Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Mashimba Mashauri Ndaki (2 total)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kipekee zaidi namshukuru Mungu kwa fursa hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la msingi nimeuliza sehemu ya Serikali kama ruzuku. Nikiri kwamba nimepokea majibu ya Serikali, lakini naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubaliana na mimi kwamba kuku wa kienyeji ndio mradi wa chini kabisa wa mwananchi yeyote kumudu Tanzania. Kila kaya ingepata kuku wa kienyeji tungeboresha hata chakula chetu sisi wenyewe na pia miradi kwa akinamama. Nimeambiwa hapa kwamba bei ya ruzuku ni shilingi 1,400/= na shilingi 1,500/= naomba niseme kwamba hiyo ndio bei ya kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Serikali kama Serikali inatoa ruzuku gani ili kila kaya ipatiwe vifaranga hivi vya kienyeji ambavyo pia Serikali inatakiwa kutoa elimu, vifaa vya kulishia kuku hawa, vyakula vya kulishia ikiwemo starter, growers na pia dawa za kuku hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa swali hili nimekuwa nikiliuliza kwa awamu zote na sasa ni mara ya tatu niko Bungeni na jibu linajibu kwamba wako wanafanya utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka 15 ya utafiti kwa nchi ambayo ina Chuo cha Kilimo na Mifugo kama ilivyo SUA ni jambo ambalo halikubaliki. Swali, ni lini sasa Serikali itawezesha Wabunge wote Viti Maalum wakafanye miradi hii ya kuku wa kufuga kwenye mikoa yao? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, lakini pia, nichukue nafasi hii kumshukuru sana mama yangu Mama Raymond kwa swali lake hili ambalo ameendelea kuliuliza kila wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza kwamba Serikali inatoa ruzuku gani, ili bei ya vifaranga hao tunaowauza angalao iwe chini kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba hiyo bei ya shilingi 1,400/= na shilingi 1,500/= kuna ruzuku ndani yake, kwa sababu bei ya kifaranga ni shilingi 2,200. Sasa badala ya kuuzwa shilingi 2,200 Serikali kwa kushirikiana na kampuni nilizozitaja wanatoa ruzuku ili kwamba wahitaji wa vifaranga hawa wawapate kwa bei ya shilingi 1,400 na shilingi 1,500. Kwa hiyo, ni kwamba Serikali pamoja na wadau wake tunatoa ruzuku. Sasa kama bei ya shilingi 1,400 na shilingi 1,500 bado ni kubwa, hilo linaweza kuwa ni suala lingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la pili kama ulivyoelekeza, basi tutaona ni kwa namna gani Wabunge wa Viti Maalum tuwapeleke Naliendele mahali ambapo tunafanya utafiti, ili waelezwe kitaalamu utafiti huo unachukua muda gani na kwamba utaisaidia nchi hii baada ya muda gani. Nadhani itakuwa ni suala la msingi sana, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wakati anajibu swali la msingi nilitaka tu nimkumbushe kwamba nimeuliza swali hili mwaka juzi nikiwa humu ndani ya Bunge na Serikali ilijibu kwamba itafanyia kazi, sasa amekuja na majibu mengine kwamba ataangalia.

Je, sasa yuko tayari kuingiza Halmashauri ya Itigi ambayo ina wafugaji wengi ambao ni wapya na wameingia maeneo ambayo tunayo kwa sababu ya fursa ya malisho kuingiza kwenye suala zima la malambo ili wapate sehemu ya kunyweshea mifugo yao?

Lakini lini Mheshimiwa Waziri upo tayari kuambatana na mimi kwenda kujionea uhalisia wa wafugaji walivyo wengi katika Jimbo hili la Manyoni Magharibi, kwa maana ya Halmashauri ya Itigi angalau katika mnada mmoja tu wa Mitundu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Massare, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Itigi inavyotunza wafugaji walioko kwenye Wilaya hiyo, tunalazimika sisi, kama Wizara kujali sasa kwenye bajeti ijayo na kutekeleza suala la kujenga lambo kwenye Wilaya yake ya Halmashauri ya Itigi. (Makofi)

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lambo ambalo tumesema tutaangalia kwenye bajeti, kimsingi tutachimba lambo kwenye halmashauri yako kwa sababu, tunaelewa una wafugaji wengi na mifugo ni wengi kwenye wilaya yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya suala lake la pili la mimi kwenda kwenye halmashauri yake na jimbo lake, ili kwenda kujionea hali halisi, niko tayari nitafanya hivyo ili tuweze kuona hali halisi na kwa pamoja tuweze kutathmini na kuona ni kitu gai tunaweza kuwasaidia wafugaji wetu walioko Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Itigi. (Makofi)