Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Anna Joram Gidarya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika bajeti hii kwa manufaa ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kunukuu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 8(1), inasema:-

“(a) Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.

(b) Lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi; na

(c) Serikali itawajibika kwa wananchi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii imeletwa na tunaisifia ni bajeti nzuri. Maandishi ni mazuri, matendo ni mabaya kuliko tunavyofikiria. Hata Biblia inasema, heri yule aliyejenga juu ya mwamba kuliko yule aliyejenga juu ya mchanga. Ndugu zangu Taifa linaenda kuangamia. Uchumi wa Taifa unaenda kuangamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, simulizi hizi za kusema uchumi umepanda amepata wapi? Wizara ya Kilimo mwaka 2016/2017 mpaka Machi fedha zilizopelekwa ni shilingi bilioni 2,252 sawa na asilimia 2.22, asilimia 98 ya bajeti haikutekelezwa. Katika Wizara ya Mifugo, makadirio yalikuwa ni shilingi bilioni 4 lakini pesa iliyotolewa ni shilingi milioni 130 sawa na asilimia 3.25, asilimia 97, haikutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye maji, pesa zilizotengwa ni shilingi bilioni 913, iliyotolewa ni shilingi bilioni 230,997 sawa na asilimia 25, asilimia 75 haikutekelezwa. Hizi ni simulizi alizoandika Mheshimiwa Dkt. Mpango kwenye kitabu hiki. Kama hizi za huku nyuma zimeshindikana kutekelezwa lakini amekuja tena na 2017/2018 Mifugo na Uvuvi wametenga fedha ileile ya mwaka 2017 lakini pesa iliyotolewa mpaka sasa ni sifuri. Hizi ni simulizi, Watanzania wana hali mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Mheshimiwa Waziri hamshauri Rais wakasimamia hata kwenye zile ahadi 10 za Mheshimiwa Rais? Mheshimiwa Rais wakati wa uchaguzi alitoa ahadi 10. Kwanza, alisema ataboresha mfumo wa kiutendaji Serikalini. Pili, ataboresha Huduma za Afya. Tatu, ataboresha maslahi ya wafanyakazi lakini wafanyakazi wameishia kutumbuliwa, wala hawajaongezewa hata senti tano kwenye mishahara yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya nne alisema, anaboresha elimu na elimu bure. Elimu bure imekuwa ni majanga katika Taifa letu. Ahadi ya tano alisema ataboresha maji, maji yako wapi? Namuuliza Mheshimiwa Dkt. Mpango, bajeti ya maji iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya sita akasema ataboresha kilimo, uvuvi, mifugo na viwanda. Kilimo na Mifugo ndiyo hiyo ya sifuri sifuri. Mheshimiwa Dkt. Mpango ameleta simulizi isiyosahaulika ndani ya Bunge. Saba, Mheshimiwa Rais alisema kuwe na kipato kizuri cha kuongeza uchumi, uchumi uko wapi? Nane, akasema kuongeza fursa za ajira, ajira ziko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya tisa akasema, kupunguza tozo na kodi zisizo za lazima hasa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo. Sasa tozo imekuwa ni mwiba, mshike mshike mtaani. Watu wanaingia wanakagua mpaka draw za watu. Umetusakizia mbwa mkali wa mapato, TRA. Leo hii mpaka mabeseni ya vitunguu yanakamatwa, ukiwa na nyanya tano, ushuru, ukiwa na nyanya 10 ushuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mpango, asifikiri tunamchukia, tunamwambia kwa sababu Bunge ndilo lenye dhamana ya wananchi. Vichwa vyote hivi unavyoviona, watu hawa wanajibika kwa Watanzania. Kwa nini Waziri mmoja tu aliangamize hili Taifa? Baba yangu yangu Mheshimiwa Waziri tulia, kaa, mshauri Mheshimiwa Rais, timizeni hizi ahadi. Hizi bajeti za kisekta zinaendana na ahadi za Mheshimiwa Rais, kwa nini hamtaki kumshauri? Mnasema viwanda, viwanda mtavipata wapi wakati kwenye kilimo kuna sifuri, elimu ndiyo hakuna, kila siku tunalalamika.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tozo za TRA ambazo zinatuletea shida, TRA wamekuwa kama wezi. Umetoka na TV yako nyumbani unapeleka kwa fundi, anakwambia nipe risiti. Mimi nimenunua TV tangu mwaka 2008, risiti najua iko wapi? Msituchonganishe, mnavunja mahusiano baina ya TRA na watu wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za sikukuu, wanusanusa kwenye maduka ya watu wanataka nini? Saa 4.00 asubuhi anakwambia naomba ripoti, ripoti inatolewa pale mtu anapofunga mahesabu ya siku, hiyo ya saa 4.00 yeye anatoa wapi ripoti? Kwa hiyo, saa 4.00 anatoa ripoti, saa 7.00 akifunga duka akienda kula akirudi anatoa ripoti. Kwa nini hamjatengeneza utaratibu wa kuelimisha wafanyabiashara? Hii ni dhambi kubwa sana, itamtafuna Mheshimiwa Dkt. Mpango. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii issue ya Polisi, tunataka watuambie Polisi wamegeuka kuwa wakusanya ushuru wa nchi hii? Polisi wamejazana barabarani, kila mtu ana mashine, wameongeza idadi ya magari, kila siku magari matano, utakamata magari ya nani? Wanasababisha nchi hii kuangamia kwa sababu ya maarifa. Serikali haijakokotoa vyanzo vya mapato ambayo tunafikiri kwamba tutapata mapato wamekuja tu wana-hang halafu sasa wameelekeza kwa wale wanaofikiri wataleta hela, Polisi hawataweza kuinua uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna issue ya standard gauge. Mradi huu hauwezi kutekelezeka. Kama tunataka kuingia kwenye ushindani wa soko, Kenya wanatengeneza standard gauge inayotumia mafuta sisi tunatengeneza inayotumia umeme kwa kutegemea umeme wa Stiegler’s Gorge. Tutatoka humu Bungeni mpaka huo mradi utimie, wote tumekufa. Tukifika kule, tutakuta na Kenya nao wameshatuwahi hakuna tena habari ya standard gauge. Nani anayekuja kwenye gharama kubwa wakati kuna standard gauge inayotumia mafuta yenye gharama nafuu? Hakuna standard gauge inayoweza kujengwa kwa ajili ya kubeba tu abiria. Kama huo ndiyo mpango wenu, tutakuwa tumefeli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengine siyo lazima tuyaseme kwa sababu macho yanaona lakini inabidi tuyaseme. Kwa nini Serikali isije na vipaumbele vinne tu ambavyo vinaweza kutekelezeka kuliko kuja na mlolongo wa vipaumbele ambavyo havitekelezeki? Leo nchi hii inahema kwa ajili ya sigara na pombe. Kila mwaka kodi ya pombe na sigara inapandishwa, japo wameandika ni hatari kwa afya zetu. Hakuna vyanzo vingine vya mapato? Wameacha kuweka wasimamizi katika zile sekta tunazofikiri zinatuletea pesa, wamekuja na hizi hela ndogo ndogo za kuokoteza, hizi ni pesa za kuokoteza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mheshimiwa Waziri akajipange, tunataka bajeti inayotekelezeka.