Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa nafasi hii na kunijaalia uzima na afya, lakini pia nichukue nafasi hii kumshukuru Waziri na Naibu Waziri, Katibu Mkuu Wizara hii, Naibu Katibu Mkuu na Wakurugenzi kwa kazi kubwa wanayoifanya na nzuri. Tunajua zipo changamoto kadha wa kadha ambazo huwezi kuzikwepa.

Nichukue nafasi hii pia kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu ya Tano kwa kazi ambayo inafanyika chini ya Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikianza na miradi ya maji, Wabunge wengi wamelalamika kuona jinsi ambavyo miradi mingi ya maji ambayo imeanza kwa muda mrefu hasa miradi ile ya vijiji kumi, imechukua muda mrefu kukamilika. Niombe kwa sababu hili limejitokeza pia hata kwenye Jimbo langu la Ngara, miradi ile ya vijiji kumi bado mpaka sasa hivi haijakamilika. Niombe kwamba sasa tuweke nguvu kubwa katika miradi hii ambayo tumewekeza fedha nyingi takribani shilingi bilioni 5.1 kwenye Wilaya yangu ya Ngara iweze kukamilika ili wananchi waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Spika, sambamba na miradi hiyo ya vijiji kumi, kuna vijiji viliongezwa kufikia 13 ambavyo ni vijiji vya Kabalenzi, Murugarama na Kumbuga Kata ya Nyamagoma. Vijiji viwili kati ya hivyo vipo kwenye programu inayoendelea na miradi inakaribia kukamilika. Kipo kijiji cha Kumbuga, Kata ya Nyamagoma, vilichimbwa visima vitatu tangu mwaka 2014 wakamaliza kuchimba lakini pampu hazikufungwa wala DP hazikujengwa ili kuwafikia watumiaji. Kwa hiyo mradi ukatelekezwa. Niombe sasa kwamba mradi huu wa kijiji hiki cha Kumbuga ambapo wananchi wanahangaika, wanatembea zaidi ya kilometa 16 kwa maana ya kilometa nane kwenda na kurudi kufuata maji, mradi huu ukamilike, zinunuliwe pampu zifungwe na DP zijengwe ili wananchi waweze kupata huduma za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaamini kwamba hili litafanyika kwa sababu mmeniongezea pia miradi ya vijiji vitatu; Kijiji cha Mrugina, Mkariza Kata ya Mabawe na Kijiji na Kanyinya Kata ya Mbuba. Kwa maelekezo yaliyotolewa ni kwamba mradi huu wa Kumbuga utaunganishwa kwenye vijiji hivyo, niombe basi kwa sababu tayari wataalam wako site kwa ajili ya kufanya survey kwenye vijiji hivi vitatu na baada ya hapa watatengeneza BOQ kwa ajili ya kutangaza tender, niombe kijiji hiki cha Kumbuga kisisahaulike, kiunganishwe ili iweze kufanyishwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka jana aipotembelea Ngara tuliomba pump akatupatia shilingi milioni 13, tukaomba shilingi milioni 24 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji mjini, tukapewa. Vile vile akatupatia shilingi milioni 75 kwa ajili ya eneo la K9 ambapo kuna kiteule cha Jeshi pamoja na shule mbili za sekondari. Mradi huu unaendelea vizuri, wameshafunga pump, umeme umeshafika kwa hiyo tunaamini kwamba wananchi wataanza kunufaika muda si mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kuna mradi mkubwa ambao niliomba wa kutumia chanzo cha Mto Ruvuvu na kutumia kilele cha mlima Shunga ambao ndio mlima mrefu kuliko milima yote Mkoa wa Kagera ambapo yakijengwa matenki makubwa pale yanaweza yakapeleka maji kwa mtiririko na kwa gharama nafuu Wilaya nzima ya Ngara, Biharamulo, Karagwe kuendelea mpaka hata Mkoa wa Geita kwa maana ya Mbogwe, Bukombe mpaka Chato. Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikifuatilia juu ya hili, nishukuru kwa ushirikiano ambao umenipa na Katibu Mkuu na niliahidiwa kwamba zitatengwa shilingi milioni 200 kwa ajii ya kuanza usanifu.

Mheshmiwa Spika, hata hivyo nimejaribu kuangalia kitabu cha bajeti nimeona fedha za jumla, kwamba kwenye Jimbo langu la Ngara wamenitengea shilingi bilioni 1.7, kati ya hizo shilingi bilioni 1.05 ikiwa ni fedha za ndani. Hakuna mchanganuo lakini nitaomba Waziri atakapokuja kuhitimisha basi unipe ufafanuzi kama hizi shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuanza usanifu wa mradi huu zitakuwa ziko kwenye fungu hili ili angalau niweze kupata amani na wananchi wa Jimbo la Ngara waweze kuamini kwamba sasa tatizo la maji likuwa historia katika Wilaya yetu ya Ngara na Wilaya jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona katika ukurasa wa 195 katika miradi ile itakayotekelezwa katiak mikoa 17 ukiwemo Mkoa wa Kagera ni Mradi wa Rusumo ambao umeelezwa hapa. Mradi huu najua kwamba utatekelezwa katika vijiji vitano; vijiji vitatu vya Kata ya Rusumo ambavyo ni
Nyakahanga, Mshikamano na Kasharazi na vijiji viwili Kata ya Kasulu ambavyo ni Rwakalemela na Nyakariba na hapa imeonesha kwamba fedha hizi zilizotengwa, takriban shilingi bilioni moja ni kwa ajili ya mikoa hii 17.

Mheshimiwa Spika, nitaomba Waziri atakapokuja kufanya majumuisho basi niweze kuelezwa kwamba kwenye mradi huu wa Rusumo ambao utatekelezwa kwa ubia wa Serikali na NELSA ni kiasi gani ambacho tumekuwa tumetengewa kwa ajili ya kuanza kufanya feasibility study, detailed design na kutangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mhandisi mshauri.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye umwagiliaji, nchi ya Misri wanatajirika na uchumi unakua kwa kasi kutokana na kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia Bonde la Mto Nile. Mto Nile asili yake inatokewa kwetu huku Ngara, mto Kagera na Ruvuvu ambayo inapoungana ikaingia kwenye Ziwa Victoria, ndiyo inaenda kutengeneza mto Nile kule, sisi huku mito hii hatujaitendea haki. Sasa naomba kwamba kwenye upande wa umwagiliaji tuwekeze hapo.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia scheme ya umwagiliaji nchi nzima tumeshatumia tu asilimia 1.6 kwa hekta zaidi ya milioni 29 ambazo zinaweza zikafanya kilimo hiki. Niombe kwamba tuweze kutumia fursa hizi ili kuweza kuinua uchumi kwa kutumia scheme za umwagiliaji. Ipo scheme ya umwagiliaji ya Bhigomba ambayo ilishaanza tangu mwaka 1913, ilitakiwa ikamilike 2014, ilianza mwaka 2013 ikamilike 2014. Ilitumia gharama ya shilingi milioni 715 ambayo ilitakiwa kukamilisha mradi, lakini mpaka sasa hivi huo mradi haujakamilika, umetekelezwa. Ukienda kufanya tathmini sasa hivi, kwa tathmini iliyofanyika mwaka juzi inaonekana inahitajika karibuni shilingi milioni 185 ili kukamilisha mradi huo. Niombe kwamba sasa Wizara ya Maji kuukamilisha mradi huu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba mwezi uliopita tumepokea delegation kutoka Kuwait Fund kwa ajili ya kuangalia bonde la Mhongo, ili kuanza usanifu wa scheme ya umwagiliaji katika bonde hili. Niombe kwa sababu tunazo fursa, tuna zaidi ya hekta 5,000 katika Wilaya yetu ya Ngara ambapo tukiweza tuzitumie kwa scheme hii ya umwagiliaji. Kuna scheme tano ambazo tayari Serikali tulishaziingiza kwenye mpango.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 tulitengewa bilioni mbili kwa ajili ya scheme ya umwagiliaji ya Mgozi, Kata ya Mbuba na Mhongo, Kata ya Bukirio lakini fedha hizo hazikutoka. Scheme ya umwagiliaji kwenye bonde hili la Mgozi hata kwenye bajeti hii ya mwaka huu haikuwekwa. Kwa hiyo niombe, kwa sababu ni fursa ambazo zinaweza zikainua uchumi wa wananchi wa Jimbo la Ngara ambao zaidi ya asilimia 80 ni wakulima basi tuwekeze hapo ili kusudi tuanze scheme hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba yapo mazao ambayo unaweza kulima katika maeneo ya kawaida, lakini yapo mazao ambayo huwezi kulima kwenye highlands, inatakiwa yalimwe kwenye maeneo ya mabonde ambapo unaweza ukafanya umwagiliaji na Ngara tumejipanga kwa sababu yapo mazao ambayo tunaendelea kufanyia utafiti ambayo tunaamini tukipata kilimo hiki cha umwagiliaji unaweza ukatumia hekta moja ukawa tajiri kama mazao haya ni kama vile stevia na chia seeds, Waheshimiwa wanajua kwamba tunaweza tukainua uchumi wa wananchi wetu, vile vile tukaboresha hali ya lishe na tukachangia Pato la Taifa. Kwa hiyo, niombe tuwekeze kwenye scheme za umwagiliaji ili kusudi tuweze kuinua kipato cha wananchi wetu na pia tuinue uchumi wa Watanzania, ikiwa ni pamoja na kupata malighafi za kulisha viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niunge mkono uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini, hii itakuwa ni suluhishi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja bajeti hii ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Ahsante.