Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii. Kwanza kabisa napenda kumwomba Waziri wa Fedha na Naibu Waziri wa Fedha watupe taarifa sahihi, nzuri na itakayoturidhisha ambayo tutaweza kwenda kuwaambia wananchi wetu kuhusiana na suala zima la shilingi trilioni 1.5. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili mtaliona kama dogo mkiwa mmekaa kwenye viti vyenu lakini mkienda kule kwa wale ambao mnadhani hawajui masuala ya uchumi ni zito na ni kubwa na wanahitaji majibu ya kuridhisha. Mheshimiwa Naibu Waziri alitujibu hapa hata sisi Wabunge wengine ambao hatujui masuala ya kiuchumi tunajiita mabushi uchumi hatukumuelewa alichotuambia. Watakapokuja kumalizia tunaomba watuambie na watupe kauli ya Serikali wapi iko shilingi trilioni 1.5? Ili na mimi nikitoka hapa nikienda kumwambia mwananchi wangu wa Itonjanda kule Tabora aelewe hii shilingi trilioni 1.5 imetumika vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye bajeti. Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hatua yake ya kuamua kwenda kwenye Kiwanda cha Urafiki. Sisi kama wajumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira tulikwenda pale na yale aliyokutana nayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ni masuala ambayo na sisi kama wana Kamati tulishauri na tuliiomba Serikali iende pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda kile Serikali ya Tanzania inakimiliki kwa asilimia 49 na China inamiliki kwa asilimia 51. Kwa yanayoendelea pale, tungeiomba sana Serikali na kwa sababu na Waziri Mkuu amekwenda ni afadhali tukamiliki sisi wenyewe ili tuweze kupata faida inayotokana uzalishaji ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, demand ya nguo za Kiwanda cha Urafiki ni kubwa sana nchi kwetu kuliko hata ambavyo watu wanafikiria. Siku tulipokwenda pale tulikuta msururu wa magari umepaki pale unasubiri mzigo utoke kiwandani ili waweze kusafirisha. Cha ajabu mzigo hakuna kwa siku wanatengeza khanga chache na nafikiri ndani ya miezi sita ama saba iliyopita walishafunga kabisa hata huo uzalishaji. Hayo ambayo Waziri Mkuu alitaka kuyajua hata sisi Kamati tuliuliza mashine zetu mmepeleka wapi? Hizi mlizoleta mbona hamjazifunga mnasema ni mbovu, leteni zile za kwetu kwanza halafu na hizi mlizonunua ambazo ni mbovu zirudisheni mtuletee nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wizi wa hali ya juu katika nchi hii. Wakati Waziri wa Viwanda akisisitiza viwanda aanze na Kiwanda cha Urafiki ambacho tunamiliki asilimia kubwa sana, asilimia 49 siyo mchezo, hiyo asilimia moja kuichukua ni rahisi sana tukisema jamani sasa ninyi basi mmeshindwa kuzalisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna viwanda vya khanga Morogoro vya Textile, viwanda vya khanga vya Nida, vinafanya kazi vizuri sana na ukienda sokoni khanga za Nida na Morogoro ni nyingi ziko wapi khanga za Kiwanda cha Urafiki? Kwa nini Nida na Morogoro wanaweza Urafiki wanashindwa? Lipo tatizo na tatizo hili tunaomba liangaliwe. Tunamshukuru Waziri Mkuu ameingilia kati tunaamini kabisa sasa hivi Urafiki itaanza kufanya kazi kwa faida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee kuhusu Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe. Hili neno la Liganga na Mchuchuma nimekuwa nikilisikia toka nikiwa binti mdogo sana. Kwanza nilikuwa naona kama ni kitu fulani cha kuchekesha, nilikuwa sielewi lakini nimeelewa hii Liganga na Mchuchuma ni kitu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la makaa haya ya mawe linakadiriwa kuwa na zaidi ya tani milioni 428 na wanasema tunaweza kutumia kwa takribani miaka 500 kwa mujibu wa NDC. Chuma kiko zaidi ya tani milioni 126. Hivi ndugu zangu utajiri huu wote tulionao toka tumeanza kusikia Liganga na Mchuchuma, hatujawahi kusikia tumepata mafanikio gani kwenye hili. Hivi hizi pesa ambazo tunazitoa kutakwenda kununua Bombardier, kujenga viwanja vya ndege, kujenga kuta Mererani kwa nini tusiwekeze kwenye mradi huu ambapo tutapata faida kubwa na ya haraka kabisa. Ndugu zangu tutakapochimba wenyewe chuma chetu tutapata faida kubwa kwelikweli katika hii nchi ya Tanzania ya viwanda ambayo tunaizungumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na kauli mbiu ya Tanzania ya Viwanda na imekuwa ikizungumzwa sana. Mpaka tunakwenda kumaliza bajeti hii, Wizara hii imepata asilimia 9 peke yake ya fedha za maendeleo. Halafu tunasema hii ni Tanzania ya Viwanda, ndugu zangu Tanzania ya Viwanda ipi? Asilimia 9 peke yake kwenye fedha za maendeleo halafu tunajinasibu kwamba Tanzania ya Viwanda, kwenye viwanda vipi? Watendaji wa Wizara ukiangalia maelezo yao na taarifa zao wana mikakati mizuri kwelikweli ya kuijenga Tanzania ya Viwanda lakini hawana pesa. Kwa nini tusiwasaidie ili waweze kutimiza azma ya Mheshimiwa Rais ya Serikali ya Viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo kumekuwa na fungua fungua ya viwanda vingi sana, tunaambiwa tuna viwanda 3,306, mimi sijawahi kuviona na Mheshimiwa Mwijage anajua hatujawahi kuviona lakini takwimu ndiyo zinavyosema na zinavyoonyesha. Viwanda hivi pamoja na kufunguliwa lakini vipo vingine ambavyo vinafungwa kutokana na ukiritimba wa mambo mengi ikiwepo mambo ya kodi za hovyo hovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa kwenye Kamati lilikuja suala la sukari ya viwandani. Naomba hili niwaambie Wizara ya Fedha, mambo haya mnayafanya mwisho wa siku ng’anya linakuja kuwashukia Wizara ya Viwanda. Ninyi ndiyo mnatakiwa mtoe vibali na msababishe sukari ile iweze kutolewa mwisho wa siku hamtoi na kusababisha viwanda kufungwa. Kiwanda cha Sayona kilifungwa kwa sababu kilikosa sukari. Matokeo yake unaambiwa Wizara ya Viwanda haifanyi kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliletewa list ya viwanda 10 ambavyo walisema tayari vimeshapata vibali vya kutolewa sukari, lakini mpaka tunamaliza kikao cha Kamati walikuwa hawajapata. Nami naendelea kushauri Serikali, kama hawa wafanya biashara wanashindwa kulipia kodi za pale bandarini tengenezeni bonded warehouse muweke hizo sukari ili hawa wafanyabiashara wakishakuwa tayari waweze kuchukua mzigo wao wafanye biashara. Leo mmezuia, mnawadai madeni makubwa ambayo na wao wanashindwa kufanya uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine kuna sababu gani ya sukari hii isitozwe kodi ili kupunguza huu urasimu ambao mnausema, mnauona, mnaudai na mnaujua. Kwa nini msitoze kodi? Kwa nini msifanye kama sukari ya kawaida inayoingia ili mfanyabiashara ajue nikiagiza sukari ya kiwandani nitalipa kodi kuliko ilivyo hivi sasa hawalipi kodi lakini mwisho wa siku kumekuwa na urasimu wa hali ya juu. Hali ni mbaya, baadhi ya wafanyabiashara ambao wanaotengeneza bidhaa zinazotumia sukari wanahangaika, wanateseka kupata hiyo sukari waambieni kama kuna kodi waweze kulipa ili maisha yao yaweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusu suala la biashara. Watu wanafunga biashara kwa sababu kuna mambo yanayowakera. Mimi kama mfanyabiashara niambieni natakiwa kulipa kodi kwa mwaka kiasi gani nilipe, nikishamaliza hapo niacheni nifanye biashara yangu. Leo kumekuwa kuna ufuatwaji wa wafanyabiashara mpaka inaleta kero. Kuna baadhi ya wafanyakazi wa TRA wasiokuwa waaminifu, mmewatengenezea mazingira ya rushwa ya ajabu, Mheshimiwa Dkt. Mpango nilimwamba hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wafanyabiashara na wafanyakazi wa TRA wamekuwa wanachukua watu wanakwenda kwenye maduka, ananunua kitu cha Sh.20,000 au Sh.50,000, nimeshuhudia mwenyewe kwa jicho langu, anaambiwa subiri risiti anasema nina haraka. Dakika tano nyingi anarudi na watu wa TRA wanakwenda kumdai mtu Sh.3,000,000 kwamba hujatoa risiti, nimelishuhudia mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanapoomba hizo Sh.3,000,000 wakiona mfanyabiashara hataweza kulipa hela hiyo wanaomba rushwa. Kauli wanazotumia wanasema utatoa mita, ukiambiwa kutoa mita ni Sh.1,000,000, ukiambiwa kutoa nusu mita ni Sh.500,000. Mimi ni mwakilishi wa wananchi niliuliza hilo suala na Mheshimiwa Dkt. Mpango TRA wapo wengi, hawa vijana mnaowatuma kwenda kufanya hiyo shughuli huko wanakera sana wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna sehemu iliyokuwa na tatizo la kupata mlango wa biashara kama Kariakoo. Leo milango Kariakoo inatangazwa. Ukifika unaambiwa mlango huu unakodishwa watu wamefunga biashara zao.