Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kuungana na wale wote ambao wamepeleka pongezi zao kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. Pia nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote kwa kutuletea bajeti ambayo kwa kweli kwa kiasi kikubwa sana inaakisi yale mawazo yetu tuliyoyatoa na Mheshimiwa Waziri ameya- accommodate mengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi Wabunge tumekuwa tukiambiwa sana kwamba tumekuwa Wabunge wa kutumia, kila siku tunadai hospitali, shule, barabara na kadhalika hatuji na mawazo mbadala namna gani Serikali inaweza ikapata mapato. Katika mchango wangu wa leo najikita zaidi kutoa namna mbadala ambapo Serikali inaweza ikapata mapato mengi sana na ndiyo utakuwa mchango wangu kwa siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kule nyumbani. Mheshimiwa Waziri tuliteta siku moja lakini naomba leo niliweke hapa hadharani na naomba sana alifanyie kazi. Kule Mafia tuna Taasisi ya Hifadhi ya Bahari inakusanya maduhuli, si wajibu wao, wanaifanya kazi ile siyo kwa ufanisi mkubwa. Niliomba maduhuli yale kutokana na watalii wanaoingia Kisiwani Mafia yachukuliwe na TRA maana ndiyo wataalam wa kukusanya mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Taasisi ya Hifadhi ya Bahari tunaitwika kazi nyingi. Kazi yake iwe ni kuhakikisha kwamba wanahifadhi mazalia ya samaki na shughuli nyingine za mambo tengefu yale. Mambo ya mapato wangechukua TRA, kuna kama shilingi bilioni mbili mpaka shilingi bilioni tatu kwa mwaka, kama mtatuletea TRA tutapata mapato mengi. Ofisi ya TRA ipo pale Mafia, wanaweza kukusanya yale mapato na Serikali ikapata pesa nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nimemuona hapa Waziri wa Nishati. Pale Mafia tuna kisima cha gesi kilichimbwa takriban miaka 10 au 15 iliyopita na Kampuni inaitwa M&P - Maurel and Prom, mwanzo waligundua kuna gesi nyingi sana pale lakini baadaye kukawa na technical problems hawakuweza kuendelea na kazi ile. Walipokuwa tayari sasa kwa ajili ya kuanza kuchimba na kuipata ile rasilimali ya gesi iliyopo Kisiwani Mafia, leseni yao ikawa imekwisha. Mpaka leo hii wanahangaika TPDC, Wizarani na kila mahali ili waweze ku-renew ile license yao waweze kuendelea na uchimbaji wa gesi ambayo imeonekana ipo nyingi sana katika Kisiwa cha Mafia. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati namwona hapa wahakikishe kwamba wanaharakisha huu mchakato wa hii kampuni ya M&P wapate hii license waje wamalizie kazi ambayo tayari walishaianza pale Kisiwani Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka niishauri Serikali namna bora ya kupata mapato ni eneo la uvuvi hususan katika bahari kuu. Nilipata bahati na heshima kubwa ya Mheshimiwa Spika kuwemo katika Kamati ile ya masuala ya Uvuvi wa Bahari Kuu. Tumeona mambo mengi lakini kwa ufupi tu ningeomba kumshauri Waziri wa Fedha muende mkaitafute ripoti ile, siwezi ku-summarize yale yote kwa muda huu wa dakika hizi chache nilioupata hapa lakini kuna habari nzuri sana mle ambazo zinaweza zikaisaidia Serikali yetu kupata mapato mengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa ufupi tu kuna suala la bandari ya uvuvi na hili limezungumzwa sana. Mwaka wa Fedha 2014/2015 zilitolewa shilingi milioni 350 na Wizara ya Fedha kwenda Wizara ya Uvuvi ili kuanza masuala ya usanifu ili kuhakikisha kwamba bandari ile inajengwa lakini zile pesa sijui zilipotea wapi. Mwaka jana hii bajeti tunayoimaliza kesho kutwa zimetengwa shilingi milioni 500, hazikuwahi kutoka kutokana na makusanyo madogo. Bajeti hii zimetengwa shilingi milioni 500 nyingine kwa ajili ya usanifu wa kujenga bandari ya uvuvi lakini mpaka sasa bado haijaamuliwa site itakuwa wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kuishauri Serikali kwa kuwa tayari tuna mradi wa kujenga Bandari ya Bagamoyo, kwa nini msiunganishe Bandari ile ya Bagamoyo kukawa na section ya bandari ya uvuvi? Tunakosa mapato mengi sana katika uvuvi ule wa bahari kuu kwa sababu tu hatuna bandari ya uvuvi. Bandari ya uvuvi multiplier effect yake ni kwamba value chain yake ni kubwa sana inaweza ikatusaidia sana kupata mapato mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tulizungumza habari hapa ya kuwa na meli ya uvuvi, sikuliona suala hili katika bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, sijui wazo lile limefia wapi. Tuwe na meli zetu wenyewe ambazo zitakwenda mpaka kwenye maji ya kina kirefu kwa ajili ya
kupata mazao mengi ya uvuvi. Tumewaachia makampuni ya nje, yanakuja yanachuma, yanaondoka na bahati mbaya sana na katika eneo hili Mheshimiwa Naibu Waziri nimemuona, wahakikishe wanawaambia TRA basi walau waweke mechanism nzuri ambayo itatoza kodi katika hizi meli kubwa ambazo zinatoka nje, zinakuja hapa kwetu, zinavuna rasilimali lakini TRA hawakusanyi hata senti tano. Kwa hiyo, ni eneo ambalo tunaweza tukasema ni oevu, mnaweza kuangalia namna gani mnaweza mkaongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi kulikuwa na sakata hapa la kupima samaki kwa rula. Mimi natokea Mafia, sisi ni wavuvi, kimsingi bajeti hii kwenye uvuvi wametusahau, hakuna kitu, kuna asilimia 0.01ya pesa zimewekwa pale kwa ajili ya mambo ya maendeleo kwenye tasnia hii ya uvuvi, kwa hiyo, tuna tatizo kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi navyozungumza na bahati nzuri nimemwona Waziri wa Uvuvi kule Mafia kimsingi tuna kiwanda kikubwa sana cha kuchakata samaki pale cha wale Tanpesca na Alpha Logistics, kinakaribia kufungwa. Walikuwa kila mwezi wanaondoa pale tani 20 mpaka tani 25 za samaki lakini kutokana na haya matamko yaliyokuja sasa hivi kiwanda kile kinashindwa kutoa samaki kwa sababu kuna samaki aina kama ya misusa, ngalala, hao ukubwa wao hakuna namna wanaweza wakaongezeka zaidi ya hizo sentimeta mnazozitaka ninyi. Kwa hiyo, wale ndugu zetu wa Tanpesca wamekataa kununua samaki kutoka kwa wavuvi wadogo kwa kuhofia kwamba huenda wakakamatwa. Hawa samaki niliowataja Mheshimiwa Waziri akae na wataalam wake waruhusiwe kuvuliwa kwa sababu hao samaki hakuna namna wanaweza wakaongezeka ukubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni ile ilikuwa kila mwezi wanaleta tani 20 mpaka tani 25 sasa hivi huu mwezi wa tatu meli haijaja kwa sababu samaki wote wanaokwenda kule wanakuwa ni reject. Siyo wanakuwa reject kwa sababu labda umri haujafika, hapana! Hawa samaki kwa maumbile yao hawawezi kufika hizo size ambazo Wizara imeziweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na kuwa Serikali ina nia njema ya kuhakikisha kwamba tunapamba na uvuvi haramu, naomba Waziri au wataalam wake waende Mafia, wakae na wavuvi, waangalie ni aina gani ya samaki wanakua kiasi gani. Kwa sababu mnatoa matamko au sheria lakini msiangalie kwamba samaki duniani au hapa Tanzania wapo kwenye maziwa tu kwenye bahari kuna species mbalimbali za samaki na zinakuwa na ukubwa tofauti ambao hauwezi kufikia pengine hivyo viwangowanavyovizungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo suala la utalii. Sisi Mafia kule pamoja na uvuvi, kitu kingine kikubwa kule ni utalii lakini accessibility ya Mafia ni kama haipo, kwa sababu usafiri una matatizo. Nashangaa sana, bahati mbaya watu wa Uchukuzi hapa hawapo, lakini Bakhresa ameipa Serikali meli ile (sea bus) ije Mafia. Meli ile ina matatizo madogo tu ya kurekebishwa lakini mpaka leo Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi bado wanaendelea na taratibu tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Mafia wanateseka, hakuna usafiri, wanapanda boat mbovu ambazo siyo salama, wanahatarisha maisha yao, lakini Serikali imeshapewa boat kinachotakiwa ni logistics za kumaliza ili kuhakikisha kwamba ile meli inakuja Mafia na inaanza kazi. Kwa bahati mbaya sana ndugu zetu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wanasuasua. Kwa nini hawataki kuiruhusu ile meli ikaja kuanza kazi Mafia hata kesho kutwa, kwa sababu tumepewa bure tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.