Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mwantum Dau Haji (17 total)

MHE. MWANTUMU D. HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri aliyoyasema Mheshimiwa Waziri, naomba niongeze swali langu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kuna Askari Polisi ambao kwa maksudi wanafumbia macho masuala ya biashara za madawa ya kulevya katika kuhakikisha mipango ya Serikali ya kudhibiti madawa ya kulevya inafikiwa. Je, kutakuwa na utaratibu gani wa kuwadhibiti Askari ambao hawaendi na kasi ya kupambana na biashara hiyo haramu ya madawa ya kulevya? (Makofi)
MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI - NAIBU WAZIRI, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Spika, labda niseme tu kutokuchukua hatua kuzuia uhalifu ni kosa la jinai kisheria. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge, Wabunge wote au mwananchi yeyote mwenye taarifa kuhusu Askari ambaye kwa maksudi kabisa hajatimiza wajibu wake, aviarifu vyombo husika na Askari huyo atachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri aliyonipatia, lakini naomba kuuliza swali langu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imejipanga vyema kwa ujenzi wa barabara hizo. Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua zaidi barabara hizo ili ajali zisitokee?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, upanuzi wa barabara unakwenda sambamba na bajeti. Nadhani Serikali ina mipango mizuri na imefanya kazi kubwa ya kuimarisha mitandao ya barabara nchini na sasa hivi nimesikia kuna mradi wa upanuzi wa barabara ambayo inatokea Dar es Salaam kupitia Chalinze na mbele zaidi. Kwa hiyo, ni mipango ambayo inaendelea kufanyika hatua kwa hatua kadri uwezo wa Serikali utakavyoruhusu.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza. Kupitia misaada mbalimbali ambayo Wizara inapokea kutoka kwa wafadhili, haoni kuwa, kuna haja hususan Hospitali ya Mnazi Mmoja, ya kuisaidia Wizara ya Afya ya Zanzibar kwa kuwapatia dawa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa hayo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mambo yaliyopo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano afya si mojawapo. Kwa maana hiyo sisi kama Wizara ya Afya hatuwajibiki moja kwa moja kushughulikia mambo yanayohusu afya kule Zanzibar. Hata hivyo, katika utaratibu na ushirikiano na umoja tulionao tunafanya kazi kwa karibu sana na wenzetu pacha Wizara ya Afya ya kule Zanzibar na hivyo ushirikiano huu tutaendelea kuudumisha.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na namshukuru Waziri kwa masuala yake mazuri aliyonipatia, lakini napenda kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni hatua gani zinachukuliwa kwa wale askari ambao watabainika kuchukua rushwa kwa madereva ambao wametenda makosa?
Na je, madereva wanaojaza abiria kwenye magari kuliko level seat, hawa wanachukuliwa hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ambazo askari wanachukuliwa wanapobainika wanajihusisha na vitendo vya rushwa ni kufukuzwa kazi mara moja. Lakini pamoja na kufukuzwa kazi, pia kushitakiwa.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi kwa kuniona. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni, kuna baadhi ya nyimbo zinazoimbwa katika ma-stage show au zinazooneshwa katika runinga. Nyimbo hizi huwa zinatudhalilisha wanawake kuvaa yale mavazi yao ambayo yanaonesha, je, Serikali inazingatia suala hili au kisheria ni sawa kuimba nyimbo kama zile zinazotudhalilisha sisi wanawake?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kuhusiana na nyimbo ambazo zinadhalilisha wanawake ni swali jipya naomba alilete vizuri ili kusudi tuweze kulijibu vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyo vyombo ambavyo vinasimamia kwa kupitia sheria zetu. Tuna Bodi ya Filamu ambayo huwa inaangalia, inapitia maudhui yenyewe kama ni ya filamu au wimbo, lakini pia tuna Kamati ya Maudhui ambayo ipo chini ya TCRA. Kwa hiyo, kwa kutumia sheria zetu tunadhibiti hali kama hii. Vilevile wale ambao wanaona kwamba hali hairidhishi, tunaomba wawasilishe ni wimbo upi au ni filamu ipi ili kusudi hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
MHE. MWANTUMU D. HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri aliyoyajibu na naona yametosheleza hasa na wananchi huko watasikia jinsi walivyojipanga. Nina swali langu moja dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itakamilisha mradi huu na kuondoa msongamano wa daladala ambazo nyingine ni za kizamani kabisa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Mheshimiwa Mwantumu Dau, kwa sababu yeye ni Mjumbe wa Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana mpaka kuanza kwa mradi huu.
Naomba niwahakikishie wakazi wa Dar es Salaam kwamba mradi huu awamu ya kwanza umekamilika na sasa tunajiandaa katika mradi wa awamu ya pili kuanzia Mbagala na mradi wa awamu ya tatu kuanzia Gongo la Mboto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmesikia Mheshimiwa Rais wakati anazindua fly over za Ubungo pale, kwamba fedha zimeshapatikana na muda wowote sasa kazi hii inaweza ikaanza. Lengo kubwa ni kuondoa foleni kabisa na kuondoa haya magari madogo katika Jiji la Dar es Salaam na Serikali kuwahudumia wananchi na kukuza uchumi wake. (Makofi)
MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo ameyatoa hapa hivi sasa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza nataka kuuliza. Je, Serikali inasema nini katika kuboresha kilimo cha umwagiliaji maji kwa kupitia mito mikubwa, maziwa na mabwawa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na kilimo cha umwagiliaji maji, je Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wakulima juu ya kilimo hicho. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumejibu kwenye swali letu la msingi ambapo Serikali imeweka mipango mikakati ya kuhakikisha kwamba kilimo cha umwagiliaji na hasa pale ambapo tunakuwa na matatizo ya ukame; matatizo ambayo yanasababisha mvua zisijulikane sana. Ndio maana mipango ambayo nimeisema katika majibu yangu ya msingi, inabidi izingatiwe.
Mheshimiwa Spika, vilevile wakulima wanashauriwa katika kilimo hiki cha kutumia maji vizuri, kikiwemo na kilimo hiki ambacho tunaita drip irrigation. Kilimo ambacho kinatumia matone ya maji na hivyo kuweza kuwa na maji mengi kwa ajili ya watumiaji wengine.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la pili ambalo ni la elimu kwa wakulima. Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la NEMC tumekuwa na mikakati mbalimbali ya kuwapa wakulima elimu. Vilevile kwenye Sikukuu ya Wakulima ya Nane Nane tumekuwa tukichapisha majarida mbalimbali; majarida mengine ambayo ninayo hapa ambayo baada ya hapa nitampatia Mheshimiwa Mbunge. Wadau mbalimbali na wakulima wamekuwa wakitembelea mabanda yetu na kupata vipeperushi pamoja na majarida mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia mikakati ambayo tumeizungumzia hapa, nitampatia Mheshimiwa Mbunge kuna hii ya National Climate Change Strategy ambayo tumeizungumzia ya mwaka 2012 halafu vilevile tunayo miongozo ambayo ni ya kisera kuhusiana na suala la sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, niseme pia kwa faida ya Watanzania wote, masuala ya mazingira ambayo yanaathiri kilimo yameanzia kwenye Biblia ukisoma Mwanzo 10:15 ambapo Mungu alianzisha utaratibu kwenye ile mito minne akamwambia mwanadamu nakuagiza ukalime na kuitunza.
Mheshimiwa Spika, hivyo, vyanzo vya maji ni asili yake kwenye Biblia. Hii ndio maana na sisi kwa kutunga Sheria hii namba 20 ya 2004, vilevile tumechukua kipengele hicho tukaweka kifungu cha sita (6) ambacho kinatoa wajibu wa kisheria kwa kila mtanzania kutunza na kuhifadhi mazingira.
Mheshimiwa Spika, Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri naomba kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi, wanaendelea kunyanyasika katika maeneo hayo, je, Serikali ina mpango gani wa kutoa muda maalum kwa kumaliza mgogoro huo wa kitaifa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumekuwa tukitoa majibu kwa muda mrefu kwamba sasa hivi tunayapitia matatizo na changamoto zote zilizopo katika hifadhi zetu, ikiwa nia pamoja na maeneo yale yanayosimamiwa na jumuiya za wananchi, naamini kabisa kwamba baada ya muda mfupi na baada ya Serikali na wadau wengine kukaa kwa pamoja tutaleta ufumbuzi wa suala hili na haya matatizo yatapungua kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
MHE. MWAMTUMU D. HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kwa kuniona. Kwa kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kwenye suala la ubakaji, je, Serikali imejipanga vipi kuhusu suala hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikihakikisha ulinzi kwa watu wenye ulemavu kila iitwapo leo. Kwa hiyo, niseme kwamba hata hili la ubakwaji kwa watoto wenye ulemavu Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba inawapatia ulinzi. Hata hivyo si hilo tu, mtu ambaye atabainika kwamba amefanya kitendo hicho kwa mtu mwenye ulemavu atachukuliwa hatua kali na hatua stahiki kama inavyostahili ahsante.
MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana na yenye msingi, nampongeza sana. Hata hivyo, nina maswali yangu mawili ya nyongeza hapa. Swali la kwanza, kwa kuwa ubakaji umekithiri hapa nchini na hasa wanaume ndio chanzo kikuu cha masuala hayo; je, Serikali itachukua hatua gani za kimkakati ili wananchi watokwe na hofu na suala hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali ina mpango gani wa kutunga sheria kali ili kudhibiti ubakaji na udhalilishaji? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeeleza mikakati ambayo Serikali inaifanya kuhakikisha kwamba tunapunguza sana matukio haya ya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto na mikakati naomba niirudie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni kuuhakikisha kwamba mpango mkakati ule ambao tumeuandaa tunausimamia vizuri; Pili, tumeendelea kushirikiana na vyombo vya dola na kuanzisha madawati mbalimbali; Tatu, kuanzisha one stop centre; Nne, ni kutoa elimu kwenye jamii. Tunatambua kwamba matukio mengi ya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto yanafanya karibu sana na wanafamilia. Niendelee kutoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba tusifumbie macho matukio kama haya na tusimalizane nayo katika ngazi ya familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, linahusiana na kwa nini tusitunge sheria kali; sheria tulizokuwa nazo za mwenendo wa adhabu na Sheria ya Mtoto na Sheria ya Masuala ya Kujamiiana zinajitosheleza kabisa na hatua zilizokuwepo pale zinatosha kabisa kuchukua hatua kwa wale wote ambao wanafanya matukio kama haya.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri aliyoyatoa hivi sasa. Kwa kuwa hakuna ucheleweshwaji wa mishahara, napenda kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Serikali inasema nini kuhusu uongezaji wa mishahara kwa watumishi hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali inasema nini kuhusu upandishaji wa madaraja mbalimbali kwa watumishi wa umma?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameuliza Serikali inasema nini kuhusu uwekezaji wa mishahara ya wafanyakazi. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mshahara ni mali halali ya mfanyakazi mwenyewe hivyo kuhusu uwekezaji ni mfanyakazi mwenyewe anaamua mshahara wake nini aufanyie, akitaka kuuwekeza wote yuko huru kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu upandishwaji wa madaraja, Serikali yetu siku zote imekuwa ikiwatendea haki wafanyakazi wetu kwenye upandishaji wa madaraja na kila mwaka wafanyakazi hupandishwa madaraja.
MHE. MWATUM DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri aliyoyatoa yenye kila aina ya vinjonjo. Napenda kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa programu hizi katika sekta ya kilimo linahusiana na suala la kuhimili mabadiliko ya tabianchi; je, Serikali ina mkakati gani kutoa elimu kwa wakulima ili waende sambamba na mabadiliko ya tabianchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Mwatum ambaye amekuwa akifuatilia sana masuala ya mazingira na hasa mambo haya ya mabadiliko ya tabianchi. Namhakikishia kwamba pamoja na mipango hii ambayo Serikali tumekuwa tukiifanya, hata kule Unguja na Pemba tunashirikiana na Taasisi za Kimataifa USAID pamoja na FAO katika miradi ya kilimo ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kutoa elimu, nimhakikishie Mheshimiwa Mwantum tayari mpaka sasa Serikali ilishatoa mwongozo pamoja na mafunzo kwa watu wapatao 192 wakiwemo Maafisa Kilimo, Maafisa Uvuvi, Maafisa Mifugo pamoja na Maafisa Mipango kutoka kwenye Halmashauri za Wilaya na kuwaelekeza kwamba katika mipango wanayoipanga Wilayani pamoja na bajeti waweze kushirikisha mipango hiyo ya kilimo himilivu cha mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, elimu hii tayari tulishaipeleka kwa wananchi na bado tunaendelea katika mpango huu tuliosema endelevu wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi, ni element ambayo pia inahusishwa. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais alizindua juzi hapa ASDP II, vilevile kuna element ya kutoa mafunzo ya kilimo himilivu kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
MHE. MWATUM DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa jibu lake zuri ambalo alilolitoa hapo, lakini naomba kuuliza swali la langu la nyongeza. Tunaelewa kuwa Serikali inawajibika vilivyo katika kushughulikia na kutatua matatizo hayo. Je, ni lini hasa Serikali itafikia ukomo wa suala hili kwa kuwa imekuwa ni kero kubwa kwa Askari wetu, kwani kufanyiwa hivyo pia kunawanyima haki zao na vilevile itawapelekea kutokufanya kazi kwa ufanisi na uadilifu? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ni kwamba Maofisa, Wakaguzi pamoja na Askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Polisi na hata vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vilivyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mishahara yao inaendelea kurekebishwa. Hata hivyo, pale ambapo kutorekebishwa kwa mshahara kwa askari yeyote kutatokana na uzembe wa makusudi kwa Afisa ambaye anashughulika na mishahara ya Askari nimeshatoa maelekezo kwamba ifikapo mwezi wa Tano mwaka huu asiwepo Askari, wala Afisa wala Mkaguzi anayelalamikia stahiki yake. Pia nimewaelekeza kwamba wasicheze na maslahi na stahiki za Askari. Kufanya hivyo ni sawa na kushika mboni ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, suala alilosema Naibu Waziri ni suala zuri sana wala halina mjadala, lakini sasa Serikali haioni ni wakati sasa wa kufanya matibabu yakawa bure nchini hasa kwa wale waliokuwa hawana bima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Waziri ametoa rai kwamba watu waende kwenye mazoezi, kuhusu suala la mlo na mambo mengine, ni kweli lakini napenda kuishauri Serikali, je, ni kwa nini haitoi elimu kwa jamii namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukizika hasa haya ya pressure, sukari na shinikizo la damu? Ahsante.

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Je, Serikali haioni sasa kuwaondolea matibabu yakawa bure nchini hasa kwa wale wasio na bima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili, Mheshimiwa Waziri ametoa rahi hapa kwamba watu waende kwenye mazoezi, kuhusu suala la mlo na mambo mengine, ni kweli lakini napenda kuishauri Serikali. Serikali haitoi elimu kwa jamii namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa hasa haya ya pressure, sukari na shinikizo la damu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwantumu Dau kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nianze kumpa tu maelezo ya awali kuhusiana na swali lake la kwanza ambalo ameliongelea. Magonjwa haya yasiyoambukizwa ni magonjwa ambayo yana gharama sana na ni magonjwa ya kudumu. Naomba nitoe mfano, mgonjwa wa tatizo la figo ili kusafisha damu kwa wiki anahitaji kati ya laki saba na nusu mpaka milioni moja; na upandikizaji wa figo kwa sasa nchini tunafanya kwa takribani milioni 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mgonjwa wa kisukari anahitaji kati ya shilingi 50,000 mpaka 100,000 kutokana na idadi ya dawa; vivyo hivyo kwa mgonjwa ambaye ana shinikizo la damu. Kwa hiyo tumekuwa tunaona ongezeko kubwa sana na ndiyo maana utaona kwamba sisi kama Serikali tumeweka msisitizo mkubwa sana na tunataka kuanzisha program ya kitaifa; lengo ni kuanza kupambana kwasababu mwanzoni tulikuwa tunapambana na magonjwa ya kuambukiza. Unapomtibu malaria mtu leo hatorudi tena katika kituo chetu cha huduma za afya labda baada ya mwaka mmoja. Lakini mgonjwa ambaye anatatizo la kisukari, pressure na saratani, huyu anaingia katika mfumo wetu wa kudumu wa kupata huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo gharama za matibabu haya ni kubwa, na sisi kama Serikali ili kutoa nafuu kwa wananchi ndiyo sasa tunataka tuelekee katika mfumo wa bima ya wananchi wote na mwezi Septemba tunataka tulete Muswada huo ambao utaweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba kila mwananchi anakuwa na bima ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika kipindi hiki cha awali msisitizo mkubwa ambao tunaendelea nao ni kutoa elimu. Tunatoa elimu kupitia Wizara, na ndiyo maana tuliona hata tumepiga marufuku matumizi ya tv zetu katika vituo vya afya ili viweze kutoa elimu kwa umma. Tunaongea na wenzetu wa SUMATRA ili hata katika vyombo vya usafiri elimu ya afya kwa umma.

Mheshimiwa Mwneyekiti, na mimi niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, magonjwa haya ya kuambukiza yanazidi kukua; nitoe rai ya kuhakikisha kwamba tunatunza afya zetu na kutunza afya zetu ni kuhakikisha kwamba tunakula mlo sahihi tunafanya mazoezi na tuhakikishe kwamba tunakuwa na matumizi ya wastani ya vileo ikiwa ni pamoja na pombe na sigara.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mazingira kwa suala lake zuri ambalo alilolitoa hivi sasa hivi hapa. Lakini pia nimpongeze kwa suala langu la Bunge lililopita wakaja Zanzibar wakaja kutuhimiza ahadi yake ya kuja kuangalia mambo ya hali ya hewa ya mmomonyoko wa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza, kwa kuwa mikoko ina mchango mkubwa wa kunusuru mazingira nini mpango wa Serikali katika kuhakikisha inaotesha mikoko ambayo inauwezo wa kunusuru maji chumvi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili bila maji baridi hatima ya kilimo na uhai wa binadamu viko hatarini. Je, kuna tafiti zozote za kuyalinda kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji baridi ahsante? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ridhaa yako nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji Mbunge wa Viti Maalum ni kweli amekuwa mstari wa mbele na sasa hivi amekuwa mwana mazingira tunamtumia sana hasa kwenye eneo hili la Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru kwa maswali yake mawili; moja, tunao mkakati maalum na unaendelea kwa kushirikisha wenzetu wa Serikali za Mitaa hasa kwenye halmashauri zetu kuhakikisha wanaweka miche kwa ajili ya mikoko ambayo itatumiwa kwenye maeneo hayo tuliyoyaeleza ya Pwani pembezoni mwa bahari. Na mkakati huo unaendelea na miche ipo ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili, utafiti zinaendelea na mpaka sasa tupo na utafiti unaendelea na wakati wowote tutaweka suala hili katika utaratibu ambao tutahakikisha maeneo haya kunakuwepo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwenye kila eneo ambalo kuna mwambao wa bahari ahsante sana.
MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu ya kina kuhusu swali langu hili, nampongeza sana, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, yamekuwepo matukio ya ongezeko la kina cha bahari kiasi cha kuwepo kwa tishio la kimazingira katika baadhi ya maeneo. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na suala hilo katika Visiwa vya Unguja na Pemba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tatizo hili ni la muda mrefu kweli, toka lilivyogundulika kuhusu mazingira katika Visiwa vyetu vya Pemba na Unguja. Mheshimiwa Naibu Waziri atakuja lini sasa Zanzibar kuangalia maeneo yaliyoathirika katika Visiwa vya Pemba na Unguja? Nataka unihakikishie utakuja lini Zanzibar mbele ya Bunge letu hili.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mwantum Dau Haji kwani amekuwa mdau mzuri wa eneo hili la mazingira. Nimhakikishie tu kwamba katika miradi ambayo inaendelea na kama nilivyosema kwamba tunashirikiana vizuri na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sasa tunaifanyia tathmini. Katika tathmini ile ambayo tunaifanya kila baada ya miezi mitatu maana yake sasa nitakuja rasmi baada ya Bunge hili, walau siku mbili hivi kwa ridhaa ya Mwenyekiti, ili tukishirikiana nawe na Wabunge wengine kwenye maeneo ya Pemba kuyaona hayo maeneo vizuri na kuhakikisha tunayapatia ufumbuzi wa kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na yenye tija ndani yake na pia nakiri kwamba katika kituo cha Dunga ni kweli tayari hili jengo liko katika kukamilisha mwisho wake kuwa zuri sana na lifanye kazi. Niseme maswali yangu mawili ya nyongeza, kwa kuwa jengo la Makunduchi la muda mrefu na mwaka 2015 waliamua polisi kuweka foundation pale ili wapate kituo chao cha uhakika, je sasa swali langu liko hapa; Serikali itamaliza ujenzi huu lini? Swali langu la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwamba eneo la Makunduchi ni eneo la utalii. Kila mwaka kule Makunduchi kunakuwa kunafanywa Mwaka Kogwa, na ukizingatia hata mwaka jana Mheshimiwa Waziri wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa yeye ndiyo mgeni rasmi alikwenda kule. Swali langu lipo hapa, Serikali ina mpango gani wa kuweka ulinzi katika eneo lile hasa sambamba na ujenzi wa vituo vya polisi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na swali lake la kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika maeneo ambayo tunayaangalia kwa karibu pale ambapo bajeti itakapokaa vizuri tuweze kumaliza ni hilo jengo ambalo amelizungumza la kituo cha polisi Makunduchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuimarisha ulinzi hasa ukizingatia eneo la Makunduchi ni sekta ya utalii, nimhakikishie kwamba sasa hivi tunavyozungumza tuna mkakati kabambe wa kuimarisha usalama katika maeneo hususan Ukanda wa Pwani wa Zanzibar maeneo ambayo yamekuwa yanatumika kiutalii ili tuweze kuongeza imani ya watalii na wawekezaji katika ukanda huo. Kwa hiyo, tutakapokamilisha mkakati huo, sehemu ya Makunduchi ni moja katika maeneo ambayo yatafaidika.