Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kupata nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Waziri, nitaunga mkono hoja yake kwa mara ya mwanzo iwapo ataturidhisha kwa majibu ya maswali yetu tunayoyatoa hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la TRA. Wafanyabiashara wa Tanzania wanateseka sana kwa matatizo yanayosababishwa na Maafisa wa TRA. Kilio cha Waheshimiwa Wabunge ni matokeo halisi ya kinachofanyika huko nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Jiji Kuu la kibiashara la Dar es Salaam, maeneo ya Kariakoo, fremu nyingi zimefungwa na wafanyabiashara wameamua kuacha kufanya biashara kutokana na manyanyaso yanayotokana na TRA. Maafisa wa TRA wanajipa uwezo mkubwa wa kuandaa mazingira, Mheshimiwa Hawa amezungumza vizuri, nami namuunga mkono sana kwa alichokizungumza. Bahati nzuri kafikia mpaka kuwa shahidi wa matendo ya udhalilishaji wanayoyafanya baadhi ya Maafisa wa TRA wasio waaminifu kwa wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara hususan wadogo wadogo wa nchi hii ni watu ambao wanajiandalia mazingira; maana mitaji yao kuanzia mwanzo wa biashara zao ni watu ambao hawana msaada wowote unaotokana na chanzo chochote cha Serikali, ni jitihada zao binafsi zinazowafikisha mpaka kupata mitaji wakaanzisha biashara zao ndogo ndogo. Bahati mbaya sana mfanyabiashara huyo mdogo wa Tanzania, anapopata wazo tu la kufanya biashara, anapoenda TRA kutaka kuanza hiyo biashara yenyewe, kwanza anaambiwa lipa kodi ya mapato. Hata biashara hajaifanya anatakiwa kulipa kodi. Kuna kitu kinaitwa clearance, hiyo huwezi kuipata kama hujalipa kodi ya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niwaulize TRA, kodi ya mapato iliyotokana na nini? Hebu mtuambie, hiyo kodi ya mapato inatokana na nini? Ana wazo la kufanya biashara, anaenda kutafuta certificate zinakazomruhusu kufanya biashara lakini anaambiwa kwanza lazima ulipe clearance, ulipe nini, umepata nini na kutoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo ya kufungwa fremu za Kariakoo siyo tija kwa TRA wala kwa Taifa. Matokeo ya wafanyabiashara kuhama nchi wakaenda kufanya biashara nchi za jirani siyo tija kwa Taifa hili. Mnapofanya jitihada za kuongeza mapato, lazima mzingatie mambo haya muhimu sana. Busara itumike katika kukusanya kodi, pia lazima kodi zetu ziendane na uhalisia wa kipato cha anayelipishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vitu vya ajabu sana. Nataka kutoa mfano mdogo. Leo hii ukileta kontena la vitenge kutoka nje, kodi inayotozwa na TRA kwa takwimu zao na hesabu zao, ni karibia shilingi milioni 80, kontena moja. Matokeo yake wafanyabiashara wanaingiza vitenge lakini kinachofanyika inakuwa ni transit goods, zinaishia nchi jirani ya Zambia. Kontena zinaenda Zambia na Uganda. Wanafungua kule na wanazirejesha ndani ya nchi yetu kwa njia za vichochoroni, njia zisizo rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda leo Kariakoo utakuta vitenge vya nje vingi vinauzwa lakini nenda kwenye taarifa za TRA uone ni kontena ngapi za vitenge zimelipiwa, mtakuta hamna lakini kwenye soko la vitenge Kariakoo vimejaa tele. Kwa sababu ukienda Zambia kontena la vitenge haliwezi kuzidi shilingi milioni 20, lakini ninyi mmejiwekea kodi ya shilingi milioni 80, mmetaka yote, mmekosa yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, bidhaa ya magari yaliyotumika. Sheria za Kodi zilizoweka viwango, sina tatizo, asilimia 25 ni import duty, excise duty zote siyo tatizo. Tatizo linakuja kwenye valuation ya gari iliyotumika kutoka nje. Hivi tokea lini kitu cha kununuliwa mnadani TRA wanakiwekea valuation, yaani hiyo ni bei ambayo haitikisiki. Umeona wapi? Kitu cha mnada maana yake inategemeana na bei ya soko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Suzuki Carry hata uki-google hapo utaikuta Japan inauzwa dola 500, 700 mpaka 1,000. Rudi kwenye tariff za TRA, utaikuta imewekewa valuation ya dola 3,000. Maana yake akileta gari lile maana yake analipia kodi ambayo siyo halali kwa sababu sheria inataka valuation itozwe kulingana na viwango vya kodi ya TRA. Sasa vitu vya mnada toka lini vikawekewa indicative price ambayo inatumiwa na TRA? Hii inasababisha watu watafute njia nyingine za vichochoroni kupitisha magari yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii gari aina ya Land Cruiser V8 ushuru wake unafikia shilingi milioni 80. Tembea, Land Cruiser zote zilizopo nchini, asilimia 90 ni ya msamaha wa kodi, ni la Msikiti, Kanisa hata kama wanaoendesha siyo wenyewe. Hii ni kwa sababu ya kodi ya shilingi milioni 80 laiti kodi ingewekwa shilingi milioni 25, 30 au 40 watu wangelipa, lakini mnataka nyingi, mnakosa vyote. Tuliache hilo, lakini nawaambieni tena, rudini muangalie, Maafisa wa TRA wanachowafanyia wafanyabiashara kinawaudhi na tena kinakera na sisi wawakilishi wao tunasema na naomba mchukue hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie kilio ambacho wenzetu wa Kusini wanalia sana. Tunaapa hapa kila asubuhi, tunamwomba Mungu kwa dua kwamba tuwatendee Watanzania haki na tunamwombea sana Rais wetu Mungu amwongezee hekima ili yeye na sisi tunaoshauri tutimize haki kwa Watanzania. Watu wa Mtwara au watu wa Kusini wanalia kilio hiki kwamba pesa zao wenyewe mnazizuia, humtaki kuzipeleka wakaendeleza maisha yao, nia ya Waziri ni nini kwa wananchi wa Kusini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamdhihaki Mungu kwa sababu tunapomlilia Mungu kwa kiapo na tunapoanza harakati zetu kwa kiapo cha kuwatendea haki Watanzania, tunakuwa tunamshtakia mambo yetu Mungu leo tunamdhihaki Mungu. Mheshimiwa Jenista ni hodari sana kusimama anapodhihakiwa Mheshimiwa Rais hapa lakini sio hodari wa kusimama anapodhihakiwa Mungu kwa kutowatendea haki Watanzania, hata kidogo. Akiguswa Mheshimiwa Rais, najua anatimiza wajibu wake lakini tutimize wajibu, asidhihakiwe Mungu kwa kutokuwatendea haki Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanacholilia watu wa Kusini ni haki yao, siyo kwamba wanaomba, ni chao wenyewe. Serikali inayosema imeongeza makusanyo, uchumi umekua, mko vizuri lakini nawaambieni, kama uchumi kukua ni hivi, maisha ya Watanzania yalivyo, ni afadhali ule utawala wa Mheshimiwa Kikwete uliopita ambao ulionekana unawapigaji, una wanaosafiri nje sana, kuna hewa nyingi lakini bado tija kwa Watanzania ilionekana. Serikali iliyodhibiti leo watumbuaji wanatumbua mpaka pesa za wakulima wa korosho wa Kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.