Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mafia kijiografia ni kusini na inahudumiwa na kituo kimoja cha Polisi cha Wilaya. Mapema mwezi wa Nne mwaka huu, gari pekee linalohudumia kituo hicho aina ya Land Cruiser (Pick Up) lilipata ajali ya kutumbukia baharini kwenye Bandari ya Kilindoni, Mafia. Kwa kuwa kina cha maji kilikuwa ni kikubwa, gari lile limeharibika sana kiasi cha kutoweza kutengenezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia hali hii, Wilaya ya Mafia haina gari la Polisi; na kutokana na jiografia yake, hatuwezi hata kuazima gari kutoka Wilaya jirani. Mbaya zaidi, wahalifu wamechukua fursa ya kufanya uhalifu. Namwomba Mheshimiwa Waziri atupatie gari lingine, kwani hali inazidi kuwa mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri atupatie Kituo kidogo cha Polisi katika Tarafa ya Kivungwe, Kata ya Kivungwe. Hii inatokana na ukweli kwamba umbali kutoka kwenye Kituo cha Polisi cha Wilaya ni mkubwa, wananchi wanalazimika kusafiri masafa marefu kufuata huduma hii ya Kipolisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mashehe wa Uamsho linaingia mwaka wa tano sasa bila ya kujulikana hatma yao. Mashehe hawa wamekaa rumande kwa muda mrefu na mmoja wa wake wa Mashehe hao amejiua kutokana na kushindwa hali ya maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, wapiga kura wangu watatu kutoka Wilaya ya Mafia wanashikiliwa rumande mwaka wa pili huu sasa kwa tuhuma za ugaidi. Tunaomba haki itendeke kwa mujibu wa sheria za nchi. Kama hawana hatia, basi waachiwe huru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.