Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mariamu Ditopile Mzuzuri (3 total)

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona na kunipa nafasi. Swali langu, je, kwa tafiti ambazo zimefanywa nchi nyingi sana, ikiwemo kwa nafasi kubwa nchi za Kiarabu, sigara ina madhara makubwa, mara dufu kuliko hii Shisha na kila siku tunasema ajira, ajira. Biashara ya Shisha ilikuwa inaajiri vijana wengi sana na kweli wamepata matatizo tangu hili zuio.
Swali langu kwa Serikali; je, mlifanya utafiti wa kutosha wa kuona kwamba hii Shisha ina madhara makubwa kuliko sigara? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mariam kwa kutaka kujua kuhusu utafiti wa jambo hili. Nimhakikishie tu kwamba jambo hili lilifanyiwa utafiti na Wizara ya Afya na hivi vitu ambavyo vina vilevi, ubaya wake ni kwamba vijana wetu hawavitumii peke yake, wanachanganya na vitu vingine, kwa hiyo, wanaongeza makali zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira, nimhakikishie Mheshimiwa Mariam kwamba vijana bado wana fursa nyingi sana na nitolee mfano wa kwake yeye mwenyewe, ni mmoja wa vijana wanaofanya vizuri sana kwenye kilimo na yeye ni shahidi na amefanikiwa sana; ni mmoja wa Waheshimiwa Wabunge vijana waliofanikiwa sana kwenye kilimo. Kwa maana hiyo, vijana wengine wanaweza wakaiga mfano ule, wakalima mazao ya biashara. Mheshimiwa Mariam analima ufuta, wao nawakaribisha walime alizeti ama mazao mengine yanayostawi katika mikoa yao ili waweze kufanya biashara iliyo halali isidhuru maisha ya watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira ya kudumu, ndiyo maana Mheshimiwa Rais ana mpango wa muda mrefu wa kukuza uchumi kwa kuhakikisha kwamba fedha zote zinatumika vizuri ili kuweza kutengeneza uchumi wa viwanda, uchumi unaojitegemea, uchumi unaotengeneza ajira nyingi ambazo zitakuwa zinaingiza kipato halali kwa vijana na afya za Watanzania.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Spika, napenda kwanza kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yana tija kwa vijana wa Mkoa wa Dodoma; na kwa vile yeye mwenyewe ni mtu sahihi, ni Waziri kijana, ni kijana na ni Mbunge anayetokana na Mkoa wa Dodoma, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, moja ya mazao ya biashara yaliyoonyesha kuwa na tija kwenye kilimo biashara Mkoa wa Dodoma ni pamoja na zao la zabibu, lakini mara baada ya Dodoma kutangazwa kuwa Makao Makuu ya Nchi, wageni wengi hususan kutoka katika nchi jirani za Afrika Mashariki, wameonekana kuvutiwa na uwekezaji kwenye zao la zabibu kama zao la biashara. Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga ardhi na pembejeo kwa vijana wa Mkoa wa Dodoma ili wawezeshiriki rasmi kwenye Sekta ya Kilimo cha Biashara kwenye zao la zabibu? (Makofi)

Swali la pili. Kwa kuwa kuna vijana tayari wamejiajiri kwenye ujasiriamali wa mazao, hususan katika zao la biashara la ufuta, lakini hivi karibuni kumetokea sintofahamu kwa Mkoa wa Dodoma hasa kwenye Wilaya ya Kondoa kuwazuia vijana hawa wasinunue ufuta kutoka kwa wakulima kwa kisingizio cha kuwa na stakabadhi ghalani, jambo ambalo halipo katika Mkoa wa Dodoma:-

Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu vijana hawa ambao wameamua kujiajiri?

Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY PETER MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Mariam Ditopile kwa namna ambavyo anawasimamia vijana wa nchi yetu ya Tanzania na hususan Vijana wa Mkoa wa Dodoma. Mwenyezi Mungu akubariki sana.

Mheshimiwa Spika, ni kweli, baada ya tangazo la Makao Makuu na pia baada ya Serikali ya Awamu ya Tano sikivu kufanya marekebisho katika ule mchuzi wa zabibu ili kuwavutia zaidi wakulima wa zabibu kuendelea kuilima zabibu, mwamko umekuwa mkubwa kwa vijana na kama Serikali mkakati wake katika eneo hili ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza, yalitoka maelekezo mwaka 2014 kutoka kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, ya kila Halmashauri nchi nzima kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli za vijana kufanya kilimo. Kwa Mkoa wa Dodoma na hasa katika maeneo ambayo yanalima zabibu, tayari maelekezo yalishatoka na katika master plan ya Jiji la Dodoma, ambayo itakwenda kukamilika hivi karibuni, yametengwa maeneo maalumu ya kuhakikisha kwamba zao hili la zabibu halipotei.

Mheshimiwa Spika, hivyo, vijana pia watapata fursa ya kuweza kunufaika kupitia maeneo hayo ili nao waweze kulima zabibu na kujiongezea fursa ya kuendeleza mitaji yao na biashara zao.

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi kuliko yote ni kwamba, Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika maeneo yake ambayo wametenga kwa ajili ya shughuli za vijana, wameshapeleka wataalam kwenda SUA kukaa na wataalam wa SUA kwa ajili ya kuja na mpango mzuri endelevu wa kilimo cha zabibu ambacho kitakuwa kimefanyiwa utafiti ili vijana wengi zaidi waweze kunufaika.

Mheshimiwa Spika, siyo zabibu tu, kwa Dodoma hapa, vijana wengi hivi sasa wanafanya biashara za mazao, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema; na hivi sasa tayari tunavyo viwanda ambavyo vimeanza kufanya kazi. Kwa mfano, Kiwanda cha Mazao Mchanganyiko ambacho kwa mwaka kitahitaji tani 12,000 za mahindi na tani 6,000 za alizeti. Kwa hiyo, tunachukua fursa hii pia kuwaalika vijana kushiriki katika kilimo hicho.

Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, analijibu Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo ambaye ameandaliwa kwa ajili ya kulijibu swali hilo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameyatoa. Ni kweli kabisa kumetokea sintofahamu katika zao la ufuta katika maeneo mengi hapa nchini na hasa katika mikoa ambayo inazalisha kwa kiwango kikubwa sana. Utaratibu ambao tumeweka kama Serikali, ni kwamba tunatumia ule utaratibu wa mwaka 2018 wa kuhakikisha, mtu yeyote anayetaka kununua ufuta, anaruhusiwa kwenda kununua maadam afuate taratibu zinazostahili; na wote wanaruhusiwa na hatujaweka masharti yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kumetokea katika baadhi ya mikoa, wanasema kwamba tunatumia mfumo wa soko la bidhaa yaani TMX na kuna maeneo mengine wanalazimisha kwamba wanaoruhusiwa ni hawa, hatujaweka huo utaratibu. Kila mtu anaruhusiwa kwenda kushiriki na huo utaratibu wa soko la bidhaa utakapokamilika, tutatoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili kuanza kutumia huo mfumo. Kwa mwaka huu kwa sababu mfumo hatujaukamilisha sawasawa, basi mfumo wa zamani unaendelea kutumika.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Kilimo; kwa kweli wakulima wa alizeti wameona neema kubwa sana. Hivi tunavyoongea bei ya mbegu ya kilo moja ya alizeti ni 1600, haijawahi kutokea katika nchi yetu. Kutokana na bei hiyo kupanda na kuleta matumaini makubwa sasa muamko umekuwa mkubwa kwa watu kwenda kulima alizeti.

Je, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imejipangaje kutuletea mbegu nyingi za kutosha na za kisasa ili tuweze kulima zao hili kwenye msimu unaokuja hasa kwa Mkoa wetu wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ditopile kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali sasa hivi tumeanza kuchukua mahitaji ya mikoa wanayotuletea wao wenyewe kutokana na uwezo wa mkoa husika katika suala la uzalishaji. Katika mkoa wa Dodoma tunashirikiana kwa karibu kabisa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na RAS ambayo ina-coordinate kutuletea mahitaji ya kila Wilaya ili sisi kama wizara tuweze kuwapatia mbegu. Nataka niwahakikishie wakulima kuwa mwaka huu tutahakikisha wakulima wa alizeti wanapata mbegu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto zilizoko duniani za upatikanaji wa hybrid seed lakini at least tutahakikisha kwamba wakulima wote wanapata angalau standard seed ambazo zitaweza kuwasaidia katika mwaka huu na sisi Serikali wakati huo tunajipanga vizuri kwa ajili ya mwaka mwingine ili tuwe na hybrid za kutosha. Tumeshafanya aggregation tumeshaingia mikataba na wasambazaji na, hivi karibu tutaanza kusambaza mbegu kutokana na mahitaji ya mkoa husika.