Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote kwa kuniwezesha kusimama na kutoa mchango wangu katika hoja hii muhimu ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Waziri na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Makamanda Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kuandaa hotuba nzuri na Waziri kuiwasilisha vizuri. Nampongeza Waziri na Watendaji wote kwa kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao unaimarika siku hadi siku, kudhibiti dawa za kulevya, kudhibiti uhamiaji haramu na kukabiliana na majanga ya moto nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na kuipongeza Serikali kwa kupeleka fedha kwa ajili ya shughuli za kawaida na shughuli za maendeleo na kufikia kiwango cha asilimia 78 bado tatizo la upelekaji wa fedha za kutosha katika sekta ya Mambo ya Ndani jambo ambalo linasababisha kushindwa kutekeleza kikamilifu wajibu wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuingalia Wizara hii nyeti ya Mambo ya Ndani kwa jicho la pekee na kuwapelekea fedha kama zinavyopitishwa na Bunge kwa sababu kutofanya hivyo wanashindwa kutengeneza magari, kununua vipuri vya magari, kununua mafuta ya magari na kununua vitendea kazi muhimu kama magari na hasa magari ya zimamoto. Mfano, Makao Makuu hapa Dodoma magari ya zimamoto yapo mawili ambapo moja lipo uwanja wa ndege na lingine ndilo linalotegemewa katika Mkoa mzima wa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya ujenzi wa nyumba za Askari na vituo vya Polisi; pamoja na kuipongeza Serikali kwa ujenzi wa makazi na vituo vya Polisi na pia kumpongeza Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, tarehe 7 Aprili, 2018 wakati akizindua nyumba za Askari Mkoani Arusha alitoa shilingi bilioni kumi kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya Askari ngazi ya chini, ambapo fedha hiyo itasaidia kujenga nyumba 400 katika mikoa yote nchini, tunamshukuru Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni Jeshi la Polisi na Magereza wafufue Kitengo cha Ujenzi ambacho kipo na kilikuwa kikifanya vizuri sana kwa sababu, kinao wataalam ambao kwa sasa wamepangiwa kazi katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo kutasaidia kujenga nyumba nyingi za Askari Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto, tena kwa wakati na kwa haraka na kuokoa fedha nyingi, kwa sababu Jeshi letu la Magereza litatoa nguvu kazi. Serikali ipeleke fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Askari Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nyumba za Askari zilizojengwa katika Mkoa wa Mara na Mwanza hazitumiki, ningependa kujua ni lini zitatumika? Pia, ningependa kujua kuna majengo na ofisi zimejengwa, lakini hazijakamilika, ningependa kujua mkakati wa kukamilisha majengo hayo na katika bajeti hii ni fedha ngapi zimetengwa kwa ajili ya kuyakamilisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maslahi ya Askari wetu, utaratibu wa upandishaji wa vyeo; pamoja na kupongeza majeshi yetu ya vyombo vya ulinzi na usalama na kuwa na utaratibu wa kanuni ya ajira na upandishaji wa madaraja, bado yapo malalamiko kwa baadhi ya Askari wetu na hasa waliokaa kwa muda mrefu ambao wamefanya kazi kwa uaminifu na uadilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa upandishaji wa vyeo haukuzingatia muda wa mtu alivyokaa kazini, bali unazingatia elimu aliyonayo. Nashauri kauni hii itazamwe upya ili kuwapa askari waliofanya kazi kwa muda mrefu, kwa weledi, uaminifu na uadilifu mkubwa ili na wao wapewe kipaumbele katika kuwaongezea madaraka na hasa kwa kuzingatia kwamba majeshi haya yanawategemea watumishi wa kada hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupandishwa vyeo bila kurekebishiwa mishahara; lipo tatizo la askari kuongezewa madaraka bila kurekebishiwa mishahara, jambo linaloathiri ufanisi. Vilevile Askari anapostaafu anajikuta amepata fedha ambayo hailingani na madaraka aliyonayo, ningependa kujua hapa tatizo ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo pia la baadhi ya Askari wanaostaafu kucheleweshewa malipo yao ya nauli na mizigo na fedha za kustaafu kupitia mifuko ya jamii. ningependa kujua hapa tatizo ni nini? Lipo pia tatizo la baadhi ya askari kukatwa madeni zikiwemo fedha za mikopo ya elimu ya juu, wakati mwingine askari hana elimu ya juu na wala hakuchukua mkopo. Swali, ningependa kujua hapa tatizo ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu posho ya chakula ya askari na posho ya vinywaji. Naipongeza Serikali kwa kuwapa posho ya chakula na posho ya vinywaji. Pia ningependa kujua posho ya nyumba kwa Askari wanaoishi uraiani kwa nini hazilipwi na lini zitalipwa? Ningependa kujua ni lini Serikali itawapa Askari Zimamoto posho ya nyumba na kuwajengea nyumba za kuishi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo ya askari. Naipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa askari wetu ili wawe na weledi na uelewa wa pamoja katika kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua askari wanaokwenda kuchukua kozi mbalimbali za usalama barabarani, upelelezi na kozi nyingine gharama za mafunzo hayo nani analipa kwa sababu zipo taarifa kwamba, baadhi ya askari wanaokwenda kila askari atakatwa 7,000/= kwa siku, fedha ambayo hana uwezo wa kuilipa na pia, kuendesha familia yake. Ningependa kujua utaratibu huu umeanza lini na kwa nini Askari akatwe fedha yake ya chakula kwenda masomoni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.