Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami nichangie Wizara hii ya Madini. Nasikitika sana, baada ya kusikia taarifa ya Wizara hapa kwamba bado inazungumza suala la STAMICO kuendelea kuwepo kama Shirika la Serikali la kusimamia madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO tumeizungumzia kwa muda mrefu sana ndani ya Bunge hili. Kamati mbalimbali zimezungumza juu ya udhaifu wa STAMICO kwamba imeshindwa kusimamia rasilimali za madini Tanzania. Leo tunasikitika kuona kwamba mpaka leo Serikali bado imeamua kuilea STAMICO kama Shirika la Madini wakati inatuingizia hasara katika nchi hii, imeshindwa kusimamia madini yetu ya vito na madini mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate taarifa kwamba kwa nini Serikali pamoja na STAMICO kuliingizia hasara Taifa hili bado mnaendelea kuibeba STAMICO? Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nazungumza suala la kuongeza thamani ya madini. Wenzangu wamezungumza hapa kwamba Tanzania tuna tatizo kubwa, madini yetu hayachakatwi hapa Tanzania eti kwa sababu zile mashine zinauzwa bei mbaya; na sababu nyingine inatolewa kwamba zile mashine kidogo zinahitaji utaalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana na juzi ndani ya viwanja vya Bunge tunayo mashirika mbalimbali, kampuni mbalimbali za watu binafsi wametuonesha mashine hapa. Zile mashine ni bei rahisi sana. Serikali ingeamua kama kweli ingekuwa na nia ya dhati ya kuchakata madini yetu Tanzania ili yaweze kutoa ajira kwa Watanzania, ingeweza kununua zile mashine. Ni bei rahisi sana tumeambiwa hapa nyuma. Kwa hiyo, naiomba Serikali kwamba, iwekeze kwenye kuchakata madini, madini yachakatwe Tanzania; tanzanite ichakatwe Tanzania. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani wakati tunapitia taarifa ya tanzanite, tanzanite imetoa ajira kwa kiasi kikubwa sana Mji wa Jaipur kule India. Zaidi ya watu laki sita wameajiriwa katika Mji wa Jaipur kule India kupitia madini ya Tanzanite ambayo yanatoka Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la ajabu sana, zile ajira zingeweza kutengenezwa hapa Tanzania, Watanzania wetu wakawa wamepata ajira kupitia madini haya ya tanzanite, madini ambayo yanapatikana Tanzania pekee duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, wakati umefika sasa wa kuhakikisha kwamba tunanunua zile mashine za kuchenjua yale madini ya tanzanite, viwanda viwekwe pale Arusha na maeneo mengine ili Watanzania wetu waweze kupata ajira na siyo tunaenda kuwatajirisha watu wa nje zaidi ya ajira 600,000 kule India, Jaipur. Naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa atuambie wana mkakati gani wa kuleta zile mashine kwa wingi za kuchenjua madini ya tanzanite ili kudhibiti utoroshaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Kamati ya Madini ya Tanzanite ilipendekeza ilikuwa ni ujenzi wa One Stop Centre. Kuwe na eneo moja maalum ambalo madini yetu ya tanzanite yaweze kuuzwa pale, yaweze kuuzwa kupitia mnada, yaweze kuuzwa kwa njia nyingine. Sasa Serikali imejipangaje kutekeleza agizo hili la pendekezo hili la Kamati ya Tanzanite ambayo ililitoa? Mheshimiwa Doto Biteko alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ile. One Stop Centre Tanzanite wamejipangaje mwaka huu kuijenga hapa Tanzania ili madini yetu haya yasitoroshwe? Kwa sababu, tunaambiwa kwamba, madini ya tanzanite huko nje yamezagaa sana kwa sababu, utoroshwaji ni mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kule Kilimanjaro kuna njia za panya nyingi zaidi ya 300. Sasa hivi tunashukuru kwamba Serikali imeweza kujenga ule ukuta, lakini bado yapo maagizio mengine ya Kamati ambayo yalipendekezwa.

Tunaiomba Serikali, kama kweli tuna nia ya dhati ya kuifanya tanzanite iweze kuwanufaisha Watanzania kwa sababu, ni madini yanayopatikana Tanzania tu duniani, tungeweza kudhibiti zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado utoroshwaji tunaamini upo, kwa sababu wachimbaji wadogo wadogo kule wako wengi, kuna leseni zaidi ya 800 pale zimetolewa na agizo hili pia nalo wamelitekelezaje kama Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Doto Biteko, Mheshimiwa Waziri, kulikuwa na pendekezo la Kamati ya Tanzanite kwamba zile leseni zile ziunganishwe kwa sababu, leseni ziko nyingi, zimetolewa zaidi ya leseni 800, eneo dogo la Mererani pale Arusha. Serikali inatekelezaje agizo hili? Kwamba, zile leseni ziunganishwe na wale watu waweke kwenye vikundi, hasa wale wachimbaji wadogo wadogo, ili kudhibiti utoroshwaji wa tanzanite. Tunaomba Mheshimiwa Waziri akija atueleze kwamba zile leseni 800 wamezi-combine au imekuwaje mpaka leo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la kudhibiti haya madini. Ni jambo muhimu sana kwa sababu haya madini yanapatikana Tanzania tu na eneo dogo tu la Mererani, lakini ukienda huko nje bei zake zimekuwa ni ndogo ukilinganisha na thamani ya madini ya Tanzanite. Ukienda maeneo mengi ya India, South Africa, yamezagaa kweli kweli na bei zimekuwa ni ndogo mpaka kule Tuckson, Marekani bei zimekuwa ni ndogo kwa sababu yamezagaa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaiomba Serikali ili kudhibiti haya madini, iweze ku-declare kwamba atakayepatikana anatorosha madini, basi aweze kuuawa, iwe nyara ya Taifa. Lilikuwa ni miongoni mwa mapendekezo ya Kamati ya Tanzanite, sijui Serikali imejipangaje kutekeleza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba iwe nyara ya Taifa kwa sababu ni madini ya kipekee, yako Tanzania tu duniani.

Mtu akikamatwa anatorosha ovyo ovyo huko, ili nasi yaweze kutunufaisha, basi ikiwezekana auawe. Naomba Mheshimiwa Waziri atekeleze hili agizo kwamba tanzanite iwe ni nyara ya Taifa kama nyara nyingine. Kwamba, smugglers wachukuliwe hatua kali ili watu wasiweze kutorosha nchi yetu iweze kuwa na manufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba kuchangia hapa ni suala hili la kampuni hizi ambazo ni kampuni hewa, kuna kampuni nyingi sana za Tanzanite zimeanzishwa. Ukipitia zile taarifa, ile Kampuni ya TML, nayo inamilikiwa na Kampuni ya TML South Africa. Tanzanite South Africa nayo inamilikiwa na kampuni ya Uingereza. Kwa hiyo, yaani tanzanite ina makampuni mengi sana, kampuni mama, kampuni dada hizi kama tatu, lakini wote hawa wanashughulikia suala moja la tanzanite. Sasa Serikali inakosa mapato sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara hii Mheshimiwa Waziri na Manaibu ni watu makini sana. Wachunguze haya makampuni hewa ambayo yapo, yameanzia pale TML, TML Tanzania, kuna TML South Africa, kuna TML England nayo pia ina kampuni mama nyingine huko. Kwa hiyo, hizi kampuni kwa taarifa tulizokuwanazo ni kampuni hewa na zinakwepa kodi kupitia mauzo ya Tanzanite.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba wazipitie hizi kampuni zote ikiwezekana waweze kuzuia wasiziruhusu hizi kampuni kufanya biashara ya madini ya Tanzanite hapa Tanzania. Madini haya ni madini yenye thamani sana. Kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe ya kwamba, inatekeleza hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala hili la madini ya blue sapphire. Tanzania hii madini ya blue sapphire pale ukienda Tunduru yamejaa sana.