Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana nami kupata nafasi angalau ya kuchangia mchana huu maneno machache juu ya Wizara hii muhimu kabisa katika maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini niwapongeze sana na nianze na pongezi kwenye Wizara hii. Nimshukuru na nimpongeze sana Waziri wa Ardhi pamoja na Naibu wake, pamoja na Watendaji wao wote kwa namna ya kipekee wanavyofanya kazi lakini kwa ubunifu wa hali ya juu ambao wamekuwa wakiuonesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wenzangu watakubaliana na mimi, kwa mara ya kwanza safari hii tumeona maonyesho makubwa hapa ndani ya Bunge yanayoendana sambamba na taasisi mbalimbali za kifedha ambapo kwa maana ndogo kabisa sisi Wabunge tumepata fursa za kujua vitu ambavyo pengine ingetuchukua zaidi ya siku nyingi kupata fursa ya kwenda kwenye benki, taasisi hizi za National Housing, sijui Watumishi Housing na nyingine nyingi kujadili na namna ya kuona namna ya upatikanaji wa mikopo ya ujenzi wa nyumba zenye gharama nafuu, mimi niwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, niongelee kuhusu Nationa Housing. Nitumie nafasi kuiomba sana Serikali; tunafahamu National Housing Serikali imewekeza fedha nyingi na msingi wake mkubwa ni kuendeleza Shirika hili liweze kujitegemea. Vile vile iko miradi na Kamati imesema vizuri, miradi mingi mikubwa, mizuri, imefanyika kwa muda mrefu na mingine imesimama fedha bado hazijakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali waliunge mkono Shirika hili ili liweze kutimiza wajibu wake kama ambavyo limejipangia na namna ya kutekeleza shughuli nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika 10 ni chache sana, nizungumze sasa juu ya habari ya urasimishaji na umilikishaji wa ardhi. Nirudie tena kusema nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya. Jiji la Mwanza pamoja na Manispaa ya Ilemela na Nyamagana tumekuwa watu wa kwanza katika nchi hii, hivi ninavyozungumza tumeshapima viwanja zaidi ya 42,563.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika idadi hii ya viwanja zaidi ya hati 13,202 zimeshakabidhiwa kwa wananchi. Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Watendaji wa Ardhi wa Manispaa ya Ilemela pamoja na Jiji la Mwanza kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kuwahudumia wananchi wa maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya Serikali kupitia mpango ambao waliuanzisha Dar es Salaam na Wizara ikatoa fedha kwa ajili ya manispaa fulani, sitapenda kuitaja jina ili itekeleze mpango wa urasimishaji makazi, kwenye Kitabu cha Mheshimiwa Waziri amesema wamepima viwanja 6,000 wametoa hati 170 peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu Nyamagana na Ilemela wamefanya kazi kubwa, tunaomba Mheshimiwa Waziri awaunge mkono kwa kuwaongezea fedha nyingi zaidi ili waweze kufanya kazi hii kwa umakini kubwa na wasiendelee kusuasua kama ambavyo wanajitahidi sasa pamoja na kazi kubwa sana hii wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo lingine juu ya namna nzima ya kushughulika na masuala ya utoaji katika suala nzima la umilikishaji. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, alipunguza ile gharama ya premier kutoka 7.5 mpaka 2.5 na sasa Kamati imeomba angalau iwe one percent, nami niendelee kusisitiza hapo aiangalie kwa upana na aweze kuona namna ya kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, program ya ununuzi wa vifaa vya upimaji; Mheshimiwa Waziri ameongea kwenye Ukurasa wa 36, ni jambo nzuri sana kwa sababu atapunguza gharama za upimaji wa maeneo mengi kwenye manispaa zetu na halmashauri zetu. Hii itamsaidia mwananchi kulipa gharama nafuu sana ili sambamba na wakati tulionao sasa aweze kupima maeneo mengi zaidi. Vile vile kila Mwananchi apime akiwa na uhuru mkubwa ili aweze kujisaidia wakati fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri ahadi hii itekeleze. Nafurahi kuona na nimpongeze tena, amesema mwezi wa Saba tunapoanza mwaka mpya wa fedha, fedha hizi na vifaa hivi vitakuwa vimeshapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Master Plan, nchi hii imekuwa ikitengeneza Master Plan nyingi, imekuwa ikitengeneza michoro mingi, lakini Mheshimiwa Waziri hakuna mpango mkakati wa kuhakikisha Master Plan hizi zinatekelezeka kwa wakati na matokeo yake tunaendelea kuchochea migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna nyingine, kama Master Plan hizi hazitafanya kazi kwa haraka, utekelezaji wake ukawa nyuma hatuwezi kufanikiwa kwenye malengo tuliyoyakusudia. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tuweke msisitizo na tuimarishe maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ni kwenye mpango mkubwa ambao tunaufanya sasa wa mpango wa miji mikubwa. Kwenye miji yetu mingi tunayo changamoto moja kubwa, mpango kabambe ni mzuri, lakini hebu tuangalie, wako wananchi kwenye maeneo fulani hawawezi kupimiwa na kupewa hati zao. Sasa hii itakuwa ngumu sana kwa mwekezaji anayekuja kuja kukutana na mtu ambaye si mmilikia halali, hana document ili aweze kumiliki eneo lile na kwenda sambamba na mpango kabambe tuliouandaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala litatukwamisha; yako maeneo ya Kata za Isamilo karibu mitaa nane na mitaa mitano kwenye Kata ya Mbugani pale kwenye Jimbo la Nyamagana. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aangalie na wajadiliaje vizuri, waone namna ambavyo tunaweza kumsaidia mwananchi huyu kwenye Kata hizi mbili za Mbugani na Isamilo ili naye awe kwenye mpango kabambeā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.