Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuipongeza Wizara kwa jitihada kubwa inazofanya kuhakikisha kwamba tatizo la maji katika nchi yetu linapatiwa ufumbuzi na kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata maji safi na salama kama ambavyo tumeahidi kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa maji, hasa maeneo ya vijijini bado siyo nzuri na hairidhishi. Nashauri kwamba namna ambavyo tunapima upatikanaji wa maji kuna haja ya kuangalia kama upimaji huu unatupa figures ambazo ni sahihi. Tunasema kwamba upatikanaji wa maji sasa hivi maeneo ya vijijini ni asilimia 58 lakini ukienda maeneo ya vijijini kwenye majimbo yetu jinsi hali ya upatikanaji wa maji ilivyo ukiwaambia wananchi upatikanaji wa maji ni asilimia 58, wananchi wanakushangaa. Hali haiko vizuri kabisa na nadhani kuna haja ya kupima kupata hali halisi badala ya hizi takwimu ambazo kimsingi hazioneshi picha halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani namna wanavyopima hii percentage ya upatikanaji wa maji wanaangalia tu fedha zilizotumika kujenga miradi ya maji na kwamba miradi hiyo ingehudumia wananchi wangapi lakini kimsingi kuna miradi mingi fedha zimetumika, imejengwa imefika mwisho lakini haitoi maji na haimnufaishi yeyote.

Mimi Jimboni kwangu kuna miradi miwili ya tangu wakati ile ya Benki ya Dunia, miradi kumi kila Wilaya, kuna miradi mikubwa zaidi ya milioni 400/400 karibu shilingi bilioni moja imetumika lakini mpaka leo miradi ile haitoi maji, wananchi hawanufaiki. Kwa hiyo, katika mahesabu ya wananchi wangapi wamenufaika na yenyewe utakuta inahesabiwa. Kwa hiyo, nadhani kuna haja ya kuwa na hesabu za uhakika kuliko kuwa na figure ambayo ina-mislead; tunasema asilimia 58 maeneo ya vijijini, lakini kimsingi maeneo hayo bado yako chini sana kwa upatikanaji wa maji.

Mheshimiwa Spika, nimeangalia ukurasa wa 130, Halmashauri yangu ya Nzega imepatiwa shilingi milioni 884 kama fedha za ndani kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji vijijini, lakini kama Halmashauri nzima ni shilingi bilioni 2.6 nyingi ni fedha za nje, za ndani ni shilingi milioni 884. Kwa hali halisi ilivyo ya tatizo la maji fedha hizi ni ndogo mno na najua bila fedha hakuna chochote unachoweza kufanya. Kwa hiyo, nashawishika kuunga mkono pendekezo la kuongeza shilingi 50 kwenye bei ya lita moja ya dizeli na petroli ili tupate fedha za kutosha na Halmashauri zetu zipangiwe fedha za kutosha. Hii shilingi milioni 884 kwa mwaka mzima kwa Halmashauri kubwa kama ya Nzega yenye vijiji zaidi ya 167 ambavyo vyote vina hali ngumu ya upatikanaji wa maji, kwa kweli mimi naona hazitatufikisha popote pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuipongeza Wizara na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kuyafikisha Tabora Mjini ambayo yanapita pia Wilaya ya Nzega na baadae yata- branch kwenda Igunga. Huu ni mradi mkubwa, zaidi ya shilingi bilioni 600 zitatumika, siyo jambo dogo, ni jambo kubwa sana. Rai yangu hapa tu ni kwamba usimamizi wa makini unahitajika ili ujenzi wa mradi huu uende kwa spidi ambayo inatakiwa na muda ambao tumewaahidi wananchi kupata maji waweze kupata maji. Kwa sababu zaidi ya vijiji 110 na wananchi zaidi ya milioni 1.1 ndani ya Mkoa wa Tabora watafaidika na maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kwamba sisi watu wa Nzega na hasa Mkoa wa Tabora kwa ujumla tunaangalia maji haya yanayotoka Ziwa Victoria yatakapofika Tabora; Nzega – Tabora – Igunga, sisi haya ndiyo yatakuwa chanzo sasa cha maji kuyatoa yalipofika kuanza kusambaza maeneo mengine. Kwa sababu Mkoa wa Tabora na hasa Wilaya ya Nzega, tuna tatizo la kupata maji chini ya ardhi, visima vingi vinachimbwa hata ukipata maji lakini ni machache ambayo kiangazi visima karibu vyote vinakauka.

Kwa hiyo, tuna shida ya maji chini ya ardhi, sasa maji ya Ziwa Victoria yakishafika Nzega tunayachukulia kama ndiyo chanzo sasa, kuanzia pale tutaanza kuyasambaza kuingiza ndani na kwenye vijiji vingine. Kwa hiyo, tunachukulia maji ya Ziwa Victoria kama kitakuwa chanzo muhimu cha kutupatia maji sasa na kuyasambaza kuelekea maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, niombe Wizara hapa kuwe na flexibility kidogo. Sasa hivi Halmashauri ya Wilaya ya Nzega tuna shilingi bilioni tatu za miradi mikubwa ya visima vya maji, lakini mkandarasi tuliyempa kazi amechimba visima karibu 26 lakini visima ambavyo vimepata maji ya wingi wa lita 4,000 kwa saa ni visima vitatu tu kwa sababu ni shida sana kupata maji chini ya ardhi. Kwa hiyo, kuna hofu kubwa tarehe 30 Juni itafika hela hazijatumika na zitapaswa kurudi na zinarudi siyo kwa sababu ya uzembe wa Halmashauri kutozitumia lakini kwa hali halisi na nature ya Nzega maji chini visima vimechimbwa vya kutosha lakini vyote hakuna maji.

Mheshimwa Spika, kwa hiyo, naomba hapa flexibility ya Wizara kwamba fedha hizi sasa badala ya kutumika kutafuta maji chini ambayo hayapo zitumike kwa usambazaji (distribution) kutoka kwenye vyanzo vya mabwawa na hapo ambako maji ya Ziwa Victoria yatafika. Kwa hiyo, naomba flexibility hiyo Wizara ijaribu kuiangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kidogo kuhusu skimu za umwagiliaji. Kwangu mimi naona hii ni solution ambayo itafanya wananchi wetu ambao hawana uhakika wa maji wawe na kilimo cha uhakika kwa kuwa na mabwawa ya umwagiliaji. Halmashauri ya Wilaya ya Nzega tumepata mabwawa mawili ya Kahama Nhalanga na Lusu, kazi imekamilika, wananchi wameanza kunufaika.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Nzega ni kubwa mno, vijiji 167, vijiji viwili tu kupata mabwawa haitoshi. Tunapenda mabwawa haya watu wa Mambali ambako tathmini ilifanyika kuna uwezekano wa bwawa kubwa kujengwa lijengwe; watu wa Kasela ambako tathmini imefanyika kuna uwezekano wa bwawa kujengwa, lijengwe; watu wa Mwangoye na vijiji vingine vingi tu ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nzega ambavyo tathmini za mabwawa makubwa ya umwagiliaji zilifanyika na zinasubiri tu pesa ni vema mabwabwa yakajengwe. Kwa hiyo, naiomba Wizara ijaribu kufanya upendeleo maalum kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kwa sababu ni halmashauri kubwa, ina vijiji vingi na mtawanyiko wa mvua siyo mzuri, haya mabwawa yatatusaidia katika kuhakikisha kwamba tunapata kilimo cha uhakika.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, nisisitize tu kwamba Serikali ikubali ombi la Waheshimiwa Wabunge la kuongeza hiyo shilingi 50 kwenye bei ya lita ya petroli na bei ya lita ya dizeli. Tuumie sasa lakini tunaumia kwa ajili ya manufaa ya kupata fedha ziende kwenye miradi ya maji ili wananchi wetu waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la msingi tu hapa ni kwamba fedha hizi kweli ziende kwenye miradi ya maji na iwe maji vijijini. Tunafahamu kwamba miradi mikubwa ya maji maeneo ya mijini hasa miji mikubwa ya Dar es Salaam, Arusha na miji mingine ina vyanzo vingine vya fedha, kwa hiyo, hizi fedha za tozo ya mafuta ziwe ni za maji vijijini siyo maji mijini...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja, ahsante sana.