Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi (3 total)

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante Sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali la nyongeza. Daraja lililopo Jimbo la Moshi Vijijini lilisombwa na maji mwaka mmoja uliopita na daraja hili ni muhimu, linaunganisha kata nne katika Jimbo la Moshi Vijijini. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa daraja hili? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua maeneo yote korofi ambayo madaraja yetu kwa namna moja ama nyingine yameathirika na mafuriko kutokana na mvua ambazo zimeendelea kunyesha hapa nchini. Serikali imeweka mkakati wa kwenda kufanya tathmini ya mahitaji katika maeneo hayo korofi ili kulingana na upatikanaji wa fedha, fedha ziweze kutengwa na madaraja hayo yaweze kujengwa au kufanyiwa marekebisho ili kuwezesha wananchi kupata huduma kama Serikali inavyodhamiria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Moshi Vijijini kwamba eneo hilo Serikali inalitambua na tutakwenda kadri ya upatikanaji wa fedha kutenga bajeti kwa ajili ya usanifu, lakini pia kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo ili tuweze kurahisisha shughuli kwa wananchi.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina swali la nyongeza ambalo lina vipengele viwili.

Mheshimiwa Spika, kwanza, katika Kata ya Uru Shimbwe kuna shida kubwa sana ya huduma ya mawasiliano ya Radio hasa kwa Redio yetu ya Tanzania na Television yetu ya Taifa. Pili, kuna shida ya huduma ya internet na imesababisha Kata ya Uru Shimbwe ishindwe kutuma taarifa kupitia kwenye zahanati yetu kwenye Shirika la Bima la Afya. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba huduma hizi zinaboreshwa kwenye eneo la Uru Shimbwe?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Patrick Alois Ndakidemi Mbunge wa Moshi Vijijini kwa sababu masuala haya tumekuwa tukiwasiliana na jiografia ya eneo husika tayari ameshanieleza jinsi ilivyo. Hata hivyo, kupitia mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma za mawasiliano vijijini zikiambatana na usikivu wa redio katika maeneo husika tayari Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeshaanza kufanya tathmini katika maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, vilevile katika eneo ambalo ameongelea kuhusu upatikanaji wa data, Serikali tayari imeshatoa maelekezo kwa watoa huduma wote, sehemu yoyote ambapo tutapeleka mradi wowote ule, lazima mradi huo ukajengwe wa kutoa huduma ya kuanzia 3G maana yake ni kwamba, ni lazima sasa Tanzania tutakuwa na miradi au minara ambayo itakuwa inatoa huduma ya internet. Nasema hivyo kwa sababu hapo kabla tulikuwa tunaangalia tu angalau kila Mtanzania aweze kupata mawasiliano, lakini kwa sasa tunalazimika kwa sababu ya mahitaji ya kuelekea kwenye digital transformation maana yake kwamba mahitaji ya internet ni makubwa zaidi ikiambata na eneo la Mheshimiwa Patrick, Moshi Vijijjini. Nashukuru.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini niseme ukweli kwamba mikopo inayotolewa ni mikopo na si zawadi. Sasa kuna kitu ambacho kimejitokeza kwamba watu wanaosoma shule binafsi au watoto wa watumishi wa Serikali hawapati mikopo huo ndio ukweli tusiseme uongo.

Je, wako tayari kama itajirudia tena hiyo kitu walete sheria Bungeni ibadilishwe ili itamke wazi kwamba watakaopewa mikopo ni watu waliosoma Serikalini na sio waliosoma kwenye shule za watu binafsi au watoto wa watumishi wa Serikali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwa Naibu Spika, ahsante na napenda kujibu swali dogo la Mheshimiwa Ndakidemi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi mikopo hii inaratibiwa kwa ile Sheria Namba 178 ya Bodi ya Mikopo ambayo imebainisha vigezo na vielelezo vya mwanafunzi gani na mwenye sifa zipi wa kupata mikopo hiyo na ambayo haibainishi kwamba amesoma shule gani na alikuwa analipa ada gani katika hizo shule za nyuma zilizopita. Lakini kwa vile yeye Mheshimiwa Mbunge amelieleza jambo hili hapa, tunalichukua tunakwenda kulifanyia kazi na kama kulikuwa na mchezo fulani ambao unachezwa nimwahidi tu kwamba katika kipindi hautatokea na mikopo hii itawafikia wote wenye uhitaji wa kupata mikopo hii.