Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Nianze kwa kusema naunga mkono hoja zote mbili. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya. Tunaelewa changamoto mlizonazo na kwa hali yetu hii tunaelewa lakini nasema hongereni sana kwa haya ambayo mnayafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia huko tulikotoka miaka 20 iliyopita maboresho ambayo yamefanywa consistently na Serikali hasa kuanzia Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne na yanayoendelea sasa ndiyo yamewezesha kuona mafanikio tunayoyaona sasa hivi. Jitihada za Serikali za kuhakikisha kwamba tunakuwa na uchumi wa jumla ulio tulivu, tunajenga mazingira mazuri ya uwekezaji na kufanya biashara, tunaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya barabara, umeme, maji, yote haya ndiyo yanawezesha mafanikio haya tunayoyaona. Mheshimiwa Waziri na timu yenu naendelea kuwapongeza sana pamoja na changamoto za rasilimali fedha ambazo tunazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii mikubwa ambayo Mheshimiwa Rais wetu ameanza kuitekeleza, pamoja na maneno mengi, hii ndiyo itakayochochea zaidi maendeleo yetu. Ujenzi wa reli ya kati kwa standard gauge na matawi yake muhimu, maboresho yanayoendelea sasa hivi katika bandari ya Dar es Salaam, niongeze hapo, siyo maboresho tu na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam lakini napenda tuanze ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo kwa sababu tunafahamu Bandari ya Dar es Salaam tayari imekuwa chocked. Tujenge bandari mpya ya Bagamoyo ambayo itakuwa ni kwa faida kubwa ya Taifa hili kwa miaka 100 inayokuja ili tuweze kushindana na tujenge mazingira ambayo yatatuwezesha kutumia nafasi yetu ya kijiografia kama vizuri kama nchi, tunaweza, tunaweza. Ndiyo maana Mwalimu alikuwa anatukumbusha wakati wenzetu wanatembea sisi tukimbie. Ndiyo maana ya kufanya uwekezaji mkubwa kama huu, ndio una gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia, ni vema tukachukua uamuzi haraka, tukapata a financing instrument itakayotuwezesha ku-fund reli ya kati na matawi yake tumalize mapema kuliko hii ya kwenda vipande vipande na tutaona jinsi uchumi utakavyokua kwa haraka. Hili linawezekana, ni ombi langu sana kwa Serikali, twende haraka na baadaye mtaona faida kwa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha tulilisema miaka minne iliyopita mamlaka ya nchi haiwezi ikajiondolea sovereignty yake. Nashukuru mmerejesha mamlaka ya Waziri wa Fedha ya kuweza kusamehe pale inapobidi miradi mikubwa kwa faida ya maendelao yetu, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, kwa miradi ambayo tayari iko kwenye pipeline maamuzi yafanyike haraka, twende mbele. Baada ya Bunge kama litakubali marekebisho haya tufanye maamuzi ya haraka. Matamanio yangu ni kuona Mradi wa Liganga na Mchuchuma unaanza kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha na ndiyo tutaona faida. Tukianza utekelezaji wa Mradi huo wa Liganga na Mchuchuma mtaona wawekezaji kwa upande wa PPP kwa eneo hilo maana mzigo upo. Ndiyo rai yangu kwa Serikali twende haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la Electronic Tax Stamp. Ripoti ya Kamati ya Bajeti ni nzuri sana mapendekezo yako wazi. Sasa hivi tunatumia stamp za kodi za karatasi na wanalipia nadhani kama dola moja. Kinachogomba hapa nilivyowasikia Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wamechangia kwenye eneo hili wanasema malipo ambayo atachukua mwekezaji hayawiani vizuri na kiwango cha uwekezaji wake na lingine ni ule muda wa miaka mitano. Bidhaa ambazo tulianza nazo na stamp hizi za kodi za karatasi, tunajua ni pombe kali, mvinyo, filamu za wasanii wetu hawa, pamoja na sigara. Pamoja na maeneo ambayo wameanza kutumia mfumo huu ambao una tija sana hawajabeba bidhaa zote kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri tuanze na bidhaa chache na hasa hizi ambazo tayari zilikuwa zinatumia mfumo huu. Pendekezo langu la pili ni kwamba viwango vya sasa vinavyotumika vya dola moja kwa stamp ya karatasi ndiyo viendelee kutumika katika mfumo huu. Tunaweza kuongeza hata bia lakini tusiingize bidhaa zingine kama maji, soda na juice, hapana, tusifike huko kwa sasa kwa maoni yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tukienda hivyo tutakuwa tumeliweka vizuri suala hili. Tunataka tujiridhishe na uzalishaji wa ndani wa viwanda hivi na baada ya pale tutaona, Serikali itakuja Bungeni itaonesha, pale ambapo mapato yatakuwa yameongezeka tutakuwa na hoja ya msingi ya kusema sasa twende mbele kwenye bidhaa nyingine, tukienda hivyo tutafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda mfumo huu mpya tufanikiwe kwa sababu haiwezekani leo Tanzania makusanyo yetu ya ndani yawe around 15 au 14.5 chini ya viwango tunavyovifahamu katika region hii vya kati ya 17 na wengine wameenda mpaka 20. Naomba sana tuunge mkono jitihada hizi za Serikali lakini tuanze na bidhaa chache ambazo tutazisimamia lakini pia viwango vinavyotozwa sasa ndivyo vitumike, tusiongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kutoongeza Ushuru wa Bidhaa na hili tumekuwa tukilisema na baada ya mwaka mmoja tutaona numbers. Napenda eneo hili Waheshimiwa Wabunge Serikali ituelewe, tusiwe tunaenda mbele halafu tunarudi, tuwe very consistent tulee manufacturing industry ya Tanzania bado contribution yake kwenye pato la Taifa ni ndogo sana ya asilimia 5 tunapenda ipande kwa haraka kwa asilimia 10 mpaka 15 na mtaona faida ya uchangiaji wake katika uchumi. Tukienda na hatua hizi za kwenda mbele na kurudi hatutaona tutakuwa tunarudi pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho naomba tuwekeze katika sekta ya kilimo kwa upana wake. Land bank ambayo tumeizungumzia kupitia TIC tufike mwisho, maeneo hayo yapatikane na tukaribishe wawekezaji wakubwa. Wawekezaji wadogo hawa wakulima wetu wametusaidia mpaka sasa lakini ili kwenda kwa kasi kubwa kwenye kilimo lazima tukaribishe wawekezaji wakubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ubarikiwe sana kwa kunipatia nafasi hii, naunga mkono hoja.