Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Janeth Maurice Massaburi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kuwapongeza Watendaji na Viongozi wote wa Wizara hii wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na vikosi vyote vilivyoko katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vijana wetu waendesha bodaboda hasa walioko Mkoa wa Dar es Salaam, kwa asilimia 90 hawana usikivu na utu wa kutosha kwa Jeshi la Polisi, kupitia Idara ya Usalama Barabarani kwa kutozingatia usalama wa raia wakati wawapo barabarani. Vijana wengi wa bodaboda huendesha wakati wakiwa wamekunywa pombe au kuvuta bangi. Hali hiyo husababisha ajali nyingi za bodaboda na hivyo kuua na kujeruhi wananchi wengi wasiokuwa na hatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Jeshi la Polisi kupitia Idara ya Usalama barabarani liangalie upya jinsi ya kuzuia ajali zilizokithiri katika Mkoa wa Dar es Salaam zinazofanywa na vijana waendesha bodaboda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwapongeza Makamanda wa Usalama Barabarani katika Mkoa wa Dodoma kutokana na waendesha bodaboda kutii kwa kufuata Sheria za Usalama Barabarani. Vijana wa Dodoma tumewaona wakisimama kwa kuwapisha wananchi kuvuka kwa dakika mbili mpaka tatu. Kwa kitendo hicho sisi tunaotoka Mkoa wa Dar es Salaam imetushangaza kuona vyombo vya moto (pikipiki) kusimama kwa adabu na kuheshimu watu wasipatwe na ajali na kuacha ulemavu na hata vifo kwa raia wetu wasiokuwa na hatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ifanye utaratibu wa kuwapatia fedha Idara ya Upelelezi kwa ajili ya mafunzo mbalimbali ikiwemo kuepuka kulaumiwa kwa baadhi ya Maafisa Upelelezi ambao wanalichafua Jeshi letu kwa kupokea rushwa kutoka kwa walalamikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tabia ya baadhi ya Wapelelezi kutotenda haki kwa walalamikaji wakati wanapokwenda kushtaki katika Vituo vya Polisi. Wapelelezi hao hubadili kibao kwa walalamikaji na kutoa upendeleo kwa watuhumiwa. Hali hiyo inaashiria kuna mkono wa rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Jeshi litafute jinsi ya kukomesha tabia hiyo kwa baadhi ya Maofisa hao Wapelelezi. Pia Maofisa hao wapatiwe usafiri na fedha za mafuta na makazi bora ili waweze kutimiza wajibu wao wa kazi kwa ufanisi na tija. Kwa kuwapatia nyenzo au vitendea kazi kutaweza kuepusha vishawishi kwa wahalifu/watuhumiwa kwa kuwashawishi Maofisa hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Kituo cha Polisi Segerea (jirani na Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Segerea) kijengwe au kimaliziwe na kupatiwa samani, gari na Askari wa kutosha ili waweze kuimarisha ulinzi katika eneo hilo la Segerea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, narudia kuwapongeza wote waliohusika na utekelezaji katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.