Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Asha Mshimba Jecha

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kuchangia katika Wizara hii. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia leo kusimama hapa tukiwa katika hali ya uzima na afya. Pia nimshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wanafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni Wizara ambayo ina maisha ya wananchi moja kwa moja kwa sababu inalinda raia lakini inalinda na mali zao. Kwa hivyo hapo utaona ugumu wa kazi hii wewe unayelindwa una mali, anayekulinda hana mali. Kwa hiyo, hii Wizara kwa kweli ina kazi ngumu . (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais. Katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri tumeona kuna mambo mazuri ambayo yameelekezwa kwa Jeshi letu la Polisi. Tunaomba mambo hayo yafanyike kwa utaratibu kama yalivyopangwa. Mheshimiwa Waziri nimshukuru mwaka jana katika mchango wangu nilizungumzia Kituo cha Polisi Dunga na nimepata habari kwamba tayari ujenzi umeanza. Kwa hiyo namshukuru na nampongeza Mheshimiwa Waziri na naomba fedha zipelekwe kwa wakati ili ujenzi uweze kuendelea vizuri na kile kituo kimalizike kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Mkoa wangu wa Kusini Unguja tuna upungufu mkubwa wa magari kwa ajili ya kufuatilia shughuli mbalimbali za maaskari. Mkoa wetu una vituo vingi lakini kuna ukanda mkubwa wa utalii, hatuna magari, baadhi yamekuwa yakitumika magari yetu kuwasaidia askari ni wajibu wetu. Kwa hiyo, tunaomba katika haya magari ambayo nimeyaona katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri, basi na Mkoa wetu wa Kusini wasisahau kutuletea magari hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vie nimeona kuna ujenzi wa nyumba za maaskari, Mkoa wa Kusini na kuna baadhi ya vituo vinahitaji kusaidiwa nyumba za askari, kwa hivyo nayo wasitusahau pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nizungumzie, nataka nisifu Wizara hii, kazi ya kulinda raia na mali zao ni kazi kubwa. Kwa hivyo, bado namwomba Mheshimiwa Waziri, elimu ya kutii sheria bila shuruti iendelee kutolewa kwa wananchi wetu, kwa sababu maelezo yanayoelezwa humu ndani inaonesha wazi kwamba bado wananchi wanataka kupata elimu ya kutii sheria bila shuruti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi na raia ni ndugu, ni kama watoto pacha sisi tunawategemea lakini kwa kweli kumekuwa na manung’uniko mengi ambayo mengine hayana ukweli, mengine yanaweza yakawa yana ukweli fulani, kwa hiyo, ipo haja ya elimu kutolewa kwa raia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nilipongeze Jeshi la Polisi, Zanzibar kulikuwa na wakati mgumu sana, lakini tunashukuru Jeshi la Polisi waliweza kuzuia ugumu ule na sasa tunaishi kwa amani na utulivu. Wizara wanafanya kazi nzuri lakini kwa kuwa kuna wahalifu wengine hawataki kuona uzuri huu, tunaomba kila mtu achukue nafasi yake sisi raia tuna nafasi ya kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo na sisi tushirikiane nao na wao wanayo nafasi ya kushirikiana na sisi na wao washirikiane na sisi vizuri. Jeshi hili lisiwe na uadui kwa raia na sisi raia tusiwe na uadui kwa Jeshi la Polisi kwa sababu tukilikosa kwa kweli hatuwezi kuishi hata kidogo, tunauona umuhimu wa Jeshi la Polisi pale yanapotokea matatizo, lakini tumekuwa tunawalaumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kitabu cha Mheshimiwa Waziri, pia wako askari walikufa katika kutekeleza majukumu yao na wengine waliuawa kama walivyouawa raia wengine, halifurahishi kwa sababu uhai wa mwanadamu hauna thamani ya kitu chochote. Hata hivyo, haya mambo yaende sambasamba, sisi raia tuweze kutii bila shuruti, nao askari baadhi yao kwa sababu na wao ni binadamu kama sisi na wao bila shaka wengine wana upungufu, yule mtu mmoja asiharibu Jeshi zima la Polisi ambalo linafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, waendelee na kazi nzuri, yale madogo madogo ambayo yanalalamikiwa tuyafanyie uchunguzi na tuyachukulie hatua. Kuna askari wanafanya kazi nzuri na wamekuwa wakidai posho zao muda mrefu. Mheshimiwa Waziri amefanya ziara Zanzibar na Mheshimiwa Naibu wake amefanya ziara, lakini hata Wakuu wa vikosi nao wamefanya ziara na wamekuwa wakiwaahidi, kwa hiyo tuwatimizie yale matakwa yao ambayo bado hawajafanikiwa .

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kidogo inaleta huzuni kwa sababu ninapoona mwenzangu tumeingia kazini wote mwaka 2013/2014, wao wamepata zile posho, wengine hawajapata, kwa kweli haileti picha nzuri na wako hawa wanaopata posho ya kazi maalum. Kuna wengine wamepata, lakini wengine hawajapata na wote wameanza kazi pamoja, wameingia kazini pamoja, wamefuatilia, wamekwenda mpaka Makao Makuu, lakini majibu hakuna. Kwa hivyo tuwatazame hawa watu, yale manung’uniko madogo madogo tuweze kuyaondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna baadhi ya askari wa FFU Machui, walishiriki katika ile Operesheni Tokomeza na wao pia wanasema hawakupata posho zao mpaka sasa hivi. Mambo mazuri mengi wanayafanya, lakini haya madogo madogo najua yako ndani ya uwezo wao, kwa hivyo tujitahidi na wao tuwakamilishie ili mambo yaweze kwenda vizuri, lakini kiujumla Jeshi la Polisi wanafanya kazi nzuri. Kazi mnayoifanya tunaiona, tusingeweza kuishi kwa amani na utulivu kama hawapo, kuwepo kwao kuna umuhimu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, yale niliyozungumza kuhusu vituo vya polisi wayatekeleze. Naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.