Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. George Natany Malima (2 total)

MHE. GEORGE N. MALIMA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kuanzia Njia Panda ya Kongwa hadi Mpwapwa Mjini yenye urefu wa takribani kilometa 30 ambayo ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ya Njia Panda ya Kongwa hadi Mpwapwa ulianza kutekelezwa kwa kujengwa kwa kiwango cha lami kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014. Ujenzi huu ulianza baada ya kukamilika kwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka 2013 uliohusisha barabara ya Mbande – Kongwa Junction. Kongwa Junction – Ugogoni kilometa 17.5, Kongwa Junction – Mpwapwa – Ving’awe kilometa 38.85 na Mpwapwa – Gulwe – Kibakwe kilometa 46.93.

Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, ujenzi kwa kiwango cha lami ulianza, ambapo hadi sasa ujenzi wa sehemu ya Barabara ya Mbande – Kongwa Junction kilometa 16.7 umekamilika. Serikali kwa sasa inaendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Njia Panda ya Kongwa hadi Mpwapwa. Katika mwaka wa fedha huu tunaondelea nao Serikali imetenga shilingi bilioni 4.95 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami katika mji wa Mpwapwa. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Njiapanda ya Kongwa hadi Mpwapwa utaendelea kutekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeendelea kutenga fedha za matengenezo mbalimbali ya barabara hizi ili ziendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka huu wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi bilioni 1.1 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Pandambili – Saguta – Mpwapwa – Ng’ambi na shilingi milioni 751.596 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Manchali – Ng’ambi – Kongwa Junction – Hogolo Junction ambapo barabara ya Njiapanda ya Kongwa hadi Mpwapwa imezingatiwa. Ahsante.
MHE. GEORGE N. MALIMA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo la muda mrefu la uhaba wa maji kwa wananchi wa Mji wa Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua tatizo la muda mrefu la uhaba wa maji katika mji wa Mpwapwa. Katika kutatua tatizo hilo, mikakati ya muda mfupi na muda mrefu imekuwa ikitekelezwa. Kwa upande wa mikakati ya muda mfupi, mwaka 2020/2021 Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuchimba visima virefu viwili katika eneo la Kikombo. Ujenzi wa bomba kuu kutoka katika visima hivyo viwili mpaka katika tanki la Vingh’awe, kuongeza mtandao wa maji katika maeneo ya pembezoni ambayo ni Vijiji vya Vingh’awe na Behero. Aidha, kazi nyingine itakayofanyika ni kufunga pampu mpya kwenye kisima cha Kikombo ambacho kitaongeza uzalishaji wa maji katika kisima hicho kutoka lita 40,000 kwa saa hadi lita 65,000 kwa saa. Kukamilika kwa kazi hizi kutaboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika mji wa Mpwapwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Mpwapwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji ya Dodoma (DUWASA) inaendelea kufanya usanifu unaotarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2021 na kubainisha maeneo ambayo yana upungufu mkubwa wa maji katika Mji wa Mpwapwa ambapo vitachimbwa visima virefu vinne na kuongeza mtandao wa mabomba katika Mji wa Mpwapwa na viunga vyake. Aidha, katika mwaka 2021/2022, Serikali itakarabati mradi wa maji wa mtiririko wa Mayawile na Kwamdyanga.