Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nijadili hoja yetu hii ya Wizara ya Fedha kuhusu bajeti kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kabisa kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na wataalam wao kwa kweli kwa bajeti nzuri sana mwaka huu. Kwa mara ya kwanza wale waliokuwa wanategemea kwamba bei za bia na soda ndiyo zitakuwa uti wa mgongo wa bajeti nadhani wameona kwamba kuna watu wanafikiri na kufanya kazi nzuri ya kutengeneza bajeti ya maendeleo ya nchi hii na mimi nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo makubwa ambayo wamefanya ni kuanza sasa kuelekea kwenye harakati za kuvutia sana wawekezaji. Hatua ya kupunguza Kodi ya Mashirika au Corporate Tax, utaratibu mpya uliowekwa wa kumpa Waziri mamlaka ya kuweza kusamehe kodi na hasa pale ambapo tulikuwa tunatoza kodi kwenye misaada ambayo tunapewa na nchi za nje, hizi ni hatua nzuri sana. Hatua hizi nzuri zimefanywa pamoja na kuandaa Investment Blue Print mpya kwa nchi yetu na tunategemea kabisa kwamba hatua hizi kwa pamoja zitaongeza uwekezaji wa wawekezaji wanaotoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitoe mapendekezo ambayo yanajenga hatua ambazo zimechukuliwa. Jambo la kwanza, Serikali ingefikiria kupunguza VAT kutoka 18% angalau ifikie 15%. Jambo la pili, Serikali ingefikiria kuwatambua wawekezaji wa ndani kama ambavyo inawafikiria wawekezaji wa nje. Kwa sababu kwa vyovyote vile, hata kama tutavutia wawekezaji wengi sana kutoka nje lakini watakaojenga uchumi wa Tanzania na watakaokuwa wengi katika uwekezaji ni wawekezaji wa ndani, wawekezaji wadogo, wa kati na wakubwa katika nchi yetu. Hawa ndiyo watakuwa uti wa mgongo katika uchumi wetu, hili ni jambo muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya hivyo, ni muhimu Serikali ifikirie kupunguza riba ya mikopo kutoka kwenye mabenki yetu. Riba ya mikopo katika benki zetu inakatisha tamaa sana uwekezaji. Wawekezaji wa nje wanachukua mikopo kwenye benki zao kwa riba ya asilimia
1.5 mpaka asilimia 2, wawekezaji wa kwetu wanachukua mikopo kwa asilimia 21, ikiwa rahisi sana ni asilimia 15, hawawezi kushindana kwa vyovyote vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba kwa miaka 10 tumekuwa tunasukuma sana jambo hili na ni kama limeshindikana. Majirani zetu Wakenya walikuwa na hali kama hii, Bunge lao likachoka kusukuma Central Bank kupunguza riba na wakatunga sheria kwamba benki zisizidishe interest level fulani wanapotoa mikopo kwa ajili ya uwekezaji. Nasi hatuna haja sasa ya kujikusanya kama Bunge na kulazimisha benki yetu, lakini Serikali ifikirie kupunguza riba ili wawekezaji wa ndani waweze kukopa na kushindana na wale wa nje.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la lingine mwekezaji ni yuleyule. Wahenga wa Kipare wanasema kama unampenda jongoo lazima upende na miguu yake. Wawekezaji wa ndani kabla hawajaanza kufanya biashara wakapata faida ambayo ndiyo inatakiwa itozwe kodi wanakadiriwa kodi kwa maana wanatakiwa walipe kodi kwenye mkopo waliouchukua kuandaa uwekezaji, sasa haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutajengaje kada ya wawekezaji wa ndani kama tunaanza kuwakata kodi hata kabla hawajaanza kuzalisha? Napenda tuanze kufikiria wawekezaji wa ndani na wenyewe wapewe tax holiday, wawekezaji wa nje tunawapa five years tax holiday, tufikirie kuwapa tax holiday wawekezaji wa ndani, angalau hata miaka miwili. Mapendekezo yangu yangekuwa kwamba kama tunaweza kuwangojea wawekezaji wa nje miaka mitano tusishindwe kumngojea mtu mwenye duka mtaani miaka mitatu ndiyo aanze kulipa kodi wakati amejizatiti katika biashara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda sana niliseme ni juu ya mashirika yetu haya yanaitwa Regulatory Institutions. Hizi Regulatory Institutions zetu kama EWURA, SUMATRA, TBS na mashirika yote haya ambayo yanatoa huduma hiyo, yanaundwa kwa lengo la kutoa huduma lakini yakianza kazi yanaanza kazi kama mashirika ya kukusanya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alisema hapa juzi Mbunge wa Singida Mjini, Mheshimiwa Sima, kwamba mashirika haya yote yangekuwa managed chini ya paa moja (one roof) yalipwe mchango mmoja tu halafu yawe yanatoa huduma kwa wawekezaji. Yanasumbua sana wawekezaji na uwekezaji unakuwa mgumu kwa sababu hiyo. Hayo ndiyo yalikuwa muhimu kwangu niliyoyaona katika upande wa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, kwa ingenuity hiihii ambayo wametumia katika kuangalia kodi waangalie pia maeneo ambayo yanaweza kuleta mapato makubwa kwa Serikali kwa uwekezaji mdogo. Nitatoa mfano mmoja, hapa kwetu Tanzania tuna hekta ambazo ziko chini ya umwagiliaji 489,000. Uzalishaji katika haya mashamba ya umwagiliaji ya hekta 489,000 kwa uzalishaji wa mpunga ni kama tani moja mpaka tani moja na nusu kwa hekta moja. Kwa ujumla tunapata kama tani 700,000 kutokana na haya mashamba ambayo yameandaliwa kwa umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wakulima wangefundishwa kilimo bora cha kulima mpunga na wakalima mara mbili kwa mwaka, hekta moja ingeweza kutoa tani 10 mpaka 15 kama wanalima misimu miwili kwa sababu wananyeshea. Kwa uzalishaji huo tungeweza kuwalisha mchele watu wa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo, Zambia, Mozambique na Malawi, wote ambao wananunua mchele kutoka nchi za nje. Hesabu ambazo nimeā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, calculation ambayo nimefanya hapa juu ya bahasha kwa mwaka mmoja tungeweza kupata dola bilioni 3 mpaka bilioni 7 kutoka kwenye mpunga peke yake.