Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata fursa hii adhimu na mimi kuchangia. Pili, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri aliyofanya na tunakubali kibinadamu kwamba kuna yaliyopungua na ndiyo maana na sisi tumepata fursa hii ya kuzungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita katika Jiji la Dar es Salaam na bahati njema nawe ni wa Dar es Salaam. Dar es Salaam ni kitovu au chemchem ya mabadiliko kwa Tanzania. Dar es Salaam ilitoa ushiriki mkubwa kabisa katika kuleta mageuzi na uhuru wa nchi. Mheshimiwa Mwalimu Nyerere alianza Dar es Salaam na wazee wake wa Pwani pale kupigania uhuru. Kwa hiyo, Dar es Salaam tuna kila sababu ya kuhakikisha unakuwa mji wa kisasa na chemchem ya uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam ina mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi yetu. Takwimu zinaonesha makusanyo ya kodi ya nchi yetu nusu yanatoka Dar es Salaam. Kama tutapanga mipango yetu mizuri zaidi, kuna uwezekano mkubwa kabisa Dar es Salaam ikaongeza mapato. Kama tunavyofahamu Dar es Salaam ina zaidi ya ya watu milioni sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka nini sisi watu wa Dar es Salaam? Dar es Salaam tunataka Serikali ituwekee miundombinu ya kisasa ambayo itaweza kupunguza foleni. Uchumi wa Dar es Salaam unaweza ukaenda mara mbili zaidi endapo watu wa Tegeta, Mbondole na Pembamnazi wanaweza kufika Kariakoo kwa wakati na mtu wa Kongowe anaweza kufika Tegeta kwa wakati. Ili hili lifanyike, lazima Mheshimiwa Waziri aitazame Dar es Salaam kama Special Zone, kama sehemu ambayo uchumi wa nchi unaweza ukaimarika kupitia Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nazungumza hivi kama Mbunge wa Kinondoni, niko katikati pale, lakini watu wanaokwenda Tegeta wanategemea barabara za kwangu pale Magomeni, Ndugumbi, Makumbusho, Kijitonyama, Kinondoni yenyewe, Hananasifu, Kigogo lazima wapite. Tunapokuwa na miundombinu mibovu katika maeneo hayo ya kati, wewe shahidi, tunapokuwa na miundombinu mibovu Ilala mtu hawezi kufika pembezoni. Kama tunataka maendeleo ya kweli, basi lazima tujikite kuhakikisha tunaleta mabadiliko Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wangu wa Dar es Salaam siwezi kuwaombea pembejeo hapa kwa sababu kazi yao kubwa wamejikita katika sehemu ya kujiajiri wenyewe. Tunapozungumzia uchumi wa Dar es Salaam, tunazungumzia biashara. Lazima Mheshimiwa Waziri ahakikishe anatuwekea mazingira bora ya biashara. Zamani Jiji la Dar es Salaam tulikuwa tunapokea wageni kutoka Burundi, Rwanda, Congo wanakuja kununua bidhaa zao pale sasa hivi wale watu hawapatikani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napozungumza hivi naamini Mheshimiwa Waziri hili analitambua. Sasa tusiweke mazingira magumu mpaka ikapelekea wageni hawa wakaona ni bora kulichukua kontena kulipeleka kwao kuliko kuja pale Dar es Salaam. Kwa sababu wakija Dar es Salaam watu wa Ilala, Kinondoni na Temeke guest zao zitapata watu, uchumi unazunguka. Kwa hiyo, hili ni muhimu ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine watu wetu wa Dar es Salaam wamejiingiza katika sekta ya habari, utamaduni, sanaa na michezo. Tunapozungumzia Wizara ya Michezo kwetu sisi inafanana na Wizara ya Kilimo kwa sababu asilimia 60 ya watu wa Dar es Salaam shughuli zao ni za kujiajiri wenyewe, sanaa, habari na michezo. Vijana wamefungua ma-blog mengi, wako kwenye social media, wanaigiza, wanaimba na wanacheza. Ukienda katika Wizara ya Michezo katika fungu la maendeleo, utakuta kuna shilingi bilioni 8, shilingi bilioni 3 kwa ajili ya TBC, shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya viwanja, sasa unakuta hawa vijana hatujawatengea kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati wenzetu wengine wanadai pembejeo kwa watu wao, sisi watu wa Dar es Salaam tunataka vijana wetu watengenezewe studio waingie watoe muziki safi. Tunataka vijana wetu watengenezewe jumba kwa ajili ya kwenda ku-act na wapate hatimiliki ya kazi zao. Hizi ndiyo kazi ambazo nadhani watu wa Dar es Salaam tukifanyiwa uchumi wetu utakwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu mafanikio ya bajeti yetu. Kuna watu wanazungumza hii ni bajeti hewa, bajeti ya kufikirika na kadhalika, lakini jamani tuwe wa kweli, bajeti hii ni nzuri na lazima tujue tulikotoka. Sisi wengine tunakumbuka tuliingia kwenye siasa kwa matatizo gani? Tuliingia kwenye siasa wakati huo barabara ya Kibiti – Lindi haipitiki, hakuna Daraja la Mkapa. Tuliingia kwenye siasa mtu akitaka kutoka Dodoma kwenda Arusha lazima afike Chalinze. Mtu akitaka kutoka Dodoma kwenda Mbeya lazima afike Morogoro. Kulikuwa hakuna Daraja la Kikwete wala Daraja la Ifakara. Tumetoka mbali sana jamani, lazima tuone tulikotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeondoa riba kwa vijana. Mimi nikienda Misikitini kuwahamasisha watu wangu namna gani wataitumia Serikali, nikiwaambia mikopo, walikuwa wananiuliza sasa hii riba itakuwaje na sisi hatutaki kutumia riba? Leo Serikali imesikia imeondoa riba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye miradi mikubwa, sisi watu wa Dar es Salaam ndiyo watumiaji wakubwa wa umeme. Hizi propaganda ya kuacha huu mradi wa Stiegler’s Gorge zinatoka wapi? Watu wa Dar es Salaam tunatumia umeme zaidi ya nusu ya umeme wote unaozalishwa. Tunajua kuzalisha megawatt moja ya umeme wa gesi ni ghali kuliko umeme wa maji, dola milioni 1.2 na hii nyingine ni dola milioni 1. Hata uzalishaji wake, megawatt moja inauzwa kwa Sh.136 wakati ya maji ni Sh.36. TANESCO leo wananunua umeme kwa unit moja Sh.148 wanauza kwa Sh.200, tukitengeneza umeme wa maji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei itashuka na watu wa Dar es Salaam watanufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.