Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Edward Olelekaita Kisau (1 total)

MHE. EDWARD K. OLELEKAITA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Jimbo la Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Kisau Olelekaita, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mpango wa kujenga vyuo vya ufundi stadi ikiwa na lengo la kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi katika kila mkoa na kila wilaya. Kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ilitenga jumla ya shilingi bilioni 48.6 kwa ajili ya kujenga vyuo 29 vya VETA katika ngazi za wilaya ambavyo kwa sasa viko katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha ili kuendelea kutekeleza azma yake ya kuwa na chuo cha ufundi stadi katika kila mkoa na wilaya nchini ikiwemo Wilaya ya Kiteto. Aidha, endapo Halmashauri ya Kiteto inayo majengo ambayo yanakidhi vigezo vya kutumika kwa VETA, Wizara yangu itakuwa tayari kununua vifaa kwa ajili ya kuwezesha majengo hayo kuanza kutumika mara moja. Ahsante.