Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu na nitoe pongezi sana kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimwia Dkt. Mwigulu, Naibu Waziri na pia nimpongeze IGP Sirro na Makamanda wote bila kumsahau Kamanda wa Uhamiaji, dada yetu Kamanda Anna Makakala, mwanamke mwenzetu kwa kazi ambazo wamekuwa wakizifanya kulitumikia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu ambaye alikuwa Iringa kwa siku tano. Amefanya kazi nzuri sana na niseme kwamba wananchi wa Iringa kwa kweli wametambua uwepo wake na wametambua kazi nzuri ambazo amekuwa akizifanya kwa wananchi wetu. Nimpongeze sana RPC wa Mkoa wa Iringa, Kamanda Bwire kwa kuhakikisha kwamba usalama umekuwepo kwa kipindi chote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza naomba kumpongeza sana Mchungaji Msigwa, narudia tena, nampongeza sana Mchungaji Msigwa, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa kutambua kazi nzuri ambazo zinafanyika kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano na kumtambua kwamba Mheshimiwa Rais, Dkt. Pombe Magufuli anafanya kazi bila kubagua, bila ubaguzi na maneno haya mazuri ameyaongea mbele ya Waziri wetu, Mheshimiwa Jenista Mhagama, mbele ya Mheshimiwa Susan Mgonukulima na Wabunge na wananchi wa Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nasema sasa Mheshimiwa Msigwa ameanza kukomaa kisiasa. Nashindwa kushangaa, Wabunge wengine wa Upinzani wanapokutana na Rais waseme haya maneno, wamwambie ukweli, lakini wanapoingia humu ndani kwenye Bunge wanaanza kusema tofauti, sasa huo unakuwa unafiki. Hata jana eti wanasema kwamba Rais wetu hakosolewi, mbona mkikutana sasa hamumkosoi? Mnasubiri mpaka muingie humu Bungeni muanze kukosoa, muanze kutukana, mnataka kiki au mnataka nini? Jamani mimi nawaombeni, upinzani wa kweli ni kusema ukweli lakini upinzani wa kweli siyo kuanza kusema vitu ambavyo siyo vya ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nianze mchango wangu;, nizungumzie changamoto ambazo ziko katika Mkoa wa Iringa. Mkoa wa Iringa una changamoto kwa kweli, askari wetu wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana, lakini bado wanaishi kwenye makazi duni. Haya maneno tumeshayazungumza muda mrefu, askari bado nyumba zao siyo nzuri sana kuanzia Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto bado hawajaweza kujengewa nyumba nzuri kama ambavyo zilivyo za wanajeshi wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeiomba Serikali yetu kwa kazi nzuri ambazo zimekuwa zikifanywa na askari wetu, basi wajengewe makazi ambayo yanalingana na kazi zao kwa sababu tunapozungumzia makazi pia tunamzungumzia na yule mwanamke ya wale watoto ambao wanaishi kwenye zile nyumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Serikali hii ingalie umuhimu wa askari wetu kwa kuwajengea nyumba nzuri kwa sababu nyumba ambazo ziko pale Kihesa, mimi nakaa pale Kihesa, ni nyumba ambazo zimejengwa muda mrefu sana, zingeweza zikabomolewa, zikajenga maghorofa kama ambavyo zimejengwa kwenye sehemu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia OC zao za Mkoa wetu bado zinatakiwa ziletwe za kutosha. Stahiki zao zilipwe mara moja kwa sababu wamekuwa wakidai kwa muda mrefu. Upandishaji wa madaraja na vyeo jamani uende kwa muda, wapandishwe kwa muda kwa sababu askari wetu nao wanahitaji wapate stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, lakini nizungumzie Jeshi la Zimamoto, Jeshi la Zimamoto wenzangu wengi wameshalizungumzia nimpongeze Kamanda Andengenye, lakini askari wetu wa Iringa, Kamanda wetu James anafanya kazi kwenye mazingira magumu sana. Wana vituo vitano vya zimamoto lakini kuna gari moja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Iringa una uwanja wa ndege, Mkoa wa Iringa una misitu kule Mufindi, kule Kilolo ambapo mara kwa mara ajali za moto zinatokea lakini magari yao ni mabovu sana. Kuna mlima ule wa Kitonga kumekuwa kunatokea ajali mara kwa mara hakuna crane ya kusaidia kuondoa magari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile wamekuwa mara nyingi kwenye Mto Ruaha watoto wetu wa shule wanazama, tunapata ajali, wananchi wanazama, hawana hata vifaa vya uokozi vya maji. Kwa hiyo ningeomba kwa kweli hili Jeshi la Zimamoto hebu liangaliwe, lipewe pesa ya kutosha ili wananchi waweze kuishi bila ya kuwa na matatizo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishauri halmashauri zetu tunapotenga haya maeneo basi tuweke na maeneo kwa ajili ya kuonesha huduma hii ya zimamoto kwa sababu tumeona sasa hivi miji inakua, lakini inapotokea ajali haya magari yanashindwa kupita kwenda kuokoa. Hata hapa Dodoma ilitokea siku ile walibomoa nyumba. Kwa hiyo, niombe Halmashauri zetu pia zitenge maeneo kuhakikisha kwamba magari ya zimamoto yanakwenda kufanya kazi zao vizuri. Vilevile naona magari yale ya washawasha yanatumika kuzima moto. Sasa naomba Jeshi letu la Zimamoto wapewe magari ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze Kamanda wa Jeshi la Magereza na hasa wa Mkoa wetu wa Iringa, Kamanda Mwakajungu anafanya kazi nzuri sana. Nilishakwenda kutembelea Magereza, chakula kizuri sana lakini wafungwa hawana uniform kwa kweli, wanavaa kwa shida. Iringa ni mji ambao una baridi sana, wapewe masweta na mablanketi, kwa kuwa unakuta wafungwa wanaugua pneumonia. Kwa hiyo, wanatumia pesa nyingi kuwatibu badala ya kuzuia na wanapata matatizo makubwa sana kwa kuhudumia hayo matibabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niendelee kuzungumzia kwamba Wilaya ya Kilolo ni Wilaya ya muda mrefu sana bado haijaweza kujengewa Ofisi ya Wilaya. OCD anakaa mbali na DC, kwanza hawana vifaa vya kutosha kwenye ile Wilaya, kwa sababu hawana mafuta, vilevile hawajawahi kujengewa nyumba za kuishi, siku zote wamekuwa wakiishi kwenye maeneo ye makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, askari amepanga kwa mwananchi, je, yule mwananchi akifanya kosa na yeye amepanga kwake kweli atam-report? Kwa hiyo, niombe kwa kweli Jeshi la Polisi liangalie, askari wote waishi kambini kwa sababu wakati mwingine wanakuwa hawana usafiri. Kwa mfano, Kilolo, Makao Makuu ya Polisi ambayo wamepewa yako mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee kuzungumza kuhusiana na maandamano. Kwa kweli nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuondoa haya maandamano, kwa sababu kwenye Mkoa wetu wa Iringa, maandamano haya yametuletea hasara kubwa sana, yalisababisha hata gari la zimamoto lilipigwa vibaya sana, lilivunjwa vunjwa kwa ajili ya maandamano. Vilevile barabara nyingi sana ziliweza kuchomwa wakati huo na kusababisha hasara sana kwenye Mkoa wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gumu sana ambalo akinamama wote kwa kweli tumelipongeza kuhusu maandamano, watoto wengi sana walivunjwa miguu, waliumia sana na hawakuweza kupatiwa msaada wowote. Kwa hiyo, nasema kwamba wananchi waandamane kwa kufanya kazi, wasiandamane kwa kuharibu vitu na niwaombe hata wanasiasa wenzangu tufanye hawa watu waandamane kwa kufanya kazi, nafikiri itakuwa busara zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee kuhusiana na mtandao wa wanawake, maana yake sisi ni wanawake, nilikuwa mgeni rasmi kwenye shughuli ya sikukuu ya mtandao wa wanawake. Kwa kweli walionesha wanafanya kazi nzuri sana. Kila idara wapo lakini cha kushangaza IGP yuko hapa, ukitembea kule kote hawapati vile vitochi, vitochi hivi vinapewa kwa masharti, naona wanashika tu wanaume. Walikuwa wanasema kwamba hata wanawake wanaweza wakashika vile vitochi wakafanya kazi vizuri tu. Sijajua kwamba wanapewa kwa masharti vitochi ama walipewa kwa waganga wa kienyeji. Kwa hiyo, niombe hata wanawake pia wapewe vitochi siyo kwamba wanaume tu siku zote.