Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Edward Olelekaita Kisau (3 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii, lakini kabla ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunipa afya hii njema hadi leo niko Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kiteto kwa imani kubwa na wamenichagua kwa kura nyingi sana. Nawaahidi kabisa kwamba nitawajengea heshima kubwa hapa Bungeni haijawahi kutokea. Vilevile nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuniteua na nikapeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze kutoa maoni yangu kwa Mpango huu wa Maendeleo. Mpango wa Maendeleo ni mzuri sana na kwa kweli katika kupitia zipo taarifa kama tatu hivi ambazo ni kubwa kweli. Kwa hiyo, maoni yangu ya kwanza nafikiri kama hatutayatendea haki sana mapendekezo haya kwa siku zilizopangwa kama nne hivi. Document ya kwanza ina kurasa karibu 164; ya pili 51; nyingine 107. Sasa ukichanganya zote na dakika tano hizi utajua kabisa kwamba pengine tungehitaji wiki mbili hivi za namna ya kuzungumza ili tuweze kuishauri Serikali vizuri sana katika mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda kuwa mchache, nijielekeze kwenye kilimo. Kilimo hapa tumeambiwa kwamba pato la Taifa ni 27% na kinawaajiri Watanzania zaidi ya 65%. Nimshukuru sana Rais kwamba mapendekezo ya maendeleo mwaka huu ni kuwekeza nguvu kwenye kilimo. Tukiwekeza nguvu kwenye kilimo na hususan mbegu zipatikane kwa wakati na kuwaondoa wakulima kwenye jembe la mkono na ku-mechanize, tutaweza kulikwamua Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahusiano katika kuendeleza kilimo siyo tu yana tija kwenye uchumi, lakini vilevile na mahusiano makubwa sana ya kupunguza umaskini kwa Watanzania walio wengi. Kwa hivyo kwa kweli naomba Wizara ya Kilimo isilale katika hii miaka mitano, tuwekeze nguvu kubwa sana kwenye kilimo na kwenye mbegu, unajua nchi zile zilizoendelea sasa wana-patent hizi mbegu, kwa hiyo tusiwekeze tu kwenye kufanya utafiti, lakini pia tu-patent mbegu zetu ili tuweze kulinda masoko yetu huko mbele ya safari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwekeza kwenye kilimo, kwenye mifugo, kwenye uvuvi na tukaweka nguvu zetu zote huko tutakuwa tumeshughulika na vitu wanavyoita watu wengine the really economies kwa sababu ndiyo Watanzania wengi wako huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni umeme na ningemwomba sana Waziri wa Nishati anisikilize vizuri hapa, Hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa nane na nimeshamwandikia Mheshimiwa Waziri memo nyingi sana kuhusu suala la umeme. Nafurahi sana tumewekeza kwenye umeme na nawapongeza sana na Wizara wakati wanajibu maswali hapa walisema hivi, kwamba wamejiwekea miezi 18 kumaliza tatizo la umeme kwa vijiji vyote vilivyobaki. Hii ni ishara nzuri sana, lakini ni lazima sasa tuangalie umeme tulionao, Mheshimiwa Rais alisema hivi na naomba ninukuu, ukurasa wa nane wa hotuba ya 2015; “Mheshimiwa Spika eneo lingine ni TANESCO, TANESCO pamekuwa ni suala la kukatikakatika kwa umeme mara kwa mara na kuwepo na umeme wa mgao na hilo limelalamikiwa sana na wananchi wetu.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiteto kwa miezi mitatu sasa umeme ni kukatikakatika halafu hatupati taarifa yoyote ile. Sasa wakati tunawekeza huko kutengeneza umeme, lazima sasa tuwe na uhakika wa umeme tulionao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naunga mkono hoja lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante kengele imeshalia

MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na kama walivyosema wenzangu niwape pole sana Wabunge kwa msiba wa Mbunge mwenzetu Engineer Nditiye, tunamuombea Mwenyezi Mungu ailaze mahala pema peponi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda ni mdogo sana naomba nichangie hoja hii kwa kusema hivi Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025 imetaja Kiswahili mara 39 namna tunavyotaka kutumia Kiswahili kwa mustakabali wa Taifa letu. Ukurasa wa 17, 130, 167, 168, 184, 185, 186, 244, 246, 247, 268, 286,287 na 288. Ukisoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi utaona Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alivyofafanua namna tunavyotaka kutumia Kiswahili, kwa Muswada huu utatusaidia kama Taifa kuanza kubadilisha sheria zetu kwa lugha ya Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na nikinukuu tu kwa ruhusa yako ukurasa wa 167; “Kuongeza uwelewa wa wananchi kuhusu sheria mbalimbali kwa kutafsiri sheria 157 kutoka lugha kiingereza kwenda ya lugha ya Kiswahili.” Kwa hiyo, takwa hili la kubadilisha sheria kwenda Kiswahili ni kwa mujibu ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama walivyokwisha kutangulia wengine Kiswahili kwa Taifa letu inatambulisha Taifa, Kiswahili kimetumika katika ujenzi wa Taifa letu hata wakati tunatafuta uhuru Kiswahili kinaleta utamaduni wa Taifa letu. Kiswahili ni sawa sawa na uzalendo, ukombozi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiswahili ni tunu ya Taifa letu. Kwa hiyo, tumpongeze sana Mheshimiwa Rais ni wakati sasa wa muafaka tuanze kuzungumza Kiswahili kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tafiti nyingi zinaonesha nchi nyingi sana Finland, Ireland, Bangladesh, Malaysia, Hong Kong, Hong Kong ilifika mahala wakaanza kuandamana nchi nzima wanakataa kiingereza kisitumike kwa sababu waliokuwa wengi Hong Kong wanazungumza chinese sasa sisi tumeanza hata hata kabla ya Watanzania hawajaanza kuandamana. Lakini sababu nyingine kimsingi sana ya kisheria ni haki ya mtu kufahamu lugha ya mashitaka kwa kiingereza wanaita due process, huwezi kumshitaki mtu ukaleta hati ya mashitaka kwa lugha ya kigeni, haelewei.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nyingine kuna kitu kinaitwa kwa kisheria uhalali wa lugha inayotumia (legitimacy) Watanzania wengi wanaongea Kiswahili kuendelea kuwa na sheria zilizoandikwa kwa lugha za kigeni ni kukosesha legitimacy sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa na lugha ya Kiswahili kwenye sheria zetu, kwanza inajenga uelewa, vilevile inaleta watu kuheshimu sheria kwa sababu wanafahamu sheria kwa Kiswahili, wanafahamu lugha tuliyoandikia sheria. Lakini ukileta sheria zilizoandikwa kwa lugha za kigeni tutakuwa tunawasumbua Watanzania wasipo fuata sheria kwa sababu lugha hiyo imeandikwa ni ya kigeni. Kwa hiyo inaleta obedience, inaleta respect kama unaelewa lugha hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada ulio mbele ya Bunge umeandikwa kwa kiingereza na kanuni zetu zinachanganya by the way na hukumu zetu sasa kama alivyosema Mwenyekiti wa Kamati zimeshaanza kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili, kwa hiyo mabadiliko ya sheria yatarahisisha sana kazi hii ya tafsiri ya sheria zetu ziende kwa lugha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama walivyokwisha kusema wengine nchi zinazozungumza Kiswahili sasa ni Rwanda, Uganda, Burundi, South Sudan, sehemu ya Mawali, Somali, Zambia, Mzumbiji, DRC na Visiwa vya Comoro. Kwa hivyo Kiswahili tayari kina soko kubwa sana ni zaidi ya watu milioni mia mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na 2) wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Nishukuru pia kwa kuwa mchangiaji wa kwanza kwa Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, lakini kabla ya yote niwashukuru sana Wabunge kupitia ule Mfuko wa Faraja kwa support waliyonipa nilipompoteza mzee wangu. Tuendelee kumuombea alale mahali pema peponi.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Katiba na Sheria kwa umahiri mkubwa sana. Sisi ambao tunafanya kazi naye na Wajumbe wenzangu watakubaliana nami kwamba tuna-enjoy leadership yake nzuri sana. Vilevile niwapongeze Wajumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria; nikupongeze, sijui ulitumia nini kuitengeneza timu hii ya Katiba na Sheria, tuna-enjoy sana, it’s a very good team, inaongozwa na Mawakili maarufu sana kama Senior Counsel Tadayo, ana miaka karibu 40 ya practice. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile niwapongeze wadau waliokuja kwenye Kamati ya Katiba na Sheria. Kwa kweli tulijifunza mambo mengi sana kwa wadau wale. Alikuja kijana mmoja mwanasheria kutoka Tangible Initiative anaitwa Kulwa William Mduhu, very young, very brilliant. Tulijifunza mambo mengi sana kupitia kwake na wadau wengine waliokuja kwenye Kamati yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hii inasisitiza tu kama tulivyosema kwenye ripoti ya Kamati kwamba Serikali ihakikishe kwamba inawashirikisha wadau katika marekebisho ya sheria mbalimbali. Tunajifunza mambo mengi sana kutoka kwa wadau. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo mawili au matatu hivi niweke mkazo kwenye ripoti yetu. Nimpongeze Attorney General, Wizara ya Katiba na Sheria na CPD kwa kweli kwa ushirikiano mkubwa waliotoa wakati wa majadiliano kati ya Kamati na timu ya Serikali. Kama alivyosema Mwenyekiti wetu, kati ya vitu ambavyo tulizungumza ambapo kwa kweli msingi wake tulikuwa tunaufahamu, frustration wanayopata Makatibu Wakuu pale ambapo bodi hazipo na amendment iliyokuwa inaletwa ilikuwa ni kujaribu kuongeza muda ili kazi zisikwame lakini baada ya majadiliano tukasema na ni msingi tu wa kisheria kwamba hatuwezi kuongeza muda kwa sababu itakuwa ina-conflict sasa kazi za bodi zikiendelea kufanywa na mtu mmoja for an unlimited time. Kwa hiyo, baada ya mashauriano wakaamua ku-withdraw; that is excellent. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwa kukubaliana na Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya Sheria ya Mawakili ni fursa nzuri sana kwa Mawakili kwa kuwaruhusu Mawakili kwenda kwenye Mahakama za Mwanzo. Mwaka 2016 Bunge lilileta mapendekezo ya kuongeza pecuniary jurisdiction ya property, kusema sasa kwenye Mahakama za Mwanzo unaongeza thamani ya kesi ambazo zinaweza zikasikilizwa na Mahakama za Mwanzo na fear ya mawakili that time ni kama sasa mnawanyang’anya kazi kwa sababu hela nyingi sasa zinakwenda Primary Court na Mawakili hawaruhusiwi kwenda. Kwa hili, I am sure Mawakili watakuwa excited kwamba sasa wanakwenda kwenye Primary Courts, zile kazi ambazo zilikuwa zimefungwa by restriction of law sasa watakwenda, that is excellent.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba tunaleta huduma karibu na wananchi ili wapate fursa ya kusikilizwa na kupata uwakilishi wa Wakili kwenye Primary Courts, mapendekezo haya vilevile yanazungumzia kutengenezwa kwa Bodi hizi za Mikoa zinazo-discipline advocates ili ku- protect society from advocates lakini vilevile ku-protect advocates kwa kuleta process ya kusikiliza zile kesi na malalamiko ya mawakili.

Mheshimiwa Spika, lakini wakili akiwa na cheti chake tukafikiri decision ya kusema sasa huyu wakili hafai na kwamba cheti anyang’anywe isifanywe na Kamati za Kimkoa kwa sababu kwanza composition ya Kamati zile na ile ya Kitaifa ni tofauti. Quality ya watu walioko kwenye National Committees ni Attorney General, DPP na ukiangalia sasa na composition ya wale wa mikoa ambao ni Registrars tusifanye kwamba ni rahisi sana hivi vyeti vikaondolewa kwa sababu watu wamehangaika na kwa kweli lazima viwe protected ziendelee kufanya kazi nyingine hizi za usuluhishi na mwisho wa siku wananchi wawe protected ile kuondoa cheti ibaki kwenye National Committee. Kwa hiyo, I think it is an excellent provision.

Mheshimiwa Spika, suala la nidhamu ni lazima kwa kweli liwe controlled. Hakuna profession ambayo watu wanaweza wakafanya watakalo. Kwa hiyo, kuwa na hizo Disciplinary Committees zitasaidia sana kuondoa malalamiko kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, baada ya marekebisho haya kuna mambo mengi yatabadilika. Nilikuwa naangalia Cheti cha Wakili kikishatengenezwa huwa kinaandikwa hivi na ninaomba ninukuu, kinasema kwamba: “Is an Advocate of the High Court and before the Court’s subordinate thereto save for Primary Courts”

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tumesema Mawakili watakwenda kwenye Primary Courts, Wizara sasa iweke regulations in place ili vyeti vya mawakili from next year iondokane na hilo sharti ili lisilete mapingamizi ya kisheria baada ya sheria hii kupita kwa sababu atakuja mtu ana certificate of practice lakini imeandikwa is an advocate of the High Court and Court’s subordinate thereto save for primary courts. Kwa hiyo, naomba suala hilo lishughulikiwe ili lisilete mkanganyiko wa kisheria.

Mheshimiwa Spika, Kamati imesisitiza kwamba wakati mwingine sheria inatoa mamlaka kwa mamlaka za chini kutengeneza regulations fulani fulani na sisi tukasisitiza kabisa kwamba wakati mwingine hizi mamlaka za chini zijue kabisa kwamba jukumu la kutunga sheria ni la Bunge, kwa hiyo, ziwe very careful kuangalia sheria mama ili wasilete lawama kwa Bunge.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naangalia pia Amendments ya Sheria ya The Land Disputes Courts ya kuruhusu sasa wale Wenyeviti wawe Public Servant na nilikuwa naongea na Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, kwamba Kiteto haina Mwenyekiti, akaniambia tatizo ni hili. Sasa baada ya amendments hizi, naamini Kiteto sasa na wilaya zingine itakuwa mandatory kuwa na hawa Wenyeviti.

Mheshimiwa Spika, nina kitu kidogo tu, siku hizi ukisoma sheria hiyo na inasema na hii sasa inapelekea sheria zetu, siku hizi kuna mjadala unaitwa making laws work for women and men ama gender sensitive legislation. Ukiangalia kifungu kile kinaendelea kusema Chairman, and so on, sasa isituletee mkanganyiko tukafikiri kwamba wanaostahili kuwa Wenyeviti ni wanaume peke yao. Kwa hiyo, hiyo ili tuangalie isije ikaleta nanii fulani hivi.

Mheshimiwa Spika, mabadiliko haya ya sheria yatawezesha mabadiliko makubwa sana na yataleta haki kwa wananchi na yatafanya wananchi wafurahie haki hizi ambazo zimeletwa na mabadiliko ya sheria.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)