Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Lucy Fidelis Owenya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Idara ya Zimamoto; katika Jiji letu la Dar es Salaam panakuwepo na ongezeko kubwa la majengo na yaliyojengwa karibu sana na majengo mengine ni marefu sana. Pindi linapotokea janga la moto tumeshuhudia sehemu nyingi nchini magari hayo huwa yanaishiwa maji. Pili, kwa majengo marefu yaliyopo Dar es Salaam ni magari mangapi yanayoweza kutoa huduma ya kuzima moto mfano ghorofa ya mwisho kabisa ni ya ngapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dodoma kwa sasa hivi ni Jiji na patakuwepo na ongezeko kubwa la watu na majengo je, Serikali imejipangaje kuongeza magari ya zimamoto Dodoma na nchi nzima na yawe ya kisasa na yenye vifaa vyote vya kuokolea maji, ngazi ndefu, chopa na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makazi ya kuishi Askari Polisi; Askari hawa wanafanya kazi katika mazingira magumu. Mfano Askari wa Barabarani unawakuta wapo barabarani siku nzima wengine kujificha vichakani kuvizia madereva wanaoendesha magari kwa mwendo unaopita limit kupelekea kuhatarisha maisha yao. Hivyo, wakirudi nyumbani wanatakiwa wakute makazi mazuri waweze kupumzika na familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha hata hapa katika Jiji la Dodoma bado zile nyumba za bati kuanzia juu mpaka chini (full suit) bado zipo Dodoma na Askari wetu wanaishi kule. Tukumbuke hali ya hewa hapa Dodoma ilivyo na joto halafu watu waishi kule. Bado vyoo ni vya kuchangia, kichumba kidogo na wana familia, huu si utu kabisa. Je, Serikali ina mikakati gani ya kuwajengea makazi yenye hadhi kwa Askari wetu kwa kuanzia na hapa Dodoma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Askari wa barabarani (Traffic) watumie muda mwingi zaidi kutoa elimu kwa madereva na watumiaji wa barabara, madereva wa bodaboda, baiskeli hata watembea kwa miguu; ajali nyingi zinatokea tu kwa sababu wengi hawajui sheria za barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kuona Askari wetu wakitumika kama wakusanya mapato badala ya kufanya kazi zao za msingi. Kazi za ukusanyaji mapato zifanywe na idara husika na hatuwezi kuendesha nchi kwa faini za magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hali ya amani nchini; pamekuwepo na matukio ya uhalifu unaofanywa na watu wasiojulikana mfano watu wanauawa, kuokotwa katika fukwe za bahari Coco beach Dar es Salaam, watu kutekwa na kuteswa na tukio la hivi karibuni lililotokea huko Tarime kwa kijana Chacha kupigwa kisu na Askari Polisi hadi kufariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ni kitendo cha kulaani sababu raia hata wahalifu hukimbilia Polisi wakijua ndiko wanakwenda kwenye mikono salama lakini haikuwa hivyo. Ni hatua gani Jeshi la Polisi imemchukulia Askari huyo ili lisitokee sehemu nyingine? Je, ni lini Jeshi litatoa report hizo maiti zinazookotwa zinatokea wapi na uchunguzi unaonesha maiti hizo zilifanyiwa nini hadi kufariki (cause of death). Ni vizuri wananchi wakafahamishwa kinachoendelea ili utulivu uliopo usije ukaharibu amani tunayoiimba ambayo kwa sasa haipo.