Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Upendo Furaha Peneza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii nami kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 3(1) inasema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayofuata mfumo wa vyama vingi. Maana yake ni kwamba vyama vyote ambavyo viko Tanzania vyote vinasajiliwa kulingana na Katiba na sheria ambazo ziko ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo tungetegemea kwamba sheria ambazo zinaruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara iweze kuheshimiwa ili wananchi wakapate fursa ya kusikiliza vyama hivi vya siasa lakini pia vile vile kutimiza wajibu ambao upo kutokana na Sheria ya Vyama vya Siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha kusikitisha ni kwamba Jeshi letu la Polisi na mtakubaliana na mimi kwamba Vyama vya Upinzani havina uadui wowote na Jeshi la Polisi na ndiyo maana pamoja na kwamba katika bajeti hii upinzani hatujawa na hotuba mbadala kwa sababu ya changamoto zilizopo, lakini kwa miaka mingi ambayo imekuwa ikipita upande wa upinzani umekuwa ukitoa maoni namna gani ya kuboresha maisha ya askari wetu. Tumekuwa tukifanya hivyo kwa sababu tunatambua kazi kubwa waliyonayo ndani ya jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo maoni kutoheshimiwa, leo Jeshi la Polisi limekuwa ni sehemu ya kukandamiza demokrasia ndani ya nchi hii. Jeshi la Polisi limekuwa pale mtu anaposimama na kuikemea Serikali, mtu anaposimama na kuonesha kwamba hapa Serikali imekosea, mtu huyo anabadilika na kuwa adui, ataitwa mchochezi, ataitwa majina ya kila namna ili mradi tu kuhakikisha kwamba uongozi au Awamu hii haisemwi, haikoselewi badala yake ni kusifiwa tu kwa mema tu wanayoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna hiyo hatutaweza kwenda na kama Jeshi la Polisi sasa hivi kwa kazi ambayo inaifanya, mfano, kama dada mmoja ametangaza maandamano ya tarehe 26, viongozi wangu wa Geita, Katibu wangu, wamekamatwa kana kwamba ni sehemu ya Mange Kimambi. Uwoga ambao unatengenezwa ni kana kwamba wananchi wa Kitanzania hawaruhusiwi kusema na kuikosoa Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa tutakubali kwenda kwa kile tu ambacho kinasemwa na Rais, kwenda kwa kile tu ambacho Serikali inasema, basi hatutafika na tunaendelea kurudi nyuma. Jeshi letu la Polisi leo kwa kazi yote ambayo wameifanya na nitasema tu kwamba kipindi cha nyuma tukiwa na IGP Said Mwema alianzisha mpango wa kutengeneza jamii iwe na urafiki na polisi wetu. Mpango ambao sasa hivi unaendelea kurudi nyuma hatua nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakandamiza demokrasia Polisi wale wa ngazi za chini wanajengeka ubabe wa hatari. Raia wamekufa mikononi mwa polisi, kijana wa Mbeya ameuawa mikononi mwa polisi, ndugu yake Heche ambaye amezikwa jana ameuawa mikononi mwa polisi kwa kuchomwa kisu. Hatuwezi kuwa na Taifa ambalo watu ambao tunategemea watulinde na mali zetu ndiyo wanaotuangamiza na kutufanya tufe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanaanza kwa sababu ya ubabe ambao umeanza wa kushughulikia viongozi, watu ambao wanatoa mawazo mbadala, sasa yanaenda mpaka kwa raia ambao kwa namna moja ama nyingine inawezekana wana ukosefu katika maeneo yao, ubabe wa hatari unafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haina sababu ya Jeshi la Polisi kujitengenezea uadui kwa sababu hawana nyumba za kutosha, wanaishi na sisi kwenye jamii, ni ndugu zetu, ni waume zetu, ni shemeji zetu. Tungependa tuishi nao kwa amani, hakuna haja ya kuua watoto wetu akina Akwilina halafu leo jalada hilo linafungwa kana kwamba polisi wameshindwa kufanya uchunguzi hata baina yao wao wenyewe kumtambua ni nani halisi aliyepiga risasi na kumuua Akwilina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishia kumfariji mama kwa sababu anatoka familia ya kimaskini na hakuna la maana lolote linalofanyika. Kesho, keshokutwa, Watanzania ambao wameumizwa na Jeshi la Polisi kutochukua hatua yao, watatumia nguvu kuwashughulikia watu, watawaua polisi jambo ambalo halitakuwa jema. Sasa ni vyema tukachukua hatua hiyo mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi hiyo ambayo si halali ya kukandamiza demokrasia nchi hii ambayo polisi wamekuwa wakiifanya, kule Geita kuna mauaji ya akinamama ambayo yanafanyika. Sasa hivi mama akienda shambani kule Nyangh’wale anatekwa, anavunjwa shingo, wanauawa. Wanatafutwa akinamama wajawazito na akinamama tu wengine katika maeneo ya shamba, suala ambalo limejenga hofu kubwa sana. Sasa ningeomba hii nguvu kubwa ambayo inatumika kudhibiti maandamano ya magari yote hayo tunayaona barabarani, polisi na vifaa vyao hebu vitumike basi viende Nyangh’wale, hawa akinamama wafanye shughuli zao kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili nitamuomba kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba anijibu kama mtu anayetegemea kuwa Rais ndani ya nchi hii siku moja.

Alitutangazia kwamba alikuwa na nia na alishiriki kwenye kura za maoni ndani ya chama chake, kwa hiyo, sidhani kama hiyo nia imekufa mapema hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi kwamba Wabunge wa Viti Maalum wapo humu Bungeni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibara 66 na Ibara ya 78 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazungumza uwepo wa Wabunge wa Viti Maalum ambao majina yao yanapendekezwa na vyama vyao na baadaye wanapatikana na kuunda ile asilimia isiyopungua 30 ya watu ambao wako ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pamoja na Wabunge wengine wa Viti Maalum ambao tuko huku ndani tumekuwa tukizuiwa kufanya mikutano yetu ya hadhara. Namwomba Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Wabunge wa Viti Maalum tunaambiwa tufanye kazi, sisi sio Wabunge wa vyumbani, tufanye kazi chumbani tuongee na akinamama na hili linaleta mtazamo mbaya hata katika jamii, ndiyo maana Wabunge wa Viti Maalum wengi wamekuwa wakidhalilishwa kwa sababu watu hawajui kazi wanazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaache wanawake wafanye kazi, wafanye mikutano, wawawakilishe wananchi ili wananchi waone kama kweli hawa ni Wabunge ambao wapo kwa ajili ya kuwawakilisha. Badala yake tunaonekana kama tuko tu kumaliza mishahara ya Serikali, “unalipwa milionio 12, unalipwa milioni 12” sasa sawa! Kazi yangu haithamiwi, siruhusiwi kufanya kazi, sasa kwa nini nakuwa Mbunge? Kwa sababu kama unalipwa ujira basi ufanye kazi inayopaswa kufanyika na tunahitaji kuwakilisha wananchi wote. Watu wafanye mikutano katika maeneo yao. Kwa hiyo, naomba sasa sheria za nchi yetu ziheshimike, watu wawasikilize wananchi, huwezi ukaja humu ndani ukamwakilisha mwananchi ambaye hujamsikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wa Viti Maalum wafanye mikutano katika maeneo yao, kama ni katika mikoa na kuweza kuwawakilisha wananchi. Badala yake tutasema kwamba Serikali ya Awamu hii ya Tano ipo kukandamiza wanawake, Serikali ya Awamu hii ya Tano ipo kuzuia maendeleo ya wanawake, badala yake tutasema kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano inataka kutengeneza mazingira magumu ya wanawake kuwa Wabunge kwa sababu katika siasa tunasema it’s all about visibility, nani kakuona hata katika Viti Maalum, badala yake sasa kama tunawafunga watu, ngono zitatumika, rushwa ya hela itatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutawatisha jamii kutafuta nafasi za kugombea. Tuwaache wanawake waonekane na hata kuzuia mikutano ya hadhara, inaathiri hata vijana wengine wasionekane kwa sababu kwa vijana kama mimi tumekuja humu ndani ya Bunge kwa sababu ya kazi ambazo tumefanya, tumefanya mikutano, jamii imetuona ikatuamini. Kwa hiyo, si tu kwa hivi wanavyovunja sheria za nchi, lakini pia wanaathiri ndoto za akinamama, wanaathiri ndoto za vijana ambao wangependa siku moja kuwa viongozi ndani ya nchi, kuwa viongozi wema ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nategemea kwamba, katika majibu ambayo kaka yangu atanipatia asinijibu kwa kutoa sababu kama zile alizojibu kipindi kile Katiba na Sheria. Tuweke mstari wa mbele kama tunataka kuendelea na kama unategemea au siku moja unataka kuwa kiongozi wetu, basi show the art kwa majibu unayo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)