Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwa na imani nami kwa nafasi hii ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii vilevile kumshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa miongozo ambayo wanaendelea kutupatia katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku.

Namshukuru vilevile Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Watendaji, Makamanda na Maofisa wote waliopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi nikianzia na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakuu wa Vikosi na Taasisi mbalimbali kwa ushirikiano wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naishukuru sana familia yangu kwa ujumla pamoja na wananchi wa Jimbo langu la Kikwajuni kwa kuendelea kuniunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze moja kwa moja kuchangia mada ama maoni mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge ambayo yaliwasilishwa kwa njia ya maandishi na kwa njia ya kuzungumza. Ili kuokoa muda, naomba niwatambue Waheshimiwa hawa Wabunge ambao wamechangia baada ya kutoa ufafanuzi wa hizi hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa pamoja natarajia kuzungumzia mambo kama manne kama muda utaruhusu. Kwanza kabisa naomba nizungumzie suala la usalama barabarani. Hii ni moja katika hoja ambazo zimeibuka kwa kiwango kikubwa sana kwa Waheshimiwa Wabunge. Nachukua fursa hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa jinsi ambavyo wanaonekana wanaunga mkono jitihada za Serikali za kupunguza ajali nchini ambazo zimekuwa zikipoteza maisha ya Watanzania wenzetu na wengine kuwaacha vilema kwa miaka mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inadhihirisha sasa hivi katika Bunge letu Tukufu kuna Chama cha Mabalozi wa Usalama Barabarani chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Adadi. Nawapongeza sana kwa jitihada hizo. Kuungwa mkono kwao, kwetu sisi Waheshimiwa Wabunge kumechangia leo hii kusimama mbele yenu tukijivunia mafanikio makubwa sana ambayo tumefikia kwa kupunguza ajali hizi chini kwa wastani wa asilimia 35.7 toka mwezi Julai, 2017 mpaka Machi mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi ni mashahidi, katika miaka ya nyuma hapa tulikuwa tunashuhudia ajali nyingi zimetokea hasa mwisho wa mwaka, watu wengi walikuwa wanafariki lakini sasa hali hiyo imepungua kwa kiwango kikubwa. Mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa ambayo tunaifanya kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Baraza la Usalama Barabarani na Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi tuliandaa mikakati kabambe ya kupunguza ajali hizo ambapo leo hii tunazungumzia utekelezaji wa mkakati wa awamu ya tatu, tunaenda nao. Katika kila mkakati, tunaangalia upungufu wa mkakati wa kwanza kurekebisha tunapoingia katika mkakati unafuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba maoni yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge leo hapa yatasaidia sana katika kurekebisha upungufu uliojikoteza ili mkakati wetu wa awamu ya tatu tunaoenda nao uweze kuwa na mafanikio zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla hatujazungumza suala la ajali barabarani lazima tujue vyanzo vya ajali barabarani ni nini? Vyanzo vikubwa vya ajali barabarani ni vitatu. Cha kwanza ni upungufu wa kibinadamu ambao mara nyingi unatokana na uzembe na hiki ndio chanzo ambacho kinachangia kwa wastani wa asilimia 76 na vyanzo vingine viwili ikiwemo ubovu wa magari na ubovu wa miundombinu vinafuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia chanzo cha binadamu maana yake mikakati yake ni lazima ilenge katika kushughulikia na changamoto ambazo wanadamu hawa wanasababisha ajali. Ukifanya hivyo maana yake utawagusa hawa binadamu ambao ni wananchi na raia wa nchi hii ambao sisi Waheshimiwa Wabunge ndio tunawawakilisha katika Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamezungumzwa hapa, kwa mfano wapo Waheshimiwa Wabunge waliosema kwamba Askari wetu wa Usalama Barabarani hawana muda wa kutoa elimu, wamekuwa wakitoa fine kwenda mbele tu. Wako ambao walizungumzia kuhusiana na utaratibu mzima wa namna ya utoaji fine, hawajaridhika nao. Yote haya yanalenga katika madereva ambao hao binadamu wanasababisha matatizo ya ajali kwa makosa ya kibinadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mifano miwili, mitatu kuthibitisha hili. Nikichukua ajali za mwisho kubwa zilizotokea, maana bahati mbaya sana ajali za barabarani zikitokea zinavuta hisia nyingi sana kwa jamii kiasi kwamba yale mafanikio makubwa ambayo tunayazungumzia yanafichika. Ikitokea ajali moja inaweza ikaua watu hata 20 kwa mpigo na Taifa linapata taharuki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mifano miwili ya karibuni hii ya mwisho. Kuna ajali ambayo ilitokea tarehe 9 Aprili, kule Mbeya ambapo Lori la Scania lilihama njia na kuifuata Noah. Hao wananchi wasiokuwa na hatia waliokuwa kwenye Noah walikuwa wanaelekea msibani takriban familia nzima. Basi lile likaenda kuivaa ile Noah na kuua takriban watu wanane na kusababisha majeruhi mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchunguzi tulioufanya, chanzo cha ajali hii ni kwamba basi hili liliacha njia na dereva yule sijui alikuwa amelewa au amelala, lakini aliifuata Noah ile na kusababisha ajali ya watu wengi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajali nyingine ambayo ilitokea tarehe 24 mwezi wa Tatu maeneo ya Mkuranga, Lori la Scania vilevile liliacha njia na kuivaa Hiace. Katika ajali hii walikufa watu 24 na majeruhi takriban 10. Tatizo lilikuwa ni mwendokasi. Hizo hizo changamoto za kibinadamu tunazozizungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika hali kama hii na uzembe huu ambao unasababishwa na baadhi ya madereva, mbali na jitihada kubwa za utoaji elimu ambao tunafanya, leo hii mkifungua vipindi vya redio na TV mtakuta Askari wetu wakitoa elimu kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii na makundi mbalimbali, utaratibu hata wa kutoa elimu kabla dereva hajapata leseni ndio aingie barabarani. Juu ya jitihada hizi bado kuna changamoto za madereva ambao wamekuwa hawafuati sheria za barabarani na wamesababisha vifo vya watu wengi wasiokuwa na hatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali kama hiyo, elimu ambayo inabakia, elimu hiyo itatolewe katika Gereza. Maana Gerezani moja ya kazi yake ni kurekebisha tabia za watu waliofungwa, lakini hata kufungiwa leseni na ndiyo maana sasa hivi tunaelekea katika mpango wa kuanzisha utaratibu wa nukta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapofanikiwa kuoanisha mifumo yetu hii wa Polisi na TRA tuweze sasa kufungia leseni mifumo hii ikisomana, lakini itakwenda sambamba na malengo yetu kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amezungumza katika hotuba kwamba sasa suala la leseni tunataka libakie katika Polisi ili kuepusha urasimu usiokuwa na faida. Lingine ni elimu kwa utaratibu wa kutoa fine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tunaomba sana mwendelee kuunga mkono Serikali yenu inapopambana kuhakikisha kwamba inaokoa uhai wa wananchi wanaokufa na wengine kupata vilema bila hatia. Vile vile tunaendelea kutoa elimu. Kwa sauti hizi za Wabunge hatuwezi tukazidharau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusema ni kwamba, nitoe wito kwa baadhi ya Maafisa wetu wa Traffic ambao wanatumia fursa hii vibaya, wachache, kama wapo kuacha tabia hii. Maana makosa mengine ni madogo madogo. Unaweza kukuta mtu pengine kwenye foleni kubwa katika Jiji la Dar es Salaam, halafu hajafunga mkanda unamtoza faini badala ya kumwelekeza. Mambo kama hayo, nadhani wanatusikia, waweze kuzingatia. Tunazungumzia yale makosa hatarishi, lakini yapo makosa madogo madogo ambayo tunadhani wanaweza wakaanza kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine hatutaki baadhi ya Maafisa wetu wa Serikali ama wa vyombo hivi waitie madoa Serikali yetu. Waendelee kusimamia sheria lakini waendelee vilevile kuangalia mazingira na uzito wa makosa yenyewe kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lilikuwepo suala la masuala ya notification. Wapo Waheshimiwa Wabunge walilalamika wakasema kwamba kuna wakati mwingine wanapewa notification lakini hawapewi risiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu kwa ufupi. Ni kwamba bahati mbaya sana hizi mashine tulikuwa nazo katika Mikoa miwili ya Dar es Salaam na Pwani, lakini nataka nichukue fursa hii kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge kwamba tayari tumeshapata mashine takriban 3,000, tunatarajia kuzisambaza mikoani kwa awamu. Zitakapokamilika kutawanywa kote, ambapo sasa hivi tunaanza Arusha na mikoa mingine saba ambayo imeanza kupewa elimu, nadhani changamoto hii itaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwe na hofu, notification ile ina kumbukumbu zote, hakuna mwananchi ambaye atapewa notification, halafu fedha ile isiende kwenye mamlaka husika na iingie mfukoni kwa mtu binafsi. Kwa hilo, tumejiridhisha kwamba kwa mfumo uliopo vilevile fedha hizi ziko salama. Hata hivyo jambo hili tunatarajia kulikamilisha hivi karibuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niingie katika eneo la pili. Jambo la pili ambalo nataka nilichangie ambalo nimekuwa nikilijibu kwa muda mrefu sana katika Bunge letu hili Tukufu ni kutokana na Waheshimiwa Wabunge wengi wa Bunge hili kuguswa na hali ya mazingira ambayo askari wetu wanafanyia kazi. Kama tunavyojua, askari wetu hawa wanafanya kazi ngumu sana katika mazingira magumu. Moja katika mazingira magumu ambayo wanafanyia kazi ni maeneo ambayo wanaishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Waheshimiwa Wabunge leo tukitoka hapa Bungeni baada ya kazi ngumu ya kuwawakilisha wananchi, halafu turudi nyumbani mazingira yakiwa siyo mazuri, nadhani hata concentration ya kazi siku ya pili haiwezi kuwa nzuri. Askari wetu wamekuwa wakifanya kazi hii kwa mafanikio makubwa kwa miaka yote na ndiyo maana nchi yetu iko salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha miaka ya mwanzo hapa wakati tunaingia, suala hili nilikuwa nikilijibu na nilikuwa nikisema, jamani tuna mpango wa kujenga nyumba 4,136 kupitia mkopo wa Exim Bank. Baadaye Waheshimiwa Wabunge wengine katika michango yao wakadiriki kusema kwamba tunawapiga danadana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie tu kwamba wakati mwingine danadana nyingine zinakuwa ni kwa maslahi yetu sisi wenyewe na maslahi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Nadhani sasa hivi wananchi takriban wote wa Tanzania wameshamfahamu, labda wale wasiotaka tu kwa sababu ya ajenda zisizokuwa za msingi. Mheshimiwa Rais wetu amekuwa mara zote akipigania matumizi sahihi ya rasilimali zetu, kwamba fedha ambazo zinatoka za wananchi zitumike kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mfano mmojawapo. Kwamba mradi huu ambao tulikuwa tunatarajia kupata mkopo wa takriban shilingi bilioni 500 kupitia Exim Bank ambao ungejenga nyumba kama 4,136 ukiachia gharama nyingine za Bima, Consultation Fee na kadhalika, unakuta ungeweza kugharimu wastani wa kama dola milioni mia nne na kitu ambapo kwa hesabu ya harakaharaka ukigawa kwa nyumba 4,136 unaweza ukapata dola takriban 98,000, unazungumzia shilingi milioni 220 mpaka 240, nyumba moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais juzi ametoa shilingi bilioni 10 baada ya kujiridhisha juu ya ujenzi wa nyumba ambazo tunajenga kwa kutumia rasilimali zetu za ndani kwa nyumba moja ya Polisi kugharimu shilingi milioni 25. Unaona tofauti hiyo kubwa! Takriban mara kumi au mara tisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungekubali kwenda haraka na mradi ule ambao tumeukuta, tungeweza kupoteza fedha za wananchi ambazo zingeweza kutumika kwa kazi nyingine, lakini tungeweza vilevile kupata nyumba za ziada kwa askari wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wafahamu kwamba Serikali yenu ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ni Serikali makini na inayotoa maamuzi yake kwa maslahi ya Taifa na wananchi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunazungumzia hatua ambayo tunakwenda nayo katika kupunguza changamoto ya ujenzi wa nyumba za Askari wa aina zote tukianzia Magereza, Polisi, Uhamiaji na kwingineko, mpaka Fire na kwingine tutafika huko. Nataka nitoe mfano mmoja. Katika mradi wa Arusha ambapo Mheshimiwa Rais aliuzindua juzi, tulijenga takriban nyumba 31.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais baada ya kuungua zile nyumba alitoa shilingi milioni 250. Nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Comrade Gambo kwa kuhamasisha wadau mbalimbali tukaweza kujikuta tunatumia fedha hizo kujenga nyumba 31. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano huo huo, tumefanya Pemba. Kuna ujenzi wa nyumba unaendelea Pemba tunavyozungumza sasa hivi. Nachukua fursa hii kuwapongeza Wakuu wa Mikoa wote wawili; wa Mkoa wa Kaskazini na Mkoa wa Kusini na wadau mbalimbali walioshiriki. Kuna programu ya ujenzi wa nyumba 36 Pemba. 12 Unguja, 24 Pemba na tayari nyumba 12 tunatarajia zitakamilika kabla ya kumalizika kwa mwaka huu kwa sababu vifaa vyote vya ujenzi wa nyumba zile vipo, vimepatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kutoa wito na kusisitiza Jeshi la Polisi kuzingatia maagizo ya Mheshimiwa Rais pamoja na Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa kutumia fedha hizi zilizotolewa, shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Polisi zitumike kama zilivyokusudiwa. Wahamasishe wadau katika mikoa yao ili tuweze kupata nyumba nyingi zaidi. Lengo letu ni tunatarajia katika pesa hizi tutapata nyumba takriban 400 kwa kuanzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipaumbe vyetu kwanza ni Mkoa wa Dodoma ambapo ni Makao Makuu ya Serikali, yameshahamia. Maeneo mengine ni mikoa yote mipya ya Kipolisi; Simiyu, Njombe, Katavi, Geita, Songwe, Rufiji, Pwani pamoja na Zanzibar. Haina maana kwamba tutaacha maeneo mengine. Ninachozungumza ni kwamba mgawanyo unaangalia ukubwa wa changamoto katika maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba kwa utaratibu huu wa kutumia rasilimali zetu vizuri na leo hii tunazungumzia kuimarisha kikosi chetu cha ujenzi katika Jeshi la Polisi (Police Building Brigade) ambayo tumeiwezesha kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi na kuwapatia mafunzo mbalimbali, hali kadhalika kwa upande wa Magereza, tunafanya hivyo hivyo. Ndiyo maana nyumba ambazo tunajenga Ukonga kwa fedha ambazo Mheshimiwa Rais ametoa kwa utaratibu huo huo, takriban 320, mchango wa Kikosi cha Ujenzi cha Jeshi la Magereza, wafungwa na rasilimali zilizopo kwa kweli unafanikisha sana kufanya tujenge kwa fedha hizi kwa unafuu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uhamiaji ni mashahidi, juzi Mheshimiwa Rais amezindua nyumba 103 pale Dodoma. Kwa hiyo, tunakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini katika miaka michache inayokuja, masuala yenu kuhusiana na changamoto ya makazi kwa askari wetu itakuwa inapungua, haitakuwa tena ni swali la kila siku katika Bunge hili kwa kasi hii. Kwa hiyo, hayo ni moja ya maelezo yangu katika eneo la nyumba za Askari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nizungumzie kwa haraka haraka suala la Uhamiaji haramu. Kwanza nataka nirudishe kumbukumbu nyuma. Wakati Serikali hii inaingia madarakani, tulikuwa tuna tatizo kubwa la wahamiaji haramu katika nchi hii. Mtakumbuka miaka miwili iliyopita tulifanya operesheni kabambe na tukafanikiwa kuwaondoa wengi sana katika mikoa yote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa operesheni hiyo kwa kushirikiana na Wizara yenye mamlaka ya Kazi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tuliweza kukagua makampuni 429 na watuhumiwa takriban 2,199 walikamatwa kwa makosa mbalimbali ya Uhamiaji. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kufikishwa Mahakamani, wengine waliondolewa nchini, wengine walihalalishwa ukazi wao na vilevile tukafanikiwa kuweza kukusanya maduhuli ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumetengeneza nidhamu katika nchi yetu kwamba sasa nchi yetu siyo sehemu ambayo unaweza ukaja tu ukaishi kiholela bila kufuata utaratibu; kwamba unaweza ukaja hapa ukafanya kazi ambazo Watanzania wanaweza kuzifanya, kwamba unaweza ukaja hapa ukajifanya ndio una nguvu zaidi ya kunyanyasa wananchi wa nchi hii. Kuna vijana wetu ambao wangeweza kutumia fursa hizi wakatumia watu wengine wa nje ya nchi bila sababu ya msingi. Nidhamu hiyo imerudi katika nchi yetu kwa kazi kubwa ambayo tumeifanya na tunaendelea kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, operesheni hizi zilikuwa zimetengeneza misingi, maana nchi yetu haiwezi kuendeshwa kwa operesheni. Tumeleta operesheni kutengeneza misingi na mifumo ambayo sasa hivi tunaendelea nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka mmoja huu uliopita, tunazungumzia wahamiaji haramu takriban 13,000 waliokamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali na wengine kushtakiwa, lakini idadi hii kubwa inahusisha pia wale wapitaji haramu. Nataka niseme kwamba wote ni wahamiaji haramu lakini najaribu kutofautisha ili nieleweke vizuri na hasa wale raia wa Ethiopia. Wako Waheshimiwa Wabunge ambao walisema kwa nini tusiwarudishe kwao? Kwa nini tusiwasindikize tu wakaenda wanapoenda midhali hawakai hapa nchini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo siyo tu kukiuka Sheria za Uhamiaji, lakini vilevile ni kukiuka Sheria za Kimataifa kuhusiana na biashara haramu ya kusafirisha binadamu. Kwa hiyo, kama nchi yetu ambayo tunaheshimu misingi ya utawala bora, hatuwezi kufanya hivyo. Tunachokifanya ni kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba jambo hili linakoma na ni endelevu, badala ya kukimbizana nao kila siku, ili rasilimali zetu chache tulizonazo katika vyombo hivi likiwemo Jeshi la Uhamiaji, ziweze kutumika kwa mambo ambayo yana faida zaidi, sisemi kwamba hili halina faida, lakini tuna changamoto nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mkakati kabambe ambao tumeuandaa wa kudhibiti mipaka yetu ambao utahitaji fedha nyingi sana ikihusisha ujenzi wa Mobile Immigrations Posts katika mipaka yetu na kwenye vipenyo vyote tulivyovihesabu katika nchi hii. Kwa kuanzia tunaweza kuanza na vipenyo takriban 107 ambavyo ni vipenyo sugu pamoja na vifaa vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati hayo yanaendelea, tunaomba ushirikiano kwa wananchi katika kupambana na tatizo hili, maana wahamiaji haramu hawa wengine tunaishi nao, wengine wanatoa majumba yao kuwahifadhi hawa. Moja katika mikakati yetu, tunasema kwamba tunataka tufumue mtandao wote wa wasafirishaji wa biashara hii haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri katika hilo tumeshaanza kufanikiwa. Japo najua jambo hili halitachukua muda mfupi, lakini tayari tumekamata watuhumiwa kadhaa ambao miongoni mwao wanahusika na bishara hizi kwamba ni wenyeji, wengine ni wananchi wa nchi hii, maana haiwezi kuwa mtu ambaye anatoka nchi nyingine akafahamu mazingira ya nchi yetu ya kupitisha hawa watu. Kwa hiyo,


wapo watu ambao tayari tumeshawashikilia na sheria inafuata mkondo wake. Katika hili naomba sana wananchi ushirikiano na msaada wenu kulifanikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kuna mikoa ambayo ina changamoto nyingi, hasa Mkoa wa Kigoma. Wapo Wabunge wa Kigoma walizungumza hapa kwa masikitiko na wengine wameandika. Nataka niwakumbushe tu kwamba hata takwimu zetu zinaonesha kwa mazingira ya jiografia ya Kigoma ambayo inapakana na nchi jirani zetu tatu, Mheshimiwa Nsanzugwanko ananikumbusha, ambazo zimepita katika changamoto mbalimbali za kiusalama, siyo jambo la ajabu kuona, mimi nipo zaidi kwa watu ambao wanaitwa wahamiaji haramu. Nanyi ni mashahidi, leo tuna Kambi tatu kubwa za Wakimbizi; Nyarugusu, Mtendeni na Nduta, zote zipo Mkoa wa Kigoma. Wakimbizi wengine badala ya kukaa makambini wanatoroka kuja kukaa uraiani, wengine wanaingiza silaha kutoka katika nchi zao ambazo zinatumika kufanya ujambazi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika hali kama hiyo Serikali lazima ipeleke nguvu zaidi katika mkoa ule ili kuhakikisha usalama siyo tu wa wananchi wa Kigoma lakini wananchi wa Tanzania nzima. Ikiwa kuna upungufu katika utekelezaji wa majukumu hayo, tunayachukua na tunafuatilia. Ila lengo siyo hilo, lengo ni kuhakikisha kwamba wananchi wa Kigoma wanaendelea kuishi vizuri na kwa kufuata sheria. Tunatambua juu ya ujirani mwema uliopo katika ya mikoa yetu iliyopo mipakani yote, siyo Kigoma peke yake, lakini kuna utaratibu wa mahusiano na uingiaji na utokaji kati ya wananchi wanaotoka katika nchi moja na nchi nyingine. Utaratibu huu tutaendelea kuufuata na tunaomba wananchi wa maeneo yote waendelee kuhakikisha kwamba wanatuunga mkono katika hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kwa masikitiko makubwa, kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamechangia na bahati mbaya michango yao wakaielekeza katika misingi ya dini, mingine mwelekeo wa kikabila. Sisi ni watu ambao tumepewa dhamana kubwa sana na wananchi wa nchi hii. Moja katika dhamana kubwa tuliyopewa ni kuhakikisha kwamba kauli zetu tunazozitoa katika Bunge hili zinaendelea kuhakikisha umoja na mshikamano uliodumu katika nchi yetu kwa miaka tokea nchi yetu hii imeungana na imepata uhuru na mapinduzi, unaendelea kuimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nashangaa kwamba sisi tunakuwa ni wepesi sana kusahau juu ya matatizo mbalimbali yaliyojitokeza. Leo tunajivunia juu ya mafanikio makubwa ambayo tumefikia katika kupungua kwa uhalifu nchini. Hata ukiangalia takwimu za uhalifu, labda nitoe mfano wa nchi ambayo inaongoza kwa uhalifu duniani au Afrika; South Africa au Honduras ambayo wanasema katika watu 100,000 watu 98 wanauawa kwa njia mbalimbali, wengine wanapotea, wengine wanatekwa. Nani anajua kama pengine wakati anafanya uhalifu ule alivaa nguo yenye mwelekeo wa dini fulani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi linapofanya kazi yake katika kudhibiti uhalifu halishughuliki na dini ya mtu, halishughuliki na kabila la mtu, halishughuliki na sehemu mtu anapotoka. Wakati mwingine ni matumizi mabaya tu ya hivi vitu. Wapo watu wanatumia dini kwa manufaa ya kisiasa, kitu ambacho siyo sahihi kwa dini zote. Hakuna dini ambayo inaruhusu hilo. Wako watu kwa kukubalika tu anatumia ukanda, siyo sawa. Wapo wahalifu vilevile katika kutimiza uhalifu wao wanaweza wakatumia dini, ukanda au ukabila. Nasi hao tunawa-treat kama wahalifu wengine wowote. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge katika hili tuwe makini sana. Serikali hii ya CCM ni Serikali ya Watanzania wote ambapo Serikali hii imechaguliwa na Watanzania wa dini zote, makabila yote, maeneo yote na rangi zote na iko kwa maslahi ya watu wa aina hiyo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana leo mkimwona Mheshimiwa Rais wetu anahangaika usiku na mchana halali kwa sababu ya kuinua uchumi wa nchi hii ili faida hii ipatikane. Mkiona barabara imezinduliwa, viwanda vinajengwa, ni kwa maslahi ya watu wote wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali au Jeshi la Polisi nasi ambao tumepewa dhamana ya kusimamia, hatuwezi kukubali. Kama kuna Mbunge yeyote ana uthibitisho wa hilo basi waje watuletee, tutafuatilia. Kama kuna mtu ambaye amechukuliwa hatua kwa sababu ya misingi ya imani yake au anakotoka, Waheshimiwa Wabunge, sisi ndio wenzenu, leteni tutafuatilia na kama kuna ukweli hatua zitachukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwani kuna Maaskari wangapi ambao hili suala la usalama barabarani ambalo mmelizungumza sana mwanzo, nikiwapa takwimu za askari ambao tumewashughulikia kwa kukiuka maadili yao katika kusimamia usalama barabani mtashangaa ninyi. Kwa sababu siyo malaika! Ila haiwezekani kosa la mtu mmoja lijumuishe taswira nzima ya Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na kuwaomba sana wawe na imani na Serikali yao na Jeshi lao la Polisi ambalo lipo kwa ajili yao. Hawa mnaowaona, wengine wako kule, wengine hapo, wengine hawapo hapa; hawapati usingizi, hawalali ili Watanzania tulale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tuwe fair Waheshimiwa Wabunge, kwamba wao hawaruhusiwi kuingia humu ndani wakajitetea, isiwe sababu ya sisi kuwazungumza vibaya. Hii ni nchi yetu sote, vyama hivi visitugawe wala siasa zisitugawe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisichukue muda wa Mheshimiwa Waziri wangu, naomba kuwasilisha.