Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukurani zangu za dhati kwako kwa kunipa fursa hii kutoa michango yangu katika Wizara hii kubwa katika nchi yetu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, namshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuonesha uwezo mkubwa wa kuongoza nchi hii na Insha Allah Mwenyezi Mungu ampe kila la kheri katika kufanikisha suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, namshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Watendaji wake wote kwa umahiri wao mzuri wa kuwasilisha hotuba hii ambayo imebeba mambo mengi katika nchi yetu hii. Nchi yetu hii ni kubwa lakini hotuba yao hii ni fupi sana lakini ime-cover kila kitu katika nchi yetu hii. Kwa hiyo, nawapongeza watu hawa kwa umahiri wao huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango yangu itakwenda kwenye kukumbusha masuala ambayo nimekuwa nikiyazungumza mara nyingi kwenye vipindi vyetu vya maswali na majibu. Suala la kwanza ni kuhusu kituo changu cha Mkokotoni, kituo hiki ni miongoni mwa vituo vikongwe sana katika nchi yetu hii. Ni kituo chakavu kabisa, kinahitaji matengenezo ya kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara ilianzisha jengo pale katika kituo hiki, lakini mpaka sasa hivi jengo lile limekwama, hatujui nini kinaendelea. Jengo limebakia kama gofu, hatujui hatima ya jengo lile. Kwa hiyo, nachukua fursa hii kuiomba Wizara ikamilishe jengo lile ili askari wetu pale wapate makazi mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, askari wetu pale wana hali ngumu sana, katika mvua hizi ambazo zimenyesha juzi, askari wetu imebidi wahamie chumba cha mahabusu kufanya kazi, imagine chumba cha mahabusu askari wetu wamehama kwenye Ofisi yao wanatumia chumba cha mahabusu kufanya kazi katika kituo kile. Kwa hiyo, naiomba Wizara ikamilishe masuala yale ili askari wetu wale waweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimekuwa nikizungumza kila siku ni kituo cha Polisi katika Kisiwa cha Tumbatu. Suala hili nimekuwa nikizungumza kila siku kuiomba Wizara kwamba itujengee kituo katika Kisiwa cha Tumbatu. Jiografia ya Kisiwa cha Tumbatu inahitaji huduma zote pamoja na huduma za usalama. Masafa kutoka Mkokotoni mpaka Tumbatu ni almost kilomita mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, linapotokea neno Kisiwa cha Tumbatu inabidi askari watoke Mkokotoni waende Tumbatu, wavuke kwa kutumia bahari. Imagine kama kuna kitu kimetokezea kule hatuombi kitokezee, lakini mpaka wakifika pale Tumbatu basi lililotokezea limeshaathiri sana. Kwa hiyo, naomba suala hili kwa mara nyingine kwamba Wizara itujengee kituo katika Kisiwa cha Tumbatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni vitendea kazi katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Waheshimiwa wengi hapa wamesimama wanazungumzia vitendea kazi wamekuwa wanaomba magari na vifaa vingine, lakini Wizara hii ina tatizo moja kubwa sana la vitendea kazi hasa kwenye stationeries. Mwaka jana nilipata bahati mbaya, niliibiwa simu yangu nyumbani kwangu nika-report polisi Dodoma hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipofika pale kituo cha polisi Dodoma nilitakiwa nichukuliwe maelezo, basi askari pale hata stationery hawana, stationery ya kuandika ile report yangu hawana mwisho niliona kwamba kwa kweli ni kitu cha aibu, askari pale wanatumia order paper hizi zetu za Bunge, ndiyo wanaandikia report zetu. Kwa hiyo, Wizara iwasaidie siyo Dodoma tu lakini nchi nzima kwamba kuna tatizo la stationeries katika vituo vyetu hivi vya Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo leo nataka nichangie ni kwamba utaratibu wa viongozi wetu wa Wizara hii kutembelea katika mikoa. Mheshimiwa Waziri mara baada ya kuchaguliwa alikuwa na utaratibu mzuri wa kutembelea katika mikoa yetu na wilaya zetu. Namwomba Waziri utaratibu wake ule uwe utaratibu wa kudumu aendelee nao katika Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, naunga mkono hoja.