasaidia kuwekeza katika kilimo. Kilimo kikiwa kizuri Tanzania tutapata foreign exchange. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchini India wanategemea sana agriculture, wana-export kwa hali ya juu. Serikali ya India inapata pesa nyingi sana katika kwa ku-export bidhaa za agriculture. Hata wenzetu wa Thailand kwa kiasi kikubwa cha fedha wanategemea export ya agriculture. Kwa hiyo, siyo vibaya nasi tukaipa umuhimu sana sekta hii ya kilimo ambayo kwa kiasi fulani itatusaidia kupata foreign exchange kwa sababu, njia kubwa ya kupata foreign exchange ni kuuza mazao yetu nje. Sisi Tanzania Mungu ametupa ardhi kubwa sana ambayo mimi naweza kusema asilimia kama 40 hazijatumika, bado tunayo ardhi ya kuwekeza katika kilimo. Tukikipa umuhimu kilimo basi Serikali yetu itapata foreign exchange. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kasoro kidogo imejitokeza, wafanyabiashara wengi Dar-es-Salaam hawana mashine za EFD, wanatumia receipt book. Serikali inakosa mapato, TRA inakosa mapato na naona hawawatendei haki wafanyabiashara wengine wanaotumia mashine za EFD. Kwa hiyo, naomba TRA kupitia Wizara yako ihakikishe katika kipindi cha miezi miwili kila mfanyabiashara anatumia mashine ya EFD.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono asilimia 110. Ahsante sana.