Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, na mimi sina budi kwanza kabisa kuungana na Bunge zima kumpa pole sana familia ya Mheshimiwa Tundu Lissu kwa kufiwa na Marehemu Christina ambaye alikuwa ni mwanafunzi wangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ilikuwa ni pigo sana, poleni sana.
Mheshimiwa Spika, naomba nimpogeze sana Mheshimiwa Waziri Mwakyembe kwa hotuba yake ambapo ametuelezea kabisa hatua kubwa ambazo zimeshafanyika na zinazoendelea kufanyika katika kuboresha hali ya utawala wa sheria na Katiba katika Nchi hii. Nashangaa sana na naomba niongee kwa mtazamo wangu kama mchumi, mtu ambaye naelewa hali halisi inayokabili utawala wa sheria. Mwanamapinduzi Karl Marx alisema nanukuu kwamba economics drives oolitics na akasema Karl Marx kwamba power makes law, maana yake ni kwamba uchumi unaendesha siasa na akasema mamlaka, madaraka pia hutengeneza sheria, mwisho wa kunukuu, huyo ni Karl Marx siyo Anna Tibaijuka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi yetu sasa hivi nilisema awali na narudia tena, nchi yetu imebahatika, Watanzania wamekaa wakamchagua Rais ambaye ni kiongozi wa nchi naomba tumpe support, Waheshimiwa wenzetu ambao kazi yao ni kuja kutusimamia sisi, wana haki ya kusema wanayoyasema, pia tuna haki ya kuyawekea context yake kusudi yaeleweke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa uelewa wangu wa mambo, nchi yetu sasa hivi ina nafasi ya kurekebisha yale ambayo yalikuwa yametushinda kusudi twende mbele. Kwa hiyo, Upinzani ukifilisika ukabaki sasa kukemea kwa sababu lazima useme kitu, Bunge linageuka kijiwe. Bungeni hapa hatuleti hoja za vijiweni. Kwa mfano kusema kwamba Tanganyika inainyonya Zanzibar inainyonya katika lipi? Hili ni jambo la kujiuliza! Nimejiuliza kama mchumi tena mchumi kazi yangu ya kwanza ninyi mnanijua nilikuwa kwenye Shirika la Makazi Duniani, hamjui kwamba nilikuwa kwenye Shirika la Biashara la Dunia (UNCTAD) nikisimamia…..
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, linda muda wangu, kwanza kabisa kwa wale wanaosema nimeiba hapa mtaisoma namba, mimi siyo mtu wa kutishwa na vitu vya hovyo hovyo!
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimkiwa Spika, kama kuna mtu anafikiria kwamba mimi naweza nikatishwa hoja za hovyo hovyo huyo asome namba. Soma namba nasimama hapa nataka nitetee vitu ambavyo kwa kawaida watu tunanyamaza lakini sasa mtu anapopotosha hoja inaweza ikaleta hatari.
Mheshimiwa Spika, Tanganyika kwa mtazamo wa kiuchumi, haiwezi kuinyonya Zanzibar kwa mtazamo wa kiuchumi wa haraka. Nimeona niseme hili kwa sababu sheria na Katiba ya nchi yetu nimeona Mheshimiwa amezungumzia Katiba mpya mambo ambayo nilitaka kuyaainisha hapa, kuna suala la Katiba Mpya, Katiba Mpya tuliifanyia kazi wote tukawa tumekwama na Waziri ameainisha.
Mheshimiwa Spika, tunapoleta hoja zetu, tuzilete kwenye mantiki ambayo sasa haipotoshi umma wa Watanzania na kuleta vurugu katika nchi hii. Kisiwa cha Zanzibar nilisema wakati wa Bunge la Katiba na narudia, Kisiwa cha Zanzibar huwezi kusimama ukasema itakuwa Singapore, itakuwa Singapore vipi haina bandari, Comoro ina hali gani?, Commoro ina hali gani?
(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walizungumza bila mpangilio)
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, naendelea kuchangia. Katika dunia ya ustaarabu unasikia hoja, Mheshimiwa Lissu amesoma hapa angeweza kuzomewa lakini wastaarabu wakamsikiliza wamekomaa kisiasa. Sasa ninyi mkianza kupiga kelele ilimradi kelele zote naomba muda wangu ulindwe.(Makofi)
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, suala la Zanzibar tulijadili kwa umakini, tulijadili kwa ukweli, tulijadili kwa haki lakini siyo kwa hoja za vijiweni hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, inapokuja suala la uhuru wa mahakama, wananchi wangu wa Muleba Kusini wa Kata ya Mgunda na Kata ya Karami wako katika hali ngumu. Hakimu pale anakula rushwa ya waziwazi, hatuwezi kusema kwamba Mkuu wa Wilaya ambaye anasimamia maadili ya Mahakimu au Mkuu wa Mkoa ambaye anaangalia aache mambo yaende kama yanavyokwenda. Uhuru wa mhimili wa mahakama haumaanishi kwamba wafanye wanavyotaka na wenyewe wanapofanya kosa lazima sheria itafuata mkondo wake.
Hivyo, suala hili naomba niliweke mbele na Mheshimiwa Waziri utakaposimama kwa sababu tunakutegemea wewe kwamba uwajibishwaji wa mawakili, mahakimu katika sehemu nyingi hasa Mahakama za Mwanzo imekuwa ni mgogoro na shida kubwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Muleba Kusini hali yetu siyo nzuri, tumeshahangaika, hatujui mahali pa kwenda naomba Mheshimiwa Waziri utakaposimama utuambie unavyoweza na jinsi mhimili huu utakavyoweza kusimamia utendaji na uadilifu wa Mahakimu hasa wa Mahakama za Mwanzo. Wamejifanya miungu watu, wanashirikiana wakati mwingine na polisi ambao siyo waaminifu kubambikiza watu kesi na mtu yoyote anayekubali kubambikizwa kesi au kubambikizwa hivi vitu vya hovyo hovyo, mtu dhaifu lazima tusimamie wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, hilo nimelisema naomba kabisa lishughulikiwe na kwa upande wa Muleba Kusini tuko katika hali ngumu, tunahitaji Mheshimiwa Waziri uwasiliane na mahakama utusaidie.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ninataka niliseme, tunapozungumzia sheria na Katiba, utawala wa sheria pia, hauondoi mamlaka ya watendaji wa Serikali kufanya kazi yao kama Mheshimiwa Rais anavyofanya kazi yake kwa speed kusudi twende mbele. Kwa sababu sasa you can not have your cake and eat it, hapa naona kuna hoja za mtu kula keki yake na anataka abaki na keki yake. Serikali ilipofanya kazi polepole wakasema Serikali ni dhaifu, nikasikia kauli kwamba Rais huyu ni dhaifu, Rais anapofanyakazi anasimama mtu anasema Rais anakwenda kiimla, please, mbona tunapingana? Nataka kusema kwamba tunapozungumzia sheria tusiwa-confuse wananchi wetu kwa kusema kwamba Serikali inaendesha kiimla, hakuna Serikali inayokwenda kiimla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho naomba nichangie kwa kusema kwamba, hali za mahakama hususani Muleba na Kagera nyingi zipo katika hali mbaya. Majengo yamechakaa, majengo hayatoshi yanatakiwa yafanyiwe ukarabati. Kwa hiyo, tunapogawa fedha sasa, tunapoimarisha sheria, justice delayed, justice denied kama hakuna vifaa vya kutosha katika Mahakama haiwezekani! Nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye tayari ameshawawezesha muhimili huu wa mahakama ili kusudi waweze kupata fedha wanazozihitaji na kesi ziende haraka.
Kwa hiyo, nataka kusema kwamba kwa upande wa mtizamo wa muhimili huu wa sheria inatulinda wote, hayo tunayoyasema hapa Bungeni ni kwa sababu tunalindwa na sharia, unapotuhumiwa unasimamia haki yako! Hizi kelele za chura haziwezi kumzuia ng‘ombe kunywa maji! Hiyo naomba niseme kabisa. Haziwezi kumzuia ng‘ombe kunywa maji (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nifafanue kwa sababu naelewa mambo mengi. Nilipokuwa Kenya nilishuhudia Rais Mheshimiwa Mwai Kibaki alisimamisha Majaji 23 kwa siku moja, kwa hiyo lazima watu wawajibishwe, lazima kuwe na unautaratibu wa kuwawajibisha watendaji wa Mahakama. Hivyo, msiwa-confuse wananchi, msiwadanganye, mlete hoja, wengi wetu tunazipenda tutazisikiliza lakini ziwe na mashiko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.