Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kufika mahali hapa nami kushiriki katika kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu. Naipongeza Wizara kwa hotuba nzuri yenye mlengo chanya, hotuba hii inakwenda kutekeleza yale yote yaliyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ili kuleta mapinduzi makubwa ya kiutendaji katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali ilizochukua katika kuliboresha Jeshi letu la Polisi ili lifanye kazi zake kwa uwezo wa hali ya juu kwa kuwapatia vifaa vya kisasa vya mawasiliano na vya kiuchunguzi ili liweze kupambana na ujambazi na matukio mengine ya kihalifu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, napongeza kwa kujenga Kituo cha kisasa cha Mawasiliano (Call Centre) Dar es Salaam ili kuwezesha wananchi kutoa taarifa za matukio mbalimbali kwa urahisi. Haya yote ni maboresho ya hali ya juu kwa Jeshi letu la Polisi ili kuliwezesha kufanya kazi zake pasipo shaka yoyote na kwa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali ilizochukua kuboresha idara nzima ya uhamiaji kwa kuzinduliwa kwa Mradi wa Uhamiaji Mtandaoni (e-Immigration), vilevile kwa kuzinduliwa pasi mpya ya kusafiria ya kielektroniki ya Kimataifa ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana nzima ya kuzinduliwa kwa pasi hii ni kupunguza vikwazo vya kusafiri mipakani baina ya raia wa nchi wanachama, pia kuimarisha mahusiano na shughuli za kiuchumi baina ya nchi wanachama. Pia naipongeza Serikali kwa kufungua ofisi zaidi za uhamiaji kwenye baadhi ya wilaya lakini naishauri izidi kufungua ofisi zaidi ili kuweza kuwasogezea wananchi huduma karibu na kudhibiti uhamiaji haramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kumekuwa na changamoto mbalimbali, mfano katika mazoezi muhimu ya kitaifa, kama zoezi la uandikishwaji wa Vitambulisho vya Taifa, Kadi ya Kupigia Kura, kumekuwa na matukio mbalimbali ya baadhi ya wahamiaji wasiokuwa waaminifu kujaribu kujipatia Kadi za Kupigia Kura na Vitambulisho vya Taifa, hali hii inatuonyesha kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii inatuonesha kwamba usimamizi wa masuala mazima ya uhamiaji bado kuna changamoto kubwa ya kudhibiti wahamiaji haramu na hii ni hatari kubwa kwa mustakabali wa Taifa letu. Kama hali hii ikiendelea basi nchi yetu inaweza siku kutokea tukatawaliwa na kiongozi ambaye si Mtanzania halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kujikita zaidi katika kudhibiti uhamiaji haramu na si kufanya kazi kwa mazoea, operesheni za mara kwa mara ziwe zinafanyika nchi nzima ili kuwabaini wahamiaji haramu. Tunapenda watu watakaoishi nchini kwetu kwa kufuata taratibu, sheria na miongozo na si watu wanaotaka kupita njia za panya na kujipatia uhalali wa kujiita Watanzania. Tujifunze kupitia nchi jirani, ama kwa nchi za wenzetu jinsi gani wanavyoweza kudhibiti wahamiaji haramu, Tanzania isiwe shimo la watu kuja na kujiamulia wanavyotaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza mazuri yote ya kuiboreshaji yanayoendelea kufanywa na Serikali yetu lakini sina budi kueleza changamoto zinazolikabili jimbo langu na ningependa Waziri atakapokuja kuhitimisha hapa anipe majibu ya changamoto ninazokwenda kuziainisha. Eneo la Kibaha Vijijini ni kubwa kijiografia, gari lililopo la polisi ni moja na ni chakavu haliwezi kabisa kufika maeneo yote ya vijijini na ukizingatia eneo ni kubwa na ukizingatia tena Kibaha Vijijini barabara zake ni mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naomba katika bajeti hii kupatiwa magari zaidi ya polisi ili yaweze kufanya doria na kuhakikisha hali ya kiusalama inazidi kuimarika. Naiomba Serikali kupitia Wizara inieleze hapa ni lini sasa Wizara itatupatia magari hayo ili jeshi letu liweze kufanya kazi zake bila vikwazo vyovyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hakuna makazi ya askari na kuwafanya askari wetu kuishi maeneo tofauti tofauti ambayo ni mbali na eneo lao la kazi. Kuna nyumba ya askari iliyojengwa lakini bado haijakwisha na imekwama kwenye hatua za umaliziaji, nyumba hii ikiisha itasaidia sana askari wetu kuweza kupata makazi bora. Naiomba Serikali kupitia Wizara inieleze ni lini nyumba hii itakamilika na ikizingatiwa imesalia sehemu ya umaliziaji tu. Naiomba Wizara inipe majibu pale Waziri atakapokuja kuhitimisha hotuba yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofanya uboreshaji wa majeshi yetu lazima tuzingatie na kuyapa kipaumbele pia maeneo yenye changamoto mbalimbali kama maeneo ya vijijini, lazima tuwapatie vitendea kazi vya kutosha kama magari, askari wa kutosha na nyumba za kuishi. Maeneo ya vijijini pakikosekana doria za kutosha na askari ni maeneo ambayo wahalifu huweza kujificha kwa urahisi na kupanga mipango hasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi naishauri Serikali kuyapa jicho la tatu maeneo hayo ili kuwawezesha askari wetu kufanya kazi kwa urahisi ili kuwawezesha kufika maeneo yote yanayowazunguka. Hata hivyo, napenda kuwapongeza askari wote pamoja na wa jimboni kwangu Kibaha Vijijini kwa kuendelea kufanya kazi ingawa kuna mazingira ambayo si rafiki, hii yote wanaonyesha uzalendo wa hali ya juu katika kulitumikia Taifa lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.