Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninakushukuru na mimi kwa kunipatia nafasi hii kuchangia hoja iliyopo mezani.

Mheshimiwa Spika, sina matatizo na Waziri, Naibu Waziri wala Katibu Mkuu hawa ni wageni, mimi kila nikizungumza nazungumza tuwe wazalendo kwa nchi na Taifa letu. Tukiangalia pesa na mikopo mbalimbali inayotumika kwa ajili ya maji, tukatathmini na maji yaliyopatikana kwa kweli ni mtihani mzito sana kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia kwanza Manispaa ya Lindi na Mradi wa Maji wa Lindi mpaka Mheshimiwa Rais alipata hasira kutaka kumtia ndani yule consultant. Jambo la kushangaza taarifa atakayoambiwa Waziri ataambiwa Lindi kuna maji wakati Lindi hakuna maji. Ule mradi unatia huruma na huzuni kwa nchi hii, zimetumika pesa za mkopo lakini akaunti imefunguliwa India siyo Tanzania. Consultant anakaa India, anatoka India kwa mwezi kuja kuangalia mradi Lindi na anafikia katika mahoteli makubwa anatumia gharama kubwa lakini gharama zile zipo ndani ya huu mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukifikiria huu ni mkopo, wao wanatumia gharama nyingi sana kuliko hata uwekezaji wenyewe wa maji, sasa hasara hii nani mnataka abebe? Hii ndiyo miradi yote ya maji unayiona Tanzania imefikishwa hapo, kuiingiza nchi katika dhahama wakati wao ndiyo wanafaidika hapa tunaendelea kubeba mikopo mikubwa ambayo haina faida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa Mjumbe wa Bodi ya Maji Lindi, mradi wa kutandika mabomba alipewa Ms Jandu, amechukua mara ya kwanza shilingi bilioni saba kutandika mabomba ya maji yakapasuka, akaomba tena bilioni sita ikawa shilingi bilioni 13. Leo ninachokuambia Lindi ukifungua maji yale mabomba yanapasuka, Serikali inaingia tena mzigo wa pili kwa kutengeneza mabomba na siyo kumuadhibu yule mkandarasi. Jamani tunakwenda wapi, huyu mkandarasi yupo na amepewa tena ndiyo miradi miwili wa Chalinze na wa Lindi, miradi hii yote miwili haifanyi kazi, wenyewe wanakaa India, kila kitu India na akaunti India. Hii ndiyo mikataba mibovu ya maji! Haimuhusu Waziri Kamwelwe wao wanaohusika ndiyo wataijua kwa nini wanatuingiza katika mikataba ambayo nchi inapata frustration ya kutosha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiiangalia miradi hii ya mikopo ya World Bank Tanzania nzima utaona ni kafara, kafara hii itawaangukia hawa ambao mwanzo wala mwisho. Tulipewa semina ya jinsi Watanzania tunavyopata tatizo katika masuala ya miradi. Tupo vizuri kuandika feasibility study, kufanya strategic plan, action plan na commitment lakini tupo poor katika management. Ameizungumza Mheshimiwa Ridhiwani kwa kweli usimamizi mbovu hata kama tutawaletea shilingi bilioni 500 bado maji hayatapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kitabu hiki nimeona cha Wizara ya Maji wanasema tuna upungufu wa wataalam kwa vile wale watalaam wa zamani wamestaafu, sasa hata kama unapeleka pesa hauna wataalam kuna nini tena hapo? Ina maana wewe unachukua pesa unapeleka kwa watu ambao siyo wataalam, matokeo yake zile hela zitafujwa na wananchi watakuwa hawapati maji. Tathmini yake ni kuwa hizi hela mnazozipeleka kwa vile hakuna wataalam, hakuna maji, aibu. Tufike mahali tujiulize tumekwama wapi, tumenasa wapi. Suala la kusema tunaomba pesa sikatai ombeni pesa, lakini je hizo pesa zitafanya kazi iliyoandaliwa? Hamna wataalam mnazungumza na kama hamna wataalam kila siku mlikuwa wapi msiseme suala la wataalam, mnafika mahali sasa hivi mnapigana na hela lakini hela ile mkiitoa hamna mtaalam, yale maji yatapatikana wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipata miradi ya World Bank katika vijiji pamoja na Mradi wa Sabodo, jambo la kusikitisha nenda Mchinga hakuna maji, ina maana surveyor na mchimbaji ni watu wawili tofauti, hawana ushirikiano na matokeo yake maji yamekwenda kila walipochimba maji Mvuleni, Mchinga, Kilangala na Chikonje hakuna maji. Hivyo, tena wanatafuta pesa zingine kupeleka kwa ajili ya maji wakati hela zilishapelekwa, hii ni double standard inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inanisikitisha kujiuliza suala la maji unasema unataka kumkomboa mwanamke, hata wanaume wanaweza kujitika maji maana haiwezekani kuleta kuwa lazima maji ajitwike mwanamke, hapana vilevile wanaume wanayo haki ya kuchota maji lakini suala la kujitwika maji na kukomboa maji ni lazima liwe la kila Mtanzania lakini uwepo uzalendo kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee suala la mazingira na tabianchi, nimehudhuria mikutano ya mazingira na tabianchi. Kwa vile Serikali haioni umuhimu hakuna wawakilishi wanaokwenda kuhudhuria mikutano ya mazingira na tabianchi (climate change). Nimekwenda mwaka jana na mwaka juzi hakuna Waziri aliyewakilisha, nchi nzima haina uwakilishi sasa utapate taarifa ya climate change ili angalau muweze kuangalia nini tufanye, haya maporomoko ya maji yanasabishwa na nini ina maana hamtaki kujifunza vitu ambavyo baadae vitakuja kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unakuta kuna mradi unatakiwa shilingi bilioni 500, nakubali lakini kuna kitu kinaingia ndani yake kwanza consultant na ma-expatriate wanatoka India wanaingia ndani ya huo mradi, matokeo yake wao peke yake watatumia karibu shilingi bilioni 100, sasa hata kama utaniambia nalipa ile riba kwa miaka 20 lile deni ina maana kila mwaka mimi nikilipa shilingi bilioni 25 mwakani ita- subsidize itabakia pale pale, ule mradi utachukua hata miaka 50 Serikali hii haiwezi kulipa lile deni na itakuwa ni madeni ya kudumu kila siku tunaingia katika madeni ambayo hayalipiki.

Mheshimiwa Spika, kama mdau naomba andaa Tume Maalum ikaangalie kuna nini kwenye maji, mikataba yao na usimamizi wao uje utupe ripoti hapa tuweze kuichangia tuweze kuijadili. Masuala ya kumuingiza mbuzi ndani ya gunia ukaniletea mbuzi sokoni mimi silielewi. Mara nyingi tunafanya miradi wanasema mikataba sikuoneshi, kama hata Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo haioni mikataba hii inasema nini, mnatuambia nini hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mikataba imefichwa na kama imefichwa kinachoendelea ni nini, ni kuhakikisha nchi inaingia katika dhiki kubwa ya maji lakini hela zinaliwa na wageni.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hapo nakushukuru sana.