Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mwantum Dau Haji (16 total)

MHE. MWANTUMU D. HAJI aliuliza:-
Vijana ndiyo nguvu kazi ya kutegemea katika Taifa hili na ulimwenguni
kote. Kwa bahati mbaya, vijana wetu wengi wameathirika sana na madawa ya
kulevya kiasi kwamba, badala ya kuwa nguvu kazi, imekuwa ni mzigo mkubwa
kwa familia zao na Taifa kwa ujumla.
Je, Serikali imejipanga vipi kuona inawanusuru vijana katika janga hili?
MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI - NAIBU WAZIRI, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA,
VIJANA NA WALEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu napenda kujibu swali la
Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa, matumizi ya dawa za
kulevya yana madhara mengi kwa watumiaji, familia na jamii kwa ujumla. Ili
kuwanusuru vijana wetu na madhara hayo Serikali imechukua hatua zifuatazo:-
1. Kuongeza juhudi za dhati za kimkakati za kuhakikisha za kuhakikisha wale
wote wanaojihusisha na biashara hii haramu wanakamatwa na
kuadhibiwa vikali kupitia Sheria Na. 5 ya mwaka 2015.
2. Kuendeleza huduma njema na endelevu ya Serikali ya kutoa matibabu
kwa watumiaji wa dawa za kulevya katika hospitali na vituo vya
wagonjwa wa akili nchini, ili kuwasaidia watumiaji wa madawa hayo
kuacha.
3. Kuendelea kuratibu na kusaidia kusambazwa kwa nyumba za ushauri
nasaha na upataji nafuu (Sober Houses) na huduma za kuwafikia
watumiaji katika miji mbalimbali nchini.
4. Kuanzisha huduma ya tiba kwa kutumia dawa ya methodone katika
hospitali zetu.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Kwa kuwa barabara kuu kwenda mikoani zina foleni na tukiangalia barabara hizo zinatumika na magari mengi ya mizigo ambayo mara nyingi huwa ni chanzo cha ajali na Watanzania wengi kupoteza maisha:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ajali hizo zinapungua?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyowahi kujibiwa swali la msingi namba 13, 74, 75 na 167, katika Mikutano mbalimbali ya Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zipo sababu nyingi za vyanzo vya ajali za barabarani nchini. Utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa, sababu hizo zimegawanyika katika makundi makuu matatu:-
Kwanza, sababu za kibinadamu kama vile ulevi na uzembe zinazochangia asilimia 76 ya ajali zote.
Pili, ubovu wa vyombo vya usafiri zikiwemo hitilafu za kiufundi na mfumo wa umeme wa magari unaochangia asilimia 16.
Tatu, mazingira ya barabara yaani ubovu, ufinyu na usanifu mbaya wa barabara zetu unachangia asilimia saba tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa, suala la msongamano wa magari ambao linahusiana zaidi na mazingira ya barabara linachangia kiasi kidogo cha ajali ikilinganishwa na sababu zingine nilizozitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ajali nchini ni tatizo ambalo kutokana na madhara yake kwa umma, Serikali itaendelea kukabiliana nalo kwa nguvu zote. Kwa kuzingatia hali hii, Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani likishirikiana na wadau wengine wa usalama barabarani limechukua hatua zifuatazo:-
(1) Kusimamia kwa karibu mifumo ya sheria ukiwemo utaratibu mpya wa malipo ya papo kwa papo (notification) kwa njia ya kielektroniki ulioanzishwa hivi karibuni katika Jiji la Dar es Salaam na baadaye kutumika kwa nchi nzima.
(2) Kunyang‟anya leseni za madereva wazembe wanaorudia kutenda makosa ya usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani pindi wanaposababisha ajali.
(3) Kuwafukuza au kuwabadilisha kazi Askari wa Usalama Barabarani wanaotuhumiwa kujihusisha katika vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikichochea ongezeko la ajali barabarani.
(4) Kutoa elimu na namba za simu za viongozi wa Kikosi cha Usalama Barabarani kwa wananchi ili wafahamu haki zao wanapokuwa abiria au watumiaji wa barabara na kutoa taarifa wanapotendewa isivyo halali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kuwaagiza madereva na watumiaji wengine wa barabara kote nchini kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani na kutoa taarifa za dereva, askari au mtu yoyote anayekiuka sheria za barabarani au taratibu za kazi kwa makusudi ili hatua stahiki zichukuliwe.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Hivi sasa kumeibuka wimbi kubwa la wagonjwa wa kisukari na miongoni mwa waathirika ni wanawake wenye kipato cha chini:-
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kisukari katika zahanati na vituo vya afya vya Serikali ili kusaidia watu wasio na uwezo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa ugonjwa wa kisukari ni moja ya magonjwa yasiyoambukizwa yanayoongezeka kwa kasi hapa nchini. Kitaalam imethibitika kuwa moja ya sababu kubwa ya ongezeko la ugonjwa wa kisukari hasa kwa watu wazima linatokana na mtindo wa maisha kama vile kutokufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika,ugonjwa wa kisukari unahitaji wataalam wenye ujuzi wa kumchunguza mgonjwa na kuhakikisha maendeleo yake ya kiafya yanakuwa mazuri na pia kubaini magonjwa yatokanayo na kisukari na kuyadhibiti mapema kabla hayajaleta madhara kwa mgonjwa. Madhara yake mara nyingi ni kama vile kukatwa mguu, athari kwenye macho, figo na moyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu sasa huduma za matibabu ya kisukari zimekuwa zikipatikana katika ngazi ya Hospitali ya Wilaya. Hii imetokana na ukosefu wa watumishi wenye ujuzi na weledi wa kuhudumia wagonjwa wa kisukari katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya. Pia mwongozo wa matibabu yaani standard treatment guidelines umeelekeza dawa za kisukari kupatikana kuanzia ngazi ya Hospitali ya Wilaya na kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maboresho yanayoendelea katika sekta ya afya ikiwemo kutoa mafunzo kwa watoa huduma katika ngazi za zahanati na vituo vya afya, Serikali itaanza kutoa huduma za matibabu ya kisukari katika ngazi hizo kwa awamu kuanzia kwenye vituo ambavyo watoa huduma wamepata mafunzo. Mpaka sasa watumishi wapatao 150 wamepewa mafunzo kuhusu matibabu ya akinamama wajawazito wenye matatizo ya ugonjwa wa kisukari. Pia mwongozo wa matibabu utafanyiwa mapitio na Wizara yangu ili uendane na mahitaji ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwapima wagonjwa wa kisukari zinakuwepo katika vituo vyote vya huduma za afya zenye kliniki za wagonjwa wa kisukari katika halmashauri zote zilizopo hapa nchini. Pia utoaji wa Huduma za Mkoba (Outreach clinics) utaimarishwa katika maeneo yasiyo na kliniki.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa IV wa Afya wa mwaka 2015 – 2020, mwelekeo ni kuongeza kasi ya kuzuia kuongezeka kwa wagonjwa wa kisukari kupitia uelimishaji kwenye jamii na mashuleni. Pia uhamasishaji wa kula vyakula visivyoongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari na kufanya mazoezi. Vilevile utambuzi wa mapema wa ugonjwa na kupata matibabu mapema kupitia mifumo iliyopo ni mambo ya kipaumbele katika miaka mitano ya kutekeleza mpango mkakati wa sekta ya afya.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Askari wa usalama barabarani ndio wenye dhamana ya kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara, lakini kwa sasa askari hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha askari wa usalama barabarani wanakuwa waadilifu na hawajihusishi na vitendo vya rushwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mhehimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi limekuwa na mikakati ya kuhakikisha askari wa usalama barabarani hawapokei rushwa kwa kufanya yafuatayo:-
(i) Kutoa elimu wa askari wote wakiwemo wa usalama barabarani juu ya madhara ya rushwa katika mabaraza, kwenye komandi na vikosi, ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo kwa askari kabla ya kuingia kazini na baada ya askari kutoka kazini.
(ii) Kutoa namba za simu za viongozi wa polisi, viongozi wa mamlaka nyingine za ulinzi na usalama kwa umma.
(iii) Mfumo wa kutoa notification kwa kutumia mashine za kielektroniki ambayo nimoja wapo ya mkakati wa kukomesha rushwa barabarani.
(iv) Kusambaza mabango katika maeneo mbalimbali yanayopiga vita rushwa.
(v) Kuanzishwa kwa masanduku ya maoni ili kutoa malalamiko katika vituo vya polisi.
(vi) Kuwasimamia na kuwakagua mara kwa mara askari hawa katika maeneo yao ya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mikakati hiyo Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje kuhusu huduma ya mabasi yaendayo kasi pale umeme unapokatika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakala wa mabasi yaendayo haraka umejipanga vizuri kwa kuweka jenereta moja katika kila kituo kikubwa, ambalo hutumika kama chanzo cha umeme pale umeme wa TANESCO unapokatika. Vituo vikuu vilivyowekewa jenereta ni vya Kimara, Ubungo, Morocco, Kivukoni, Gerezani na katika karakana iliyopo Jangwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia kupitia DART imeweka betri za kutunza umeme (backup batteries) katika vituo vyote vidogo 27 ili zitumike kama chanzo cha umeme, pale umeme wa TANESCO unapokatika.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Kilimo cha Tanzania hutegemea mvua za msimu ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo. Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa mpango wa Taifa wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2007 na mkakati wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2012 katika sekta mbalimbali ikiwemo na sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, mipango hii kwa sekta ya kilimo imejikita katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia zinazopunguza upotevu wa maji ili kuepuka kilimo cha kutegemea mvua, kubadili vipindi vya upandaji mazao ya misimu ili kuendana na mabadiliko ya misimu, ikiwa ni pamoja na kupanda mazao na mbegu zinazohimili ukame, kuboresha mbinu za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao na kuweka mifumo mbadala ya kilimo ili kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa inashirikiana na wadau wengine ikiwa ni pamoja na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika suala zima la kuleta maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo kwa kuandaa mpango mahususi wa sekta ya kilimo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Mpango wa Taifa wa Kilimo Rafiki cha Mabadiliko ya Tabianchi na programu mbalimbali za uendelezaji wa kilimo. Katika utekelezaji wa mipango na programu mbalimbali za uendelezaji wa kilimo.
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa mipango na programu hizi katika sekta ya kilimo suala la kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika kilimo limezingatiwa hasa kwa kusisitiza uwekezaji katika miundombinu ya kilimo, kuongeza tija kupitia kilimo cha umwagiliaji na teknolojia bora za uzalishaji kupitia kilimo shadidi, kuboresha mfumo wa upatikanaji wa mbegu bora, kuwekeza katika utafiti wa mazao ya kilimo, kutumia sayansi na teknolojia za kisasa katika kilimo kulingana na misimu na hali ya ukame na msingi mingine inayolenga kuweka mbinu mbadala za kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Kumekuwa na sintofahamu ya matumizi ya ardhi pamoja na masharti maalum yanayotakiwa katika mapori yetu hususan kwa wawekezaji na wananchi wanaozunguka hifadhi na mapori tengefu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya hifadhi na mapori tengefu yametengwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009.
Aidha, uwekezaji katika hifadhi, mapori ya akiba na tengefu, maeneo ya wazi yenye wanyamapori, maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi na Wanyamapori (WMAs) husimamiwa na sheria hiyo. Sheria na Kanuni husika hutoa taratibu za usimamizi wa maeneo hayo muhimu kwa maslahi ya uhifadhi, maliasili na mazingira, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi kupitia matumizi endelevu. Mwekezaji anapaswa kupata kibali na leseni ya kumruhusu kuendesha shughuli za utalii kutoka mamlaka zinazohusika kabla ya kuanza biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali inapitia upya kanuni na taratibu za uwekezaji katika maeneo ya hifadhi na mapori tengefu, miongoni mwa kanuni zinazopitiwa ni pamoja na Kanuni ya Jumuiya za Hifadhi Wanyamapori (WMAs).
Aidha, Serikali iko katika hatua za mwisho katika maandalizi ya kanuni za maeneo ya mapito (shoroba) ya wanyama na mtawanyiko wa wanyamapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara itaendelea kutoa elimu kwa wawekezaji na wananchi wanaozunguka maeneo yaliyohifadhiwa. Aidha, natoa wito kwa wawekezaji kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuepukana na migogoro ya ardhi baina ya wanavijiji, wawekezaji na Mamlaka za Hifadhi.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA (K.n.y) MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inarejesha kasi ya kupambana na dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mantumu Dau haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeongeza kasi na harakati za kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini baada ya Bunge lako Tukufu kutunga Sheria mpya ya Kudhibiti na Kupamabana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015. Sheria hii imeipa Serikali Mamlaka ya kuanzisha chombo chenye nguvu cha kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, ambacho kiliundwa rasmi mwezi Februari mwaka 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka hiyo imepewa nguvu Kisheria ya kuweza kukamata, kupekua, kuzuia mali na kuchunguza mashauri yote ya dawa za kulevya na makosa mengine yanayohusiana nayo ikiwemo mali zitakazothibitika kupatikana kutokana na dawa za kulevya. Hata hivyo, Serikali katika kuongeza kasi ya kupambana na dawa za kulevya, mwaka 2017 ilifanya marekebisho makubwa ya sheria hiyo na kuipa nguvu maradufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takribani mwaka mmoja sasa tangu kuundwa kwake hadi kufikia mwezi Februari mwaka 2018, Mamlaka imekwishakamata jumla ya watuhumiwa 11,071; kati ya hao, watuhumiwa 3,486 ni wafanyabiashara wa dawa za kulevya na tayari wameshafikishwa Mahakamani. Kutokana na kuongezeka kwa kasi ya kupambana na dawa za kulevya imesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa cha matumizi ya madawa ya kulevya nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote kushiriki kikamilifu katika juhudi za Serikali za kupambana na dawa za kulevya kwani madhara yanayotokana na matumizi ya dawa hizo kwa namna moja ama nyingine yanatuathiri sote kwa njia mbalimbali ikiwemo kuongeza vitendo vya uhalifu, matumizi ya Serikali katika kuwahudumia waathirika pia.
MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:-
Ubakaji na udhalilishaji wa wanawake na watoto nchini bado ni tatizo kubwa:-
Je, Serikali inasema nini katika kupambana na wanaume wanaodhalilisha wanawake na watoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kuipongeza sana Timu ya Simba. Wahenga wanasema; mla mla leo, mla jana kala nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwatum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa lipo ongezeko la vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa wanawake na watoto kwa mujibu wa matukio yaliyoripotiwa katika vyombo vya dola na vyombo vingine vya umma. Katika kukabiliana na tatizo hili, Serikali kwa kushirikiana na wadau inachukua hatua zifuatazo:-
Moja, Serikali imezindua Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano wa Kutokomeza Vitenda vya Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) wa mwaka 2017/2018
– 2021/2022. Kupitia mpango huu, Serikali imedhamiria kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji na ukeketaji wa watoto wa kike kutoka asilimia 15 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia saba mwaka 2022. Utekelezaji wa mpango huu umeanza kwa kutoa mafunzo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika mikoa yote na baadhi ya Asasi Zisizo za Kiserikali yaliyolenga kuwajengea uwezo wa namna bora ya kutekeleza mpango huu.
Pili, tumeanzisha madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya polisi ambavyo kwa sasa tuna jumla ya madawati 417 ambayo yamewezesha kuongezeka kwa mwamko wa wananchi kujiamini na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji, ulawiti kwa watoto na udhalilishaji wa wanawake katika maeneo yao.
Tatu, tumeanzisha vituo vya one stop center na vituo hivi vimekuwa na madawati ya polisi, ushauri nasaha na huduma za afya katika eneo moja, tofauti na sasa ambapo wahanga inabidi waende kwanza polisi wachukue fomu waende hospitali wapate ushauri nasaha, jambo ambalo linapoteza muda. Vituo hivi tumevianzisha katika Hospitali ya Amana kule Mbeya; Hai, Mkoa wa Kilimanjaro; na Kahama katika Mkoa wa Shinyanga.
Nne, Serikali inaendelea kuhamasisha utekelezaji wa Sheria na Kanuni za Adhabu, Sura Na. 16 na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 na kuhimiza wazazi, walezi, jamii na wahanga wa vitendo vya ukatili kutokaa kimya pindi wanapoona watoto au mwanamke anafanyiwa vitendo vya ukatili ili kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale wote wanaowatendea watoto na wanawake vitendo hivyo vya kinyama vinavyopelekea madhara ya kimwili, kiafya, kisaikolojia, hata kifo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2017, Jeshi la Polisi limeripoti jumla ya matukio 41,416 ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake. Kati ya matukio hayo, matukio 13,457 ni ya ukatili wa kijinsia kwa watoto. Serikali inakemea udhalilishaji na ubakaji wa aina yoyote kwa wanawake na watoto. Aidha, natoa rai kwa wananchi wote kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawashawishi na kuwashauri wananchi kutomaliza mashauri yaliyopo katika vyombo vya dola katika ngazi ya familia.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Kumekuwa na ucheleweshaji wa mishahara kwa watumishi wa umma:-
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Waraka wa Hazina Na.12 wa mwaka 2004, watumishi wa umma wanatakiwa kulipwa mishahara yao kabla ya tarehe 25 ya kila mwezi. Kumbukumbu za malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma zinaonyesha kuwa, kuanzia Julai, 2017 hadi Agosti, 2018 watumishi walilipwa mishahara yao kati ya tarehe 20 na 24 ya kila mwezi. Hivyo basi, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na umma kwa ujumla kuwa hakuna ucheleweshaji wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma.
MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:-
Kilimo cha Tanzania hutegemea mvua za msimu ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwatum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Sekta ya Kilimo, Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa Mpango wa Taifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2007 na Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012 katika sekta mbalimbali ikiwemo na sekta ya kilimo. Mipango hii kwa sekta ya kilimo imejikita katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia zinazopunguza upotevu wa maji ili kuepuka kilimo cha kutegemea mvua.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mipango hii inaelezea namna ya kubadili vipindi vya upandaji mazao ya misimu ili kuendana na mabadiliko ya misimu ikiwa ni pamoja na kupanda mazao na mbegu zinazohimili ukame, kuboresha mbinu za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao na kuweka mifumo mbadala ya kilimo ili kuongeza uzalishaji. Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais ipo katika mchakato wa kukamilisha kuandaa mpango endelevu wa Kitaifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (National Adaptation Plans). Mpango huu utakapokamilika utawezesha nchi kuwa na mipango itakayowezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta muhimu ikiwemo sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa inashirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Maji na Umwagiliaji katika kuandaa mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Sekta ya Kilimo. Mipango iliyoandaliwa ni pamoja na:-
Moja, Mpango Mahususi wa Sekta ya Kilimo katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Tanzania Agriculture Climate Resilience Plan); pili, Mpango wa Kitaifa wa Kilimo Rafiki cha Mabadiliko ya Tabianchi (National Climate Smart Agriculture) na programu mbalimbali za uendelezaji wa kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa mipango na programu hizi katika sekta ya kilimo, suala la kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika kilimo imezingatiwa hasa kwa kusisitiza uwekezaji katika miundombinu ya kilimo (suala la kuongeza kilimo cha umwagiliaji).
MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:-

Kuna baadhi ya Askari Polisi kupandishwa vyeo lakini hawapati stahili zao kama inavyotakiwa:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia askari hao stahiki zao?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwatum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa upandishaji vyeo kwa Askari Polisi hutekelezwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za Jeshi la Polisi ikiwemo kupandishwa vyeo baada ya kuhudhuria na kufaulu mafunzo stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kuwa Jeshi la Polisi kama ilivyo kwa Wizara na Idara nyingine za Serikali lilihusika na zoezi la uhakiki wa watumishi, zoezi ambalo pia lilisitisha marekebisho yoyote kwenye daftari la mishahara, ajira mpya pamoja na upandishwaji vyeo kwa Watumishi wa Serikali. Baada ya zoezi hilo kukamilika tayari Maofisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali zaidi ya 8,440 waliokuwa na madai mbalimbali yakiwemo stahiki za kupandishwa vyeo wamesharekebishiwa mishahara na stahili zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Maofisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wapatao 2,143 kati ya 3,089 waliopandishwa vyeo mwezi Juni, Septemba na Disemba, 2018 wamerekebishiwa mishahara yao. Hata hivyo taratibu za kukamilisha kuwarekebishia Askari waliobaki zinaendelea ili kuhakikisha kuwa Askari wote waliopandishwa vyeo wanarekebishiwa mishahara yao kulingana na vyeo vyao vipya.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Kuna wagonjwa wa Kisukari, Shinikizo la Damu na Kansa wanapata shida kubwa ya kiafya:-

Je, Serikali ina mpango gani katika kuwapatia huduma ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisukari, Shinikizo la Damu na Saratani ni kati ya magonjwa yajulikanayo kama magonjwa sugu au magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka sana duniani kote ikiwa ni pamoja na Nchi Zinazoendelea, Tanzania ikiwepo. Ongezeko hili lilianza kuonekana tangu miaka ya tisini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Sera ya Afya ya Mwaka 2007, ilitoa tamko la kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Aidha, mnamo mwaka 2009, Serikali kupitia Wizara ya Afya, ilianzisha kitengo cha kushughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kutengeneza mpango mkakati wa mwaka 2009 – 2015 na hivi sasa tunatekeleza mpango mkakati wa mwaka 2016 – 2020. Mwongozo huu unatekelezwa kuanzia ngazi ya hospitali ya kanda hadi zahanati. Huduma za Magonjwa ya Kisukari, Shinikizo la Damu pamoja na Saratani ni huduma ambazo katika hatua za awali zinapatikana katika ngazi ya kituo cha afya. Mgonjwa anapokuwa na magonjwa haya ambayo yapo katika hatua ya juu, hulazimika kupatiwa huduma za matibabu ambazo zinapatikana Hospitali za Kanda, Taifa, Rufaa za Mikoa na Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeboresha huduma ya magonjwa ya moyo ikiwemo Shinikizo la Damu kwa kufungua Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Hospitali za Ocean Road, Bugando, KCMC, Benjamin Mkapa na ipo mbioni kufungua huduma za saratani katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya ili kupunguza mzigo kwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambayo kwa miaka mingi ni yenyewe pekee imekuwa ikitoa huduma kwa wagonjwa hao. Aidha, Serikali iko mbioni kuanzisha programu ya magonjwa yasiyoambukiza kama ilivyo kwa Programu za UKIMWI, TB na Malaria ili kufikisha huduma hizi katika ngazi ya zahanati na kuzipa mwonekano wa kipekee huduma za magonjwa haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, natoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanajikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kufanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki, kula mlo unaofaa, kutotumia tumbaku na bidhaa zake na kupunguza matumizi ya pombe.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Dalili za maji safi na salama kuchanganyika na maji chumvi (bahari) zinatishia ustawi. Je, nini utatuzi wa tishio hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa maji safi na salama kuchanganyika na maji chumvi bahari yanatishia ustawi wa jamii na kilimo. Hali hiyo inasababishwa na athari ya mabadiliko ya tabianchi, kutokana na kuongezeka kwa joto la dunia linalosababisha na kuyeyuka kwa barafu kwenye ncha za dunia na kwenye vilele vya milima mirefu. Kuyeyuka huko kwa barafu kunasababisha maji kutiririka kwenda baharini na kuongeza ujazo wa maji ya bahari na kusambaa katika maeneo ya mwambao ambayo yana shughuli muhimu za kijamii kama vile visima vya maji, kilimo na miundombinu muhimu ambayo huingiliwa na maji chumvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya sita ya jopo la watalaam inaonesha kuwa ujazo wa bahari umeongezeka kwa sentimita 19 katika miaka ya hivi karibuni na kusababisha mmomonyoko wa kingo za bahari na baadhi ya maeneo ya Pwani yameingiliwa na maji chumvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utatuzi wa kudumu wa suala hili unahitaji ushirikiano wa Kimataifa hususani katika kupunguza gesi joto ambazo huchangia ongezeko la joto duniani ambalo husababisha mabadiliko ya tabia nchi. Kwa kuwa suala la kupunguza gesi joto sio rahisi kufikiwa katika kipindi kifupi nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania zinahimiza kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuchimba visima vipya, kupanda miti ya mikoko katika maeneo ya kandokando ya bahari, kujenga kuta na makinga maji pale panapowezekana na kuhamasisha shughuli za kilimo kufanya katika maeneo mengine ambayo hayajaathirika. Sambamba na suala la kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi, nchi zinazozalisha gesi joto kwa wingi zinahimizwa kupunguza gesi joto ili kuzuia athari zaidi za mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
MHE. MWANTUM DAU HAJI aliuliza:-

Kasi ya mmomonyoko wa ardhi na uhaba wa udongo katika Visiwa vya Unguja na Pemba inatishia uhai wa Visiwa hivyo:-

Je, ni hatua zipi za makusudi zimechukuliwa katika kuvinusuru Visiwa hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba nichukue fursa hii sasa kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Visiwa vya Unguja na Pemba vina maeneo takribani 148 yaliyoathirika na mabadiliko ya tabianchi (Pemba 125 na Unguja 23). Athari hizi ni pamoja na mmomonyoko wa fukwe na kuingia kwa maji ya bahari katika mashamba na makazi ya watu. Ili kuvinusuru visiwa hivi dhidi ya athari ya mabadiliko ya tabianchi, Serikali imechukua hatua mbalimbali kupitia miradi inayofadhiliwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mradi wa kujenga uwezo wa jamii kuhimili athari ya mabadiliko ya tabianchi (LDCF) ambao umetekelezwa mwaka 2012 - 2018, shughuli zifuatazo zimefanyika: Ujenzi wa kuta mbili za mita 25 kila moja katika eneo la Kisiwa Panza - Pemba na ujenzi wa makinga bahari (gloynes) matano ya wastani wa urefu wa mita 100 kila moja katika eneo la urefu wa mita 538 Kilimani
– Unguja; upandaji mikoko Pemba maeneo ya Kisiwa Panza hekta 200, Tumbe hekta 10, Ukele hekta 7 na Tovuni hekta 1; na upandaji mikoko Unguja maeneo ya Kisakasaka hekta 8 na Kilimani hekta 1.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kupitia Mradi wa Kupunguza Uhalibifu wa Ardhi na Kuongeza Uzalishaji wa Chakula katika Maeneo Kame nchini mwaka (2017 - 2022), shughuli zifuatazo zinategemewa kufanyika katika maeneo ya Micheweni, Kata ya Micheweni na Kiuyu Maziwang’ombe ambazo ni: Kujenga makinga maji katika mashamba (dykes) ili kuzuia maji ya bahari kuingia katika mashamba; kutoa elimu kuhusu kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia mashamba darasa; upandaji wa miti ili kuhifadhi udongo na kutunza mazingira; na uanzishaji wa biashara ndogo ndogo ili kuwezesha jamii kuwa na shughuli mbadala za kujiongezea kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi; kudhibiti mmomonyoko wa udongo; na kukabiliana na uhaba wa udongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za ujenzi wa jengo jipya la kisasa la Askari Polisi wa Makunduchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa nyumba za makazi ya askari katika eneo la Makunduchi na katika Mkoa wote wa Kusini Unguja. Eneo la Makunduchi lina jengo moja la ghorofa la makazi ya familia nne za askari lililorithiwa toka Serikali ya Mkoloni na Mahanga mawili yanayotumiwa kwa makazi ya askari. Makazi haya ni sawa na asilimia 10 tu ya mahitaji halisi. Kwa kutambua changamoto hii, Serikali imeanzisha ujenzi wa nyumba za makazi ya familia 12 za askari polisi katika Mkoa wa Kusini Unguja. Aidha, Serikali kwa kupitia jeshi la polisi na kushirikiana na wadau imeanzisha ujenzi wa kituo cha polisi cha Daraja B huko Dunga, kituo hiki kimefikia hatua za mwisho kumalizika.