Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Wilfred Muganyizi Lwakatare

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Bukoba Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa wale ambao hawanifahamu vizuri, niliwahi kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ndani ya Bunge hili. Nikiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, nilipata bahati kwa miaka mitano kusimamia bajeti mbadala ya Kambi lakini pia kuzisikiliza bajeti mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na Mawaziri wa Fedha na Mipango. Sikuwahi kusikia Waheshimiwa Wabunge na hasa wa upande wa Chama Tawala kwamba kuna Kambi ambayo haikupewa mashadidio kushadidiwa maana siku zote wamekuwa wakisema hii bajeti ni kiboko, haijawahi kutokea, ni funga kazi, ni mwarobaini wa matatizo mpaka bajeti ya mwaka huu wanasema haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mtu kama mimi mzoefu ambaye niliwahi kuwa ndani ya Bunge hili, ni kati ya ma-veteran wachache ambao nilichukua likizo kidogo kwenda kuchungulia wananchi wanaendeleaje halafu nikarudi, maneno haya huwa nayasikiliza kama swaga. Kwa hiyo, hayanipi matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikirejea maneno ya Mheshimiwa Spika juzi juzi hapa wakati hotuba iliposomwa, Mheshimiwa Spika, akasema angetaka maelezo fasaha kutoka kwa Mheshimiwa Mpango kwamba kwa nini bajeti ya Kenya pamoja na idadi ndogo ya watu inakuwa karibu mara mbili ya bajeti yetu? Ni bajeti ambayo uki-combine ya Uganda, Tanzania na Rwanda na vichokochoko vingine, ndio bajeti ya Kenya?

Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ni mepesi. Tatizo letu sisi tunafanya business as usual. Halafu naingiwa na wasiwasi, kwa capacity ya watu wetu; capacity ya wataalam, Mawaziri wetu, watu wanaomshauri Mheshimiwa Rais na siyo kwa awamu hii ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli, ni awamu zote tangu siku za nyuma. Ukiangalia bajeti za miaka ya nyuma, bajeti imekuwa inapanda lakini matatizo kwa nini ni yale yale? Huwa nafika mahali najiuliza, hawa wataalam wetu wanasoma shule gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nimewahi kusoma mahali, kuna Profesa mmoja wa nchi ya Norway; nitakapokumbuka citation nitaitafuta, anasema vijana na wasomi wa Kitanzania wanajua sana kukariri vitu ambavyo sometimes siyo lazima wavi-apply, kwa hiyo, ni watu ambao wamebobea kwenye theory. Nilipokuwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, kulikuwa na mwanafunzi mmoja, ukienda library utakuta amepanga vitabu vinamzidi hata urefu, vingi tu, lakini ukija mtihani akijitahidi sana anaambulia karai. Yule bwana alikuwa anasifika, halafu anabeba vitabu kweli kweli. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana nilikuwa mahali ninakokaa, nikajaribu kupanga vitabu ambavyo nimepewa hapa Bungeni, yaani mimi ni mrefu, sasa hivi vimenifika kwenye bega. Watanzania tunajua kuandika, mipango iko kwenye makaratasi, lakini unapokuja kwenye ku-practise pale ndipo tunatofautiana na wenzetu wa Kenya. Hapa tunazungumza mno vitu ambavyo vingine hata yule anayevisema haviamini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwa nasikiliza sana, japo huwa sina bahati ya kupata nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza na huenda nitahama hapa ninapokaa. Huwa nasikiliza linapigwa swali pale unakuja kusikiliza majibu; samahani, kwa mtu kama mimi naona hili jibu ni bora twende, kwamba leo lipite tukutane kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu huo, kwa staili hii tunayokwenda nayo, mfumo huu tunaokwenda nao wa kibajeti, kwa sababu ni mfumo ambao unaweza ukau- refer kuanzia miaka ya nyuma, wala siyo awamu hii tu, tunakuwa na bajeti ambazo hazitekelezeki. Tunakuwa na maneno ambayo ni matamu kuyasikiliza, lakini unapokuja kwenye practise hayapo, huwezi ukayapata yote kiasi kwamba nasema hata Mheshimiwa Dkt. Mpango tungekuwa na uwezo wa kumpitishia bajeti ya shilingi trilioni 200, haki ya Mungu kwa utaratibu na mfumo huu, nchi hii hatubadiliki, hatutoki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Kenya mtu kuja kuwa Waziri, anachujwa na vitu vingi mno. Kwanza capacity yake yeye mwenyewe, yeye vipi? Mambo aliyonayo kichwani, je, anayaamini? Je, anaweza akayaweka katika vitendo na utekelezaji? Ndipo unampata mtu kweli anayeweza kusimama na maneno ambayo anayazungumza humu. Wengi hapa huwa wakijibu maswali, wakitoa mipango mbalimbali, wakisoma matamko unamwona kabisa huyu mtu ni mwongo yaani unamsoma kabisa ni mwongo yaani hata kile anachokizungumza hakiamini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba tubadilike, tuanzie hapo, tubadilike. Tuwe na mapinduzi ya kifikra na mapinduzi ya Bunge jipya ambalo linakwenda na hiyo three line whip kwamba ni dhamira ya mtu mwenyewe na ndiyo capacity yake na mitizamo yake na mtazamo wa Chama chake na Taifa lake. Hapa over 95% unakuta ni dhamira ya kichama, that is a major problem, kiasi kwamba mtu anaweza akawa na nondo zake, ni Profesa, Doctor, ana Masters, lakini unamwona kabisa kwa sababu ya dhamira moja kubeba 95% inamsababishia azungumze kitu ambacho hata yeye hakiamini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumza na wananchi wangu wa Bukoba. Kule Bukoba Town tuna ile mialo ya Bakoba, Kahororo na Custom, watu wamezoea miaka yote tangu nizaliwe wanakwenda kuvua samaki kwa kutumia ndoano. Kuna kijana mmoja akanipigia simu jana, akasema Mheshimiwa Lwakatare, hebu tuambie nikiweka ndoana kule niweke na bango kwamba kama huna sentimita 25 usiguse? Nimekosa jibu la kumjibu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo tunalolipata, tunapotunga sheria, kwanza naamini sheria nyingi tuna-copy na ku-paste, ni matakwa ya Wazungu. Kwa sababu, Wazungu kwenye viwanda vyao wanataka samaki awe na sentimita 25 au sentimita ngapi, tukija hapa hatutumii hata loophole ya nguvu tulizopewa za kanuni. Naamini kama Mheshimiwa Waziri anaona sheria ni ya jumla sana na haitekelezeki katika mazingira yetu, basi atumie loophole ya Kanuni aweke na vigezo ambavyo vinaendana na maisha yetu ya kila siku na maisha ya watu wetu, lakini tukienda tu, yaani ni gari linakwenda lakini halijui kwamba kuna reverse na kona, haki ya Mungu wataumia wengi. Huu mtindo wa mzigo ufike, punda asife, tuache kuutumia tunawaumiza watu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Marehemu Mwalimu Nyerere, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi, aliwahi kusema kwamba mtu akikuletea vichupa vilivyosagwa vinang’aa akakwambia kwamba hii ni almasi na anataka uamini kuwa ni almasi, wewe utakuwa ni zuzu yaani ukikubali anaokuona wewe ni zuzu. Mimi huwa ni mtu wa mwisho kutoamini kitu ambacho unaona kabisa dhahiri hakipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Dkt. Mpango weka vitu ambavyo vinatekelezeka kwa elimu yako uliyonayo, usisikilize watu.