Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi hii na mimi kuchangia hoja ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza lazima nifurahie kwamba sasa hivi Tanzania inaelekea katika viwanda, ina maana Tanzania ya Viwanda. Bajeti aliyoileta Mheshimiwa Waziri imepangika, ina vionjo vya kutendea kazi na inatekelezeka. Hongera Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu na watendaji wote wa Serikali katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujielekeza katika viwanda lazima tuwaangalie wakulima. Bila ya kuwa na wakulima hodari wakaweza kutupatia malighafi viwanda vitakosa malighafi na amesema kwamba viwanda vya ndani vitapata malighafi hapa hapa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa wakulima, kama kweli watajielekeza kwenye kulima ina maana sasa ni mwaka wao nao wa kufarijika katika maisha. Kwa sababu wataweza kuongeza mashamba, watakuwa na ushindani katika bidhaa zao watakazokuwa wanalima, watakuwa na masoko kwamba watapeleka mazao yao katika viwanda vyetu. Naomba wakulima waangaliwe ili kupata malighafi ili viwanda vyetu viweze kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwa upande wa pili, tukumbuke kwamba Wizara ya Fedha wanatumia cash budget kwa maana makusanyo mnayoyapata ndiyo mnayoyatumia. Sasa inabidi lazima wajitahidi kupata kodi ili kupata pesa za kutosha, bila ya kukusanya haitawezekana kutumia. Baadhi ya watendaji wetu wanaweza wakazembea katika kukusanya huruma isiwepo, mtu anazembea kwenye kazi unamuondoa kwenye nafasi yake kwa sababu akizembea yeye ameifanya Serikali yote mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuchukulie mfano, siku za hivi karibuni zile mashine zetu za kukusanya mapato EFD zimeharibika, Wabunge wanapiga kelele, jawabu tunalolipata halitoshi kwa sababu mpaka leo ukweli hasa hatujaupata. Sasa tuangalie, tatizo lilikuwa kwa wenye mashine au uzembe wa wafanyakazi au kuna kitu gani kilichojitokeza mpaka leo hakuna suluhisho? Kuna Mbunge mmoja pia hapa kalizungumza hili kwa sababu sasa hivi watu wanatumia risiti na kama tunatumia risiti tayari tunapigwa. Mheshimiwa Waziri akija na hilo lazima alizungumzie ili tuweze kufarijika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, malalamiko mengi yanatokea hapa kuhusu malipo ya kodi mara mbili katika bandari zetu kwa vitu vinavyotoka Zanzibar. Suala hili limezungumzwa, nakumbuka Naibu Waziri wa Fedha alilitolea ufafanuzi kwamba wanakaa sasa hivi wanalizungumza na wakati wowote watafikia muafaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nina ushauri, kwa sababu jambo lolote linataka elimu, Wizara ya Muungano iko inashughulikia Bara na Visiwani, ipeni majukumu pia Wizara hii kutoa elimu. Taasisi za Zanzibar na na Bara zinazoshughulika na mambo ya fedha wapewe elimu ili waelewe kwa nini huu mvutano unatokea, kwa sababu sheria mnajua ziko vipi na mwelekeo uko vipi ili huu mvutano uzidi kupungua. Nendeni kwenye media mtoe maelezo kuna nini na baadaye mkubali watu wapige simu nao watoe taarifa au malalamiko yao, myapokee na myajibu. Haya ni mambo madogo tu yanazungumzika. Jambo hili linachukua muda mrefu ilhali si refu. Tunalifanya liwe refu ili tuweke mvutano hapa usio na maana ilhali jambo hili linazungumzika na ni rahisi kumalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja na suala lingine ambalo liko katika ukurasa wa 46(v), kuhusu kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye taulo za kike ili isaidie vijana wetu wa kike na akina mama katika matatizo yao ya kawaida. Nakubali Mheshimiwa Waziri alivyosema kwamba wamepunguza kodi, ni sawa lakini kupunguza huko kusiwe kwa mwaka huu na mwakani upunguze tena ili iwe wanapunguza kidogo kidogo mpaka ifikie sawasawa kama mtu anakwenda kununua karanga haoni shida tena bei yake itakuwa rahisi tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vya ndani vinazalisha, itakuwa kila wakiteremsha bei na bei ya dukani itakuwa inashuka na itakuwa rahisi kila mmoja kununua hata mtoto wa chini atanunua. Inaweza ikafika mpaka Sh.500; inategemea jinsi Wizara itakavyokuwa inashusha na malighafi hiyo itakavyokuwa inauzwa madukani ili vijana na akina mama wetu wamudu kununua bidhaa hiyo. Baadaye itafikia mpaka kupata bure, maana unaenda kununua kitu unaambiwa Sh.200 au Sh.500, si bure hiyo? Naomba Mheshimiwa hili aliangalie kila akija anapunguza bei mpaka tufikie katika malengo tuliyoyakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu halmashauri, ukurasa wa 54. Marekebisho ya Sheria ya Fedha Serikali za Mitaa, Sura Namba 290 kwa kuongeza kifungu cha 37A. Nakubaliana na maelezo ya Mheshimiwa Waziri, ni sahihi kwa sababu hii asilimia 10 inayokwenda kwa vijana na wanawake ilikuwa haina sheria lakini mtakapotungia sheria itakuwa ni lazima itendeke. Kwa hiyo, nawaomba TAMISEMI watengeneze kanuni haraka ili ziweze kutengenezewa sheria ije Bungeni ili tuwe na uhakika kwamba 10% ya vijana na wanawake ipo kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shida tunayoipa mkaona halmashauri hawatoi ni kwa sababu wanaona hawana panapombana ni maelezo tu ya maandishi. Isitoshe halmashauri zinajipangia miradi ambayo haina priority nyingi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, mengine nitachangia kwa maandishi. Naunga mkono hoja na Mheshimiwa hapa kazi tu, endelea na majukumu yako kama yalivyo.