Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Selemani Said Bungara

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi. Leo nakuona kabisa kama Spika kweli kweli! Uko strong, hongera sana. (Makofi)

Msheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi leo na mimi niseme kuhusu habari ya maji. Pili, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji. Tulikuwa tunadai hela tangu mwaka 1992, wananchi wangu walitoa eneo, walikuwa hawajalipwa, lakini kwa Waziri huyu aliyekuja, nilipomwandikia barua moja tu, basi Alhamdulillah vijana wangu wamelipwa hela zao zote. Namshukuru Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema kila siku, tatizo siyo Mawaziri, hakuna Waziri mzigo katika Serikali ya CCM, hakuna! Tena nampongeza Waziri wa Kilimo vilevile vijana wangu walikuwa wanadai, wamelipwa. Naomba sana, Mawaziri hamna makosa, tatizo ni Serikali ya CCM. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilisema siku moja na wakati huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa Waziri wa Ujenzi ndani ya Bunge hili. Nilimwambia Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwamba wewe sio mzigo, mzigo ni Serikali ya CCM. Nikisema hivyo, leo tunasema asilimia 22 ya miradi ya maendeleo ya maji ndiyo imetolewa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, afanye nini Waziri wa Maji wakati asilimia 22 ndiyo aliyopata na asilimia 78 hajapata? Mheshimiwa Waziri tumlaumu wapi? Na sisi ndiyo maana ikija hapa bajeti, tunasema hapana! Siyo hapana hatutaki bajeti ipite, tunasema hapana kwa sababu tunajua ninyi hamuwezi kutekeleza. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, tunasema hapana tunajua tunachokisema ndiyo, hakiwi ndiyo. Kwa hiyo, tunasema hapana kwa sababu tunataka hapana yetu iwe ndiyo, ninyi mjitahidi sasa mseme kwa kuwa Wapinzani wanasema hapana, tufanye mambo haya tuwaone kwamba Wapinzani kama wana…, yale yale, asilimia 22! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana Serikali ya CCM pelekeni fedha katika miradi ya maendeleo. Mkipeleka fedha katika miradi ya maendeleo, sisi tutasema ndiyo. Kama hampeleki fedha, tutasema hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunasema hapana kwa sababu tunajua mnachokisema sicho mnachokitenda. Hii nasema tena, hivi leo mwananchi umuulize ndege na maji nini kianze? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninyi Waheshimiwa Wabunge kama kweli kabisa mnawaonea wananchi huruma, tuwaulize kweli Waheshimiwa Wabunge wa CCM, kununua ndege na kuwapa watu maji, bora nini? Hapa tuseme sasa, wanaosema inunuliwe ndege msimame juu, halafu wananchi wawaone. Halafu wanaosema tuanze maji, wasimame juu halafu tuone kama mtarudi ninyi, mimi sio Bwege. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nakuomba uulize swali hilo, wanaosema ndege inunuliwe wasimame, halafu wanaosema maji yawepo tusimame, halafu tukaoneshe Watanzania huko, he, he, he! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, utaruhusu kidogo tusimame? Naomba sana tuwajali watu wetu, hamna Waziri mbaya, hayupo. Waziri ni Mbunge na anajua matatizo ya wananchi, lakini Serikali ya CCM ni mzigo. Simsemi Mheshimiwa Dkt. Magufuli, ah, ah, Serikali ya CCM ni mzigo. Sio Mheshimiwa Dkt. Magufuli! Mheshimiwa Dkt. Magufuli sio mzigo, Serikali ya CCM ni mzigo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, naomba sana sisi tuna matatizo ya maji katika Mji wa asili wa Kilwa Kivinje, mji mdogo tu wa Kivinje. Mwaka 1980 Mji wa Kivinje tulikuwa tuna mabomba yetu, tunafungua maji, tuliyarithi kwa mkoloni. Leo Kilwa Kivinje kuna Hospitali ya Wilaya. Ndani ya Hospitali ya Wilaya hakuna maji na nilisema siku moja hapa kwamba Hospitali ya Wilaya ya Kilwa Kivinje hakuna maji. Akasimama Mheshimiwa Mkuchika wakachukua matenki ya maji wakaweka hospitalini, wakafungua wakasema Bwege muongo, maji yanafunguka haya. Kumbe wamechukua maji Nangurukuru. (Makofi)

Tunaomba sana, Mji wa Kilwa Kivinje, Mheshimiwa Mkuchika anajua hilo. Wakanisololea sana hapa, lakini Mji wa Kilwa Kivinje hakuna maji. Hospitali ya Wilaya iko Kivinje, watu wananunua maji shilingi 1,000 wanapeleka hospitali. Hospitali ya Wilaya, halafu ninyi mnanunua ndege maskini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri, Hospitali ya Wilaya ipate maji na Mji wa Kivinje na Mji Mdogo wa Kivinje upate maji. Kuna vitongoji saba Nangurukuru, Matandu, Singino, Mgongeni, Magengeni, Mayungiyungi, Kisangi Mjini, Kisangi Shamba, vyote havina maji. Tunaomba sana tupate maji. Kuna vijiji havijapata maji vingi tu, Vimaliao, Pande, Kikole, Luatwe na Nanjilinji hakuna maji. Miaka 57 ya CCM tunaongelea habari ya maji wakati ndiyo nchi ya nne kuwa na maji duniani, lakini hakuna. Hohaa! Serikali ya CCM, amkeni! Hohaa! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hakuna maji, na nimesema hapa Bunge lililopita, kama hatupati maji mwaka 2020 CCM kwaheri, bye, bye, Waheshimiwa! Maji ni uhai, leo mashehe wetu wako Magereza huko, Magereza hakuna maji, na sisi hatuwezi kuswali bila maji. Lazima tutie udhu, tupate maji. Mashehe wako Magereza ya Segerea, maji hakuna. Hawaswali, hawafanyi chochote huko.

Mheshimiwa Spika, tunawaambia kila binadamu kaumbwa na maji, maji ni uhai. Nakusifu sana Waziri wa Maji, namsifu sana Katibu wa Wizara ya Maji Mheshimiwa Kitila Mkumbo, alikuwa huku huku na sijui ilikuwajekuwaje, alikuwa huku huku kwetu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana tuuze ndege mbili tutatue tatizo la maji. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, basi kwa kuwa leo uko vizuri, hebu piga kura, wanaotaka ndege na maji wengi nani? Ahsante sana.