Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. George Natany Malima (2 total)

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni adhma ya Serikali kuunganisha miji yote ya mikoa na wilaya kwa barabara za lami; na kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii kiuchumi kwa wananchi wa Mpwapwa, je, Serikali ipo tayari kuipa kipaumbele maalum barabara hii ili ikamilike mapema?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii ni muhimu na ndiyo maana hata hapa tunapoongea yeye atakuwa ni shahidi kwamba mkandarasi yuko site akiwa anajenga hizo kilometa 5. Naamini katika bajeti ijayo tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza hiyo barabara.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa tatizo la maji katika Mji wa Mpwapwa limekuwa la muda mrefu. Na kwa kuwa, Serikali imekiri kwamba, ni kweli limekuwa la muda mrefu na kwamba, wana mpango wa kuchimba visima viwili katika eneo la Kikombo ili kuongeza upatikanaji wa maji katika mji ule.

Je, ni lini uchimbaji huu wa visima hivi viwili utakamilika ili watu wa Mpwapwa nao wapate unafuu wa shida ya maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mwezi Januari timu kutoka Wizara ya Maji ilikuja kutembelea katika Jimbo langu, tulikagua miradi miwili ya maji mmoja katika Kijiji cha Vingh’awe na mmoja katika Kijiji cha Manhangu; na mradi ule wa Vingh’awe ulitengenezwa siku nyingi, lakini historia iliyopo ni kwamba ulipochimbwa miundombinu ilijengwa chini ya kiwango; ulifanya kazi siku tatu tu mabomba yalipasuka, lakini tenki ambalo lilijengwa below standard pia nalo lilibuja lote halafu ule mradi ulikufa, lakini mradi wa Manhangu pia una story inayofanana.

Je, Serikali inasemaje kuhusu hili, maana walikuja kukagua na wakaahidi kwamba wataifanyia matengenezo ili ifanye kazi. Je, ni lini watakuja kurekebisha hiyo miradi miwili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika,ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa George Malima, Mbunge wa Mpwapwa kama ifuatavyo:-

Swali lake la kwanza ni lini mradi ule unakwenda pesa zitapelekwa ili mradi uendelee kutekelezwa. Jibu lake kwa sababu mradi uko ndani ya mwaka wa fedha huu 2020/2021 Mheshimiwa Mbunge nakuhakikishia kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha kwa maana ya mwezi Juni hii fedha itakuwa imefika na tutasimamia utekelezaji wake kwa karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ameongelea kuwa mwezi Januari kuna timu kutoka Wizarani ilikwenda na ni kweli. Miradi hii anayoiongelea ya Vingh’wale pamoja na Manhangu kwa pale Mpwapwa ni kati ya miradi ya ule mpango wa vijiji kumi ambao Wizara imekuwa ikiifanyia kazi na vijiji hivi kwa hakika vilikuwa na changamoto kubwa sana ya maji, lakini kwa awamu hii sisi tumejipanga kuhakikisha kuona kwamba miradi ile kwenye ile programu ya vijiji kumi tunakwenda kuisimamia ambayo ina vijiji takribani 177 vyote tunakwenda kuhakikisha tunarekebisha pale ambapo kidogo palikuwa na mapungufu. Lakini vilevile tutahakikisha wananchi wetu wanakwenda kupata maji safi na salama na ya kutosheleza.